Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia muda wa kuchangia bajeti ya Wizara hii. Labda nianzie mwisho, wakati nikiwa ninachangia nina mapendekezo 14. Kwa hiyo, ukiniona ninafika la 10 unajua ninakaribia kumaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, hii Wizara tunavyoongelea Dira ya 2050 tulionesha umuhimu wa Wizara ya Nishati na nishati kuhitajika, lakini sasa kuendesha uchumi na hayo tuliyoyatarajia kufika mwaka 2050, kila kitu kipo kwenye Wizara hii. Ni kwamba na watakumbuka kwenye mchango wangu niliwaeleza ile formular ya mafanikio na ustawi wa mataifa duniani. Sasa leo siwezi kuirudia kama wamesahau waningoje mpaka wakati wa bajeti ndiyo nitairudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa cha muhimu ni kwamba safari yetu ya 2050 ni lazima tuwe na uchumi unaokua kwa kasi zaidi ya 10% na ni lazima uendeshwe na watu wajuzi (Knowledge Economy) bila hiyo hatuwezi kuvuka na hiyo ndiyo China ilifanywa mwaka 1978. Ninakumbuka wakati ninaenda kusoma lugha kule Ujerumani ninakutana na Wachina wamemwagwa huko wengi, kumbe walikuwa wanajitayarishwa kwa ajili ya mapinduzi ya uchumi nchini mwao. Mheshimiwa Waziri unafanya vizuri hii ya kupeleka vijana kwenye vyuo vikubwa vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sisi wajibu wetu kutathmini mfumo wa elimu tuliopewa; mfumo wa elimu wa Tanzania mpya ambao tunaishia darasa la sita badala ya darasa la saba. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nimemfanyia homework kumrahisishia majibu. Je, mfumo wetu tuliouchukua ni mzuri? Miaka sita shule ya msingi, miaka minne shule ya sekondari, miaka miwili high school na miaka minne chuo kikuu. Waheshimiwa Wabunge na sisi tutathmini. Sasa hiyo kazi nimeifanya na Watanzania wengi walikuwa na wasiwasi kwamba kuishia la sita huenda ndiyo elimu yetu inaenda kudorora kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hapo niongee ya jimboni mwangu kwamba, Jimbo la Musoma Vijijini tunaenda vizuri kwa sababu sisi tuna shule za msingi 120, tuna sekondari 32 halafu, tuna sekondari ya amali moja na sasa hivi tunajenga sekondari kila kijiji. Kwa hiyo, ninapeleka shukrani zangu nyingi kwa Serikali na kwa Mheshimiwa Rais kama kweli wanataka tutoe mfano wa elimu bora ni Musoma Vijijini. Tunajenga maabara kwenye kila sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Waheshimiwa turudi kwenye mfumo wa elimu; Tanzania tumeenda sita, nne, mbili, nne, kwa mwaka huu mifumo ya elimu ambayo ni bora kabisa duniani (Top Performing Education Systems in the World, the best in the World) ya kwanza ni Singapore yenyewe ina madarasa sita, matatu, matatu, manne (6,3,3,4). Kwa hiyo, mwanafunzi anasoma miaka 12 kabla ya kwenda chuo kikuu. Sisi Tanzania tuna sita, nne, mbili, nne. Kwa hiyo, Mheshimiwa Profesa Mkenda na timu yake hawajafanya vibaya ni sita ongeza nne ongeza mbili, 12. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nchi ya pili yenye mfumo bora kabisa duniani ni Japan. Yenyewe ina sita, tatu, tatu, nne (6,3,3,4). Ndugu zangu nisiwe ninarudia yaani sita ni primary school, mitatu ni junior secondary school, mitatu senior secondary school na minne university, kwa hiyo sitorudia nitaenda kwa hiyo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Finland ni ya tatu duniani yenyewe ina tisa, tatu, tatu. Yenyewe miaka 12 kabla ya chuo kikuu. Ya nne duniani ni South Korea ina sita, tatu, tatu, nne. Ya tano, ni Canada wanafungana na Switzerland ina sita, sita, nne. Kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na hata kule Musoma Vijijini ndugu zangu walikuwa wanasema Profesa hii ya darasa la sita, ninawathibitishia tuko sahihi, hatujaharibikiwa na kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya miaka sita kuna ile ya shule ya awali kindergarten. Hiyo inategemeana na umri wa mwanafunzi na ni kama Tanzania ni kati ya mwaka mmoja mpaka miwili kutegemeana na umri wa huyo kijana anayepelekwa kwenye hiyo shule ya kindergarten.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kipimo cha pili kama tunaenda vizuri. Hiki ndicho ninaomba Profesa na timu yake hiki hatujakifanya, tukifanye. Last time niliwaeleza, lakini ninadhani safari hii, yaani sasa kila mtu anasema ana mfumo mzuri. Sasa upi mfumo mzuri zaidi ya mwingine kimataifa, kuna kupimana na yanaenda kupitia mashindano ya wanafunzi duniani na sisi inabidi tukashindane huko, mfumo wetu hauna matatizo, sasa tuone ubora wake ili tuboreshe na mashindano haya yanafanywa na wanafunzi. Bado, bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwanza inaitwa Program for International Student Assessment (PISA) miaka 15 wanafunzi wanashindana kusoma hisabati na sayansi; ya pili, inaitwa Trains in International Mathematics and Science Study; na ya tatu, ni Progress in International Reading Literacy Study. Kwa hiyo, hizi tatu bajeti ijayo ninaomba Mheshimiwa Waziri akija atueleze vijana wetu wameenda huko wamefanyaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipimo kingine ni kipimo cha kila Taifa lilivyoelimika (The Most Educated Countries in the World). Kwa mwaka huu 2026 ya kwanza ni Canada. Maana yake ni kwamba 65% ya watu wenye umri mkubwa wa Canada walimaliza masomo ya sekondari wakaenda kupata mafunzo, wakapata vyeti baada ya sekondari (Tertiary Qualification);

