Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASHA J. FERUZ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Kwanza kabisa ninapenda kuchukua fursa hii kuipongeza sana Wizara kwa utekelezaji mzuri wa bajeti inayokwisha. Hakika Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wamefanya kazi nzuri sana na tunaendelea kuwapa ushirikiano tufikishe malengo ya Dira ya 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nielekeze pongezi zangu kwa Wizara na hasa kwa Mheshimiwa Rais kwa kuweza kutoa fursa kwa upatikanaji na utoaji wa ujuzi kwa vijana katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo. Tulikuwa tuna vyuo 1414, lakini sasa tuna vyuo 1446, hii ni hatua kubwa sana. Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi, amewekeza ili vijana wetu waweze kupata ujuzi na kuweza kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna vyuo vya ufundi 532, lakini tuna vyuo vya ufundi stadi 914. Unaweza kuona ni kwa namna gani sasa vyuo vyetu vimeongezeka, hata VETA pia, kutoka VETA 80 hadi VETA 145. Hakika hii ni hatua kubwa sana, tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais amefanya uwekezaji mkubwa, ambao utakwenda kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza pia Wizara kwa mpango niliouona kwenye bajeti ya 2026/2027, inakwenda kuwekeza fedha nyingi bilioni 250, kwa kuanzisha polytechnical colleges tano kubwa maeneo ya Morogoro, Kigoma, Mwanza, Mtwara na Unguja. Hakika wameyaishi maono ya Mheshimiwa Rais, tunawatakia utekelezaji mwema na kwa kutangulia tu niseme hoja hii mimi itaiunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niielekeze mchango wangu wa ushauri na maoni katika eneo la Bodi ya Mikopo. Bodi hiyo wakati inaanza ilianza kwa 70,000,000,000 sasa tuna 917,000,000,000 tulikofikia. Mchango wangu ninauelekeza kuhusu mageuzi ya Bodi hii ya Mikopo. Kweli bodi inafanya kazi kubwa, lakini uhitaji wa wanafunzi kupata mkopo ni mkubwa. Fedha ama ruzuku tunayoipata haitoshelezi kuwapa wahitaji wote. Sasa ninashauri nini kifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Bodi hii tubadilishe kutoka kwenye Bodi ya Mikopo kwenda kwenye Mfuko, ili tuweze kuipatia sheria Bodi hii au Mfuko huu tutakaouanzisha, uweze kujitanua katika eneo la kupata mapato. Kitendo cha kuendelea kusubiri chanzo kimoja cha fedha kinafanya watoto wa wanyonge, watoto wa wakulima kukosa mkopo. Tukiifanya Bodi hii kuelekea katika Mfuko, kwanza tutaipa nafasi ya kuanzisha vyanzo vyake vingine vya mapato, kwa hali iliyoko sasa hivi bodi haijitoshelezi katika utoaji wa huduma na inategemea ruzuku ya Serikali. Pia, haitumii fursa za wawekezaji na ubunifu za kifedha zilizopo nchini. Hakuna engagement ya private partnership. Tukifanya hivyo kubadilisha kutoka kwenye Bodi kwenda kwenye Mfuko itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie mfano, jana Mheshimiwa Aweso alitupa mfano wa namna Tanga walivyoweza kutumia maji na kuweka bonds wakapata faida. Sisi tunaweza kutumia kwenye elimu, lakini pia tuangalie Mfuko wa Bima ya Afya, watu wanawekeza baadaye anaweza kutibiwa. Pia, kwenye elimu mtu anaweza akawekeza kuanzia mwanzo, akaja akatumia mbele kule, lakini pesa ile inavyoingia itaendelea kusaidia watu wengine ambao wakati huo bado wanahitaji mkopo na wakasoma vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi ada yake ni shilingi milioni nne, lakini bodi inampa shilingi laki saba au laki sita. Mtoto huyu wa maskini anashindwa kuendelea na masomo, kwa sababu ule mkopo alioupata katika ada yake haujafika hata nusu na mzazi hawezi kuhimili hizo gharama. Tunaendelea kusisitiza wanafunzi wasome sayansi, akienda kusoma labda fani za udaktari, ada ni kubwa, kwa hiyo tunakuwa hatumsaidii huyu mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni heri sasa tujielekeze mkopo wa wanafunzi. Ninajua katika