Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi nami kuweza kuchangia katika hoja hii muhimu ya Wizara ya Elimu, Wizara ambayo kwetu sisi vijana ndiyo daraja katika kufikia ndoto, matarajio na maono yetu. Mnamo tarehe 26 Aprili, 2026, nchi yetu imesherehekea miaka 62 ya Muungano. Ni umri wa mtu mzima, ambaye katika utumishi wa umma anapaswa kustaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka 62 nchi yetu imepiga hatua kubwa sana katika eneo la elimu. Tumetoka kuwa na chuo kikuu kimoja cha Dar es Salaam, mpaka kuwa na vyuo vikuu zaidi ya 50. Vilevile tuna vyuo vikuu vya kati zaidi ya 400.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule za msingi na shule za sekondari kuna ongezeko. Hapa ninaomba nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha uongozi wake amejenga shule za sekondari zaidi ya 1,300 na katika kila mkoa amehakikisha kuna shule maalum ya wasichana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia ametutoa kutoka kuwa na shule za amali tano, ametufikisha kuwa na shule za amali 103. Katika shule hizo, shule 29 ni zenye mkondo au mchepuo wa uhandisi. Tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia kwa sababu, licha ya hayo ameendelea kujenga Vyuo vya VETA. Mwaka 2025 kulikuwa na Vyuo vya VETA 1,414, lakini mpaka sasa kuna Vyuo vya VETA 1,446.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ameendelea kujenga Vyuo vya VETA, sasa kuna ujenzi wa vyuo 64 ambavyo vitafanya idadi kuwa vyuo 145. Sambamba na hilo ninaomba niipongeze Wizara ya Elimu, ninampongeza Waziri, Naibu Waziri pamoja na watumishi wote wa Wizara hii kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza maono yake kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio haya yamesababisha kuwa na ongezeko la wahitimu katika vyuo vya kati na pia, vyuo vikuu, lakini licha ya ongezeko hilo na mafanikio hayo, bado wahitimu wetu wana changamoto ya ajira na sababu mojawapo inayochangia changamoto hii ni kukosekana kwa ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kuishauri Serikali yangu ninaomba nikipongeze Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuja na program maalum inayofahamika kama, Skillika, ambayo imelenga kuwajengea uwezo wahitimu, ili wawe na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira. Sambamba na hilo, ninaipongeza Serikali yangu kwa sababu, imewekeza kiasi cha shilingi 175,000,000,000 katika mradi wa kimkakati wa kukuza ujuzi unaofahamika kama E-STRIP. Mradi huu unatekelezwa katika Chuo cha NIT, DIT na ATC, ninaipongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninajikita katika kuishauri Serikali yangu. Kama ambavyo Serikali na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimetuonesha njia ya kuanzisha program kama hizi, naishauri Serikali kuanzisha program kama hizi katika ngazi mbalimbali za elimu na pia, kutumia wataalam wenye uzoefu na taaluma katika kuwafunza watu ambao tunawategemea, wawe na ujuzi ambao unatakiwa kwenye soko la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea kama Jordan na Singapore wanatumia industrial driven curricula, ambapo wao wanafanya review ya kozi zao kila mara. Sambamba na hilo wameanzisha baraza la elimu la tathmini, ambapo linafanya kazi ya kutathmini na kutafiti kama ujuzi ambao wanautoa katika vyuo vyao unaendana na kile ambacho kinahitajika katika soko la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nchi za Ujerumani, Uswiss na Austria nazo zinaenda na system inaitwa duos education model, ambapo wao wanafunzi wao wanaenda darasani siku nne za wiki, lakini siku tatu wanaenda kufanya practical. Hii haiwaongezei ujuzi tu vijana, bali pia, inawasaidia kupata kipato, ili watakapotoka katika vyuo waweze kujiajiri. Sambamba na hilo ninaomba kuishauri Serikali yangu kuongeza asilimia za uwekezaji katika elimu inayotokana na GDP ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, UNESCO inashauri na kupendekeza kwamba, Mataifa yawekeze asilimia nne hadi sita ya pato la Taifa, yaani GDP, katika elimu. Mpaka sasa Tanzania tunawekeza 3.3% hivyo, ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa, Serikali yangu iweze kuongeza kiasi cha kuwekeza katika sekta yetu ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee suala zima la wahitimu wa shahada ya uzamili ambayo inatokana na career path. Tumekuwa na mtazamo wa kwamba, wahitimu au wataalam hawa wanatakiwa kuwa na taaluma moja kwa muda mrefu, lakini tumesahau kwamba, changamoto za kisasa zimekuwa zikijikita katika taaluma mbalimbali hivyo, ninawaomba waajiri na taasisi zetu, pale ambapo mtu anaenda kujiendeleza kupitia shahada ya uzamili, basi wasiyone kama amepoteza mwelekeo wa taaluma kwa sababu, tunahitaji watu ambao wako multiskilled, lakini pia, wako multidisciplinary, ili waweze ku-solve matatizo ya wananchi kwa mitazamo mipana zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipongeza Serikali kwa kuendelea kujenga Vyuo vya VETA. Ninazidi kuihimiza Serikali, ajira nyingi zinatokana na sekta ya uzalishaji, sekta ya ufundi na pia, sekta ya ujenzi; ajira hizi zinahitaji watu ambao ni ma-technician, watu ambao wana ujuzi wa vitendo na mafundi study. Hivyo tukiendelea na kufanya mchakato wa kujenga Vyuo vya VETA ndani ya muda mfupi tutasaidia vijana wetu kupata ajira za haraka kwa kipindi cha muda mfupi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ahsante sana.