Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninaomba nami kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha, kutuongoza na kuendesha mjadala huu wa kujadili bajeti ya ofisi yangu katika hali nzuri kama hii ambayo tumeona leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninaomba kukushukuru wewe pamoja na Wenyeviti wote, bila kumsahau Mheshimiwa Spika wa Bunge letu na Mheshimiwa Naibu Spika kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendelea kutuongoza. Kwa hakika ninarudia tena, kama nilivyosema asubuhi, mjadala juu ya Mafungu Saba ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma yamejadiliwa vizuri na wizara kupitia ofisi yangu, imeyasikia yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee ninaomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na wale ambao hawakuchangia, kwani kwa namna moja wote wameunga mkono hoja tuliyoiwasilisha katika Bunge lako Tukufu, lenye lengo la kuwezesha utekelezaji wa majukumu tuliyokabidhiwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; sambamba na kutatua changamoto za waajiri, watumishi wa umma na maeneo mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yetu leo imechangiwa na wachangiaji 16; kati ya hao 14 wamechangia kwa sauti kupitia kikao hiki, lakini wawili wameandika kwa njia ya maandishi. Kwa hiyo ninawashukuru sana kwa michango yao yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhitimisha hoja hii, ninaomba kusema maneno machache yafuatayo kabla sijaanza kujibu hoja zilizoelezwa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi yangu inahusika na masuala mtambuka yanayohusisha Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Serikali hutekeleza majukumu haya muhimu kupitia taasisi za umma zaidi ya 570 kupitia watumishi wa umma ambao ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huu, bajeti iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu itaiwezesha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutekeleza majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na utendaji wa taasisi zote za umma na Serikali kwa jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mambo hayo, Serikali itayapa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2026/2027, ambayo ni pamoja na kusimamia nidhamu, utendaji kazi wenye tija, uwajibikaji wa hiari, usimamizi thabiti wa rasilimali watu na rasilimali fedha, matumizi ya mifumo, teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma, mapambano dhidi ya rushwa, kuongeza wigo wa ajira na kuimarisha maadili ya viongozi na watumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya ofisi yangu ndiyo inayowezesha utendaji wa taasisi na vyombo vinavyosaidia katika maamuzi ya kitaifa na usalama wa nchi yetu kwa jumla yake. Hivyo, kupitishwa kwa bajeti ya ofisi yangu