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili, ni Ireland; ya tatu, ni South Korea; na ya nne, ni Uingereza na ndiyo mtindo tunaoutumia. Uingereza 54% ya watu wenye umri kati ya miaka 25 na 64 wameenda kupata masomo zaidi ya masomo ya sekondari. Kwa hiyo, hii Watanzania nayo tujipime Tertiary Qualification kama tunazo, kwa hiyo, hatujaenda vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaanza mapendekezo; pendekezo la kwanza, kwa Mwaka huu wa Fedha 2025/2026, tuna wanafunzi kutoka form one mpaka form six milioni 3.43. Ninapendekeza angalau 50% ya hawa wanafunzi wawe wanasoma masomo ya sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la pili, tujenge maabara kwenye shule zetu zote za sekondari; pendekezo la tatu, na hili ni muhimu. La tatu, hili kwenye kila maabara zetu za sekondari lazima tuwe na Technicians ambao ndiyo wanaendesha hizo experiments siyo walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninasoma Mara Sekondari nilikuwa na Technician, wakati wote nitakayokwenda kufanya majaribio ananifungulia bila hata Mwalimu kuwepo; pendekezo la nne, tunapaswa kuwa na maktaba zenye kompyuta. Hizi kompyuta ni muhimu kwenye maktaba kwa sababu vinapatikana vitabu ambavyo hununui chochote viko online badala ya kung’ang’ana kuagiza vitabu; pendekezo la tano, ni uhusiano...

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ooh ninamalizia. Pendekezo la tano, ni uwiano kati ya walimu na wanafunzi yaani ukubwa wa madarasa yetu. Kwa kuwa fedha ni matatizo turudi ile ya zamani niliyosoma mimi, shule za msingi watu 45 darasani, sekondari 35 na high school 25. Hii sayansi ni lazima tutafute walimu wengi wa sayansi kwa sababu ukiangalia Physics yenyewe ina branch tisa, Chemistry ina branch 10, Hesabu ina branch sita, Biology ina branch nane. Kwa hiyo, ndugu zangu tunahitaji walimu wengi wa sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la sita, tunataka tuwe na Technical Schools, Secondary Schools kama ilivyokuwa Ifunda na Moshi. La saba, muhimu sana VETA ishuke, kila halmashauri iwe na VETA moja. Pendelezo la nane, ninakaribia kumaliza. Pendekezo la nane, tuwe na Technical Colleges ambazo tunaita Polytechnics ambayo mfano wake ni kama ile ya zamani Dar es Salaam Technical College. Pendekezo la tisa, tuwe na vyuo vya aina mbili, vyuo vya kawaida kama vya Dar es Salaam halafu tuwe na...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Profesa muda wako umekwisha.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia tu hapo.

MWENYEKITI: Ninaomba umalize.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwisho kwenye kumalizia, mwisho tuweke hela kwenye utafiti na tutumie percent moja ya GDP. La kumi na moja, course take nilipendekeza lazima iwe foundation. La kumi na mbili, Wizara itusaidie Vyama vya Kitaaluma vimekufa nchini yaani kama Vyama vya Chemists, vya Physicists na Mathematicians vifufuliwe. La kumi na tatu, Profesa mhimize sekta ya universities zianze kuwa na endowment, yaani pesa zilizotunzwa kusaidia mambo ya utafiti na nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukichukua chuo kikubwa kama cha Harvard endowment yake (hela iliyotunza kwa matumizi yake) ni dola 55,000,000,000, halafu ukichukua cha Texas wana 45,000,000,000. Kwa hiyo, hivi vyuo viwili vya Marekani, Harvard na Texas vina 100,000,000,000 zimetunzwa zinazidi bajeti yetu ya 95,000,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni kwamba Dira yetu ya Maendeleo ili tufanikiwe ni lazima tuwekeze kwenye masomo ya Sayansi. Ni lazima ...

MWENYEKITI: Profesa, ahsante sana.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. (Makofi)