Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya elimu. Kwanza niwapongeze Mawaziri wanafanya kazi kubwa sana na ni wanyenyekevu akiwepo na Naibu Waziri, Mjumbe mwenzangu wa Baraza la 2008. Mimi nimekuwa kwenye Bunge hili, nikimaliza hii ni term ya nne. Ninaomba niwaambie kama kuna mtu ameleta mapinduzi kwenye sekta ya elimu ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa alisema, adui yetu wa kupambana naye ni ujinga, maradhi na umaskini. Hayo yote misingi yake unaipata kwenye Wizara ya Elimu. Kwenye kipindi chote, bajeti hii haijawahi kufika 1,000,000,000,000. Leo tunazungumzia shilingi trilioni 2.3 kwenda kwenye sekta ya elimu. Tunatenga pesa hizi unataka kuelimisha watu wako, kwenye vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi, kwenye vyuo vya kati, kwenye vyuo vya ufundi na kwenye vyuo vya VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maandalizi ya kujenga Taifa lenye weledi, Taifa litakalojenga nchi yao wenyewe. Kwenye hizi trilioni mbili, trilioni 1.6 ni kwenye miradi ya maendeleo kwenda kuwekeza kwenye elimu, kwenda kujenga Taifa la wasomi, kwenda kujenga vijana watakaojenga nchi yao. Bajeti hii tumesema tunataka kujikomboa kifikra, kwenye pesa zote 359,000,000,000 sawa na asilimia tatu ndiyo inatoka nje, lakini trilioni 2.3 zote ni pesa za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe kupitia Wizara ya Fedha, tunataka kujenga Taifa letu, kuwekeza kwa watoto wetu kupitia pesa zetu za ndani. Bunge hili, tuiombe Wizara ya Fedha, kuhakikisha pesa hizi zinatoka ili watoto wetu tunaokwenda kuwapeleka kusoma nje ya nchi, kutengeneza wanasayansi, wawe na uhakika wa kwenda, ili mpango wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kujenga kampasi kila mkoa, iweze kutekelezwa na kwenye bajeti nimeona inaanza Mara, Tanga na Kagera. Mwanzo wa utekelezaji wa Ilani unaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wabunge tuhakikishe tunaibana Serikali itoe hizi pesa, ili dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutengeneza Taifa lenye ujuzi, kutengeneza Taifa la wasomi, kutengeneza wanasayansi wetu, ambao ndiyo dunia ilipo. Kujenga mifumo yetu, ambayo itaendeshwa na watu wetu, ndiyo maana pesa hizi zimetengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumza kwenye mpango, mataifa yote yaliyoendelea yali-invest kwenye vyuo vya kati, yali-invest kwenye VETA, ndiyo bajeti hii inavyosema, ili ule mpango wetu wa Dira ya 2050 ndiyo unaanza kujengwa hapa, kutengeneza vijana watakaopelekwa kwenye viwanda, kuijenga nchi yao. Tunaenda kwenye soko la ushindani wa elimu. Soko la ushindani la kupeleka wataalamu duniani, huwezi ukatengenezwa na nchi nyingine, wanajengwa na Watanzania wenyewe. Ndiyo maana nchi hii, iliweza kutoa viongozi wazalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa ni mtoto wa maskini kutoka pale Butiama aliandaliwa na nchi yake. Hayati Mheshimiwa Benjamin Mkapa ni mtoto wa maskini, kutoka kule Lindi, Mtwara, aliandaliwa na nchi yake, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kutoka Msoga aliandaliwa na nchi yake. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli watoto wa maskini kabisa, waliandaliwa na nchi yao, ni misingi ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumepiga hatua, kwenye Bodi ya Mikopo tumetoka 70,000,000,000 mpaka zaidi ya 900,000,000,000 na kitu. Ninaungana na hoja ya mdogo wangu Asha. Lazima tubadilishe Mfumo wa Bodi ya Mikopo, tutoke kwenye Bodi ya Mikopo uwe mfumo maalum, tutakaoutungia sheria utakaokuwa na chanzo chake. Tuwe tuna uhakika wa kupata fedha, Mheshimiwa Waziri tulifanikiwa hayo kwenye Mfuko wa Maji, tulifanikiwa hayo kwenye Mfuko wa Barabara, tumefanikiwa hayo kwenye Mfuko wa REA, tumefanikiwa kwenye Bima ya Afya, tunaweza kwenye elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hatutakuwa na kusema wale vijana wetu hawarudishi mikopo ya kwa wakati, hawarudishi mikopo kwa wakati kwa sababu walikuwa hawakupata ajira. Haitazuia Mfuko huu usiendelee, kutoa mikopo kwa watoto maskini, kwa sababu tutakuwa tuna uhakika wa kupata pesa nzuri, kupata pesa za kutosha bila kutegemea ruzuku ya Serikali peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wengi wa maskini kama hao ambao Mheshimiwa Dkt. Samia, anatoa Samia scholarship, wa Manyamanyama, wa Tanga, wa wapi, wote watapata fursa ya kusoma kwa sababu kutakuwa kuna Mfuko Maalum, siyo tu kuanza chuo kikuu na mpaka kumaliza masomo yao. Kwa unyenyekevu mkubwa Waheshimiwa Wabunge, tuiunge bajeti hii ndiyo mpango unaanza kutekeleza Dira, lakini tunatengeneza wataalam wetu watakaolijenga Taifa lao kwa uzalendo mkubwa, kwa sababu hawajasomeshwa wenyewe wamesomeshwa na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)