Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza jioni hii ya leo. Kwanza kabisa ninaanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuleta mabadiliko na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia, kwa kuendelea kumwamini Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, Katibu wake Profesa Caroline Nombo na wasaidizi wao kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia utekelezaji wa sera na mitaala mipya iliyoboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza tuanze kwa kukumbushana mwaka 1967, Mwalimu Julius Nyerere alikuja na Sera ya Elimu ya kujitegemea, ambayo lengo lake ilikuwa ni kujaribu kufuta mfumo wa kikoloni tuliokuwa tumeurithi na kutaka Watanzania, Vijana wa Kitanzania, walioelimika waweze kuwa na ujuzi wa kuweza kujiajiri, Ndipo aliposema kijana anapomaliza darasa la saba awe angalau na ujuzi mmoja wa kuweza kuutumia akirudi nyumbani, lakini utekelezaji wa elimu hiyo ya kujitegemea haukuweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na alipomaliza madaraka ndiyo ikafa kabisa tukarudi kwenye masuala ya nadharia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia malengo yake ya wakati ule ndiyo valid mpaka sasa hivi kwa sababu, tunataka kuwa na Dira hii ya Mwaka 2050; tunataka kuwa na Taifa la watu wanaojitegemea, walioelimika na wenye ujuzi mbalimbali na wanaochangia katika kuleta uchumi. Sasa Profesa Ishumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alifanya analysis hivi karibuni akasema ni kwa nini, kama Taifa, tulishindwa kutekeleza elimu ya kujitegemea. Hatukuweza kuwa na nyenzo iliyoweza kutu-guide vizuri tutoke wapi, twende wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani mwaka 2021 alikuta kuna malalamiko. Watanzania wengi walikuwa wanalalamika kwamba, elimu yetu haina msaada kwa vijana, hawapati ajira na hawezi kujiajiri. Ndipo alipoielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Profesa Mkenda na Katibu wake Profesa Carolyne Nombo, kutafuta nini kifanyike, ili Watanzania waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Mkenda kwa kushirikiana na wataalam wengine wasomi Tanzania, walipitia ile Sera ya Mwaka 2014 iliyokuwa imeshindikana ndiyo wakaja na Sera iliyoboreshwa ya Mwaka 2023; hoja na mitaala imeboreshwa, ambayo inakwenda kuwa mwarobaini wa tatizo la ukosefu wa ajira, kwa hilo, tuwapongeze tuwape maua yao, wengi walishindwa kufanya hivyo. Ukiangalia hata Sera ile ya Mwaka 2014 ilishindwa kutekelezeka kwa sababu, inahitaji matumizi makubwa ya fedha, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuweka fedha nyingi baada ya kuanza kutekeleza hii sera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawapongeza hata Wizara hapa leo wamekuja na bajeti ya 2.3 trillion na ukiangalia kwa kiasi kikubwa inakwenda katika kutekeleza hiyo sera, wamesema ni miongoni mwa mambo ambayo wanayapa kipaumbele. Baada ya kukubali kuanza kutekeleza ile sera wamewekeza fedha nyingi sana; ile sera, pamoja na mambo mengine inaelekeza uhuishaji wa amali na pia, elimu ibadilike iwe ya miaka 10, lakini ime-focus zaidi katika masuala ya sayansi, TEHAMA na hisabati na hayo ndiyo mambo yanayotupeleka kwenye Taifa lenye uchumi. Baada ya kufanya hivyo tayari shule 103 za amali zimeshajengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 90, ambapo Watoto wetu sasa wanaenda kusoma kwenye shule za amali. Kuna shule 158 zinatekeleza mkondo wa amali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sasa tunapokwenda kwenye hii dira ninatamani nione watu wa Wizara ya Fedha wakiwa humu ndani, pamoja na watu wa mipango kwa sababu, bila kusomesha hawa Watanzania hiyo Dira ya 2050 haitafanikiwa. Hatutaweza kutekeleza Dira ya 5020 kwa kutumia Wachina na Wahindi, tunatakiwa tutumie vijana wetu watakaosoma kwenye VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli Mwalimu Nyeyere aliwahi kusema mficha maradhi kilio kitamfichua kwa hiyo, tukiangalia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuta VETA zinasuasua alielekeza shilingi bilioni 100 zipatikane, ili VETA hizi ziweze kukamilika. Mpaka sasa hivi tunavyokwenda VETA 64 zipo 67% na ile VETA moja ya Songea ipo 68%. Fedha bado zinahitajika, bila kufanya maamuzi magumu itafika tena mwaka kesho VETA itakuwa bado zipo vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha nia, basi wanasema great leaders inspires everyone to take action, kwa hiyo, tunaamini sasa hivi Mheshimiwa Dkt. Samia ametu-inspire. Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango na Tume ya Mipango, kama kweli, wanataka Dira ya 2050 iweze kutekelezeka, basi watenge fedha ziende kwenye VETA, ili tuweze kuongeza ajira kwa sababu, five years development plan inasema tuongeze ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana watenge fedha ziende kuongeza ajira, bila VETA kukamilika, ajira hazitapatikana, VETA ndiyo habari ya mjini, ujuzi na ajira. Sasa, ili tukamilishe hii awamu tunahitaji shilingi bilioni 38.9 tufanye maamuzi ya makusudi tutenge shilingi bilioni 38.9, ili VETA zikamilike, Vijana wa Kitanzania waweze kuzitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza pia Wizara ya Elimu kwa kujenga majengo mengi; madarasa mengi mapya, matundu ya vyoo mengi, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Pia, maabara nyingi, shule nyingi mpya za msingi, za sekondari na za awali zimejengwa na hiyo imesababisha kuongezeka kwa ajira. Mheshimiwa Dkt. Samia ameajiri walimu wengi wa awali mpaka vyuo vikuu, tuwape pongezi zao kwa kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo imesababisha pia, ufaulu na udahili umeongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Ukija kuangalia uandikishaji kwenye ngazi ya vyuo vya juu, tumeongeza kwa 43%, lakini ukilinganisha na nchi za Afrika Mashariki, bado tupo chini kwenye gross enrolment rate. Sasa nini kifanyike?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuipongeze Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Elimu kwa kujenga campus 16 katika kila Mkoa, zitakapokamilika inasemekana zitaongeza enrolment ya wanafunzi 100,000. Hii itasaidia sana kuongeza gross enrolment rate, ambayo ni direct repercussiyon ya GDP per capita, kwa hiyo, watu wa Tume ya Mipango na Fedha ni vizuri tukawekeza sana kwenye Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ni kama unavyojenga ghorofa, msingi wa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwenye Taifa hili miaka mitano hii tuwekeze kwenye Wizara ya Nishati, Wizara ya Elimu, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na VETA zetu lazima zisomeshe wataalam, ambao watakwenda kusaidia kutengeneza matrekta, kuwe na ufundi, kwa ajili ya stakabadhi ghalani na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza pia, Wizara ya Elimu kwa kuja na ubunifu wa kuanzisha scholarships mbalimbali; Samia Scholarship, wanafunzi zaidi ya 2,000 wanasoma. Hongera sana Mheshimiwa Profesa Mkenda na wenzako. Samia Extended Scholarship tumepeleka zaidi wanafunzi nje; Mataifa mengi yaliyoendelea katika kuendeleza human capital pia, yanapeleka wanafunzi wengi nje ya nchi. Ninaomba tuongeze fedha, ili wanafunzi wengi zaidi waweze kwenda huko. Pia, ninampongeza kwa kuanzisha Samia Innovation and Commercialization Fund, ambayo inasaidia kuboresha ubunifu. Nadhani hii nayo ikiendelea kupewa kipaumbele, italeta mafanikio makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, tunajua kutokana na utekelezaji wa sera, mwaka kesho, mwaka 2028, tunakwenda kuwa na wanafunzi 3,021,177 zinahitajika fedha shilingi 1.77 trillion. Sasa nimeangalia kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa wanatenga shilingi bilioni 136, Serikali Kuu inatenga shilingi bilioni saba. Kwa hiyo, inabidi tujitahidi kuongeza kasi kubwa, ili hizi shule ziweze kukamilika, vinginevyo itakuwa ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuhakikisha kwamba, fedha zinapatikana, ili shule ziweze kujengwa. Kwa kufuatia hilo, katika Wilaya yangu ya Butiama, Shule ya Sekondari ya Isaba, Shule ya Sekondari ya Mwibagi na Shule ya Sekondari ya Misanga, tunaomba sana fedha zipatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninarudia kusisitiza kwamba, tuwekeze fedha nyingi kwenye VETA, itakuwa mwarobaini wa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)