pesa ya kujikimu ile boom wanapata sawa, lakini kwenye ada pesa ni ndogo, wanafunzi wanashindwa kujikimu. Kwa hiyo, ninashauri hapo kwenye pesa ya ada atleast tuwape nusu ya ada, hiyo ndiyo namna ya kumsaidia mwanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili niuelekeze kwa wahadhiri. Wahadhiri waliopo chini ya TCU na wahadhiri waliopo chini ya NACTVET, wahadhiri hawa wanatofautiana maslahi. Mhadhiri wa TCU na Mhadhiri aliyepo chini ya NACTVET wanatofautiana hata mshahara, lakini wote ni wahadhiri. Ninazungumza kwa upande wa Wahadhiri Waandamizi, madaktari, associate professors and professors. Hii siyo sawa, kazi ya hawa watu wote ni kazi tatu za msingi. Kazi ya kwanza ni kufundisha, kazi ya pili ni kufanya tafiti na kazi ya tatu ni kutoa machapisho. Wote waliopo TCU na walioko na NACTVET wanafanya kazi hizi, kwa nini, kwenye maslahi tuwatofautishe? Mimi binafsi ninaona iko haja ya Serikali kufanya marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa pia wanatofautiana hata kwenye muda wa kustaafu. Hawa watu waliopo chini ya TCU wanastaafu wakiwa na miaka 65, lakini yule aliopo chini ya NACTVET anastaafu kwa miaka 60. Kwa nini? Ninaomba Wizara ya Elimu washirikiane na Wizara ya Utumishi, kuona ni namna gani eneo hili linarekebishwa. Hii inawafanya watumishi hawa waliopo chini ya NACTVET wanakuwa wanyonge, tunawadogosha, lakini tunaamini kwamba taaluma zao zinaisaidia jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wahadhiri ambao wapo chini ya NACTVET wakichapisha machapisho yao kwenye tovuti ambazo vyuo viko chini ya TCU, machapisho yao yanakataliwa yanakuwa dropped. Kwa nini? Si sawa, sisi wahadhiri tunaona hii haiendi sawa. Tuone haja na sababu sasa ya kurekebisha eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kushauri Serikali itoe jicho la tatu, katika vyuo ambavyo vinatoa kozi ya afya. Nitatoa mfano Chuo cha MUHAS, hakina hospitali yake inayoimiliki na ni chuo cha Serikali. Ni kweli wanafunzi wa MUHAS wanategemea Hospitali ya Muhimbili na sote tunafahamu kuwa, Muhimbili ni taasisi inayojitegemea na MUHAS ni taasisi inayojitegemea. Kwa hiyo, iko haja sasa, ninashauri Serikali ione umuhimu wa kuipa MUHAS, Hospitali ya Mloganzila kama hospitali yao ya mafunzo. Hii itasaidia kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, wapo wanafunzi ambao hawawezi kufanya mitihani ya mwisho, wakizuiliwa na uongozi wa vyuo vyao kwa kigezo cha kukosa ada. Hii si sawa. Haki ya mwanafunzi ni katika kusoma pamoja na kufanya mitihani yake. Hili lipo Mheshimiwa Waziri. Vipo baadhi ya vyuo vinazuia wanafunzi kufanya mitihani ya mwisho, end of semester exams kwa kigezo cha kwamba hajamaliza ada. Upo mchakato mrefu katika kusoma, kuna tests, kuna assignemts, walikuwa wapi kuwabana kule. Mwanafunzi akajibana, anafika end of semester kufanya mtihani anazuiliwa. Kwa hili, tunaona haliendi sawa na wanafunzi pia waangaliwe, kwa sababu ndiyo wataalam tunaowazalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika eneo hili la wanafunzi, vipo vyuo vinatoa kada ambazo hazipo kwenye Sekretarieti ya Ajira. Mwanafunzi ameomba chuo, Serikali imemkubalia, ameomba mkopo, akapewa mkopo, akasoma akamaliza. Matarajio yake ni kuajirika, anapoingia kwenye Sekretarieti ya Ajira, anakuta kada aliyoisomea haipo. Anayeidhinisha kada hizi ni sisi Serikali, kwa maana ya kwamba Wizara ya Elimu, ndiyo wanatoa ruhusa ya kwenda ku-implement ile kozi ambayo inafundishwa kwenye chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya Utumishi washirikiane, zile kada ambazo hazipo kwenye Sekretarieti ya Ajira ziingizwe. Ni maumivu makubwa kwa mwananchi ama mzazi kule kijijini kwetu, ambako anamsaidia mwanafunzi, kuweza kusoma, anamaliza, ana matarajio makubwa, halafu mwanafunzi yule haajiriki inaumiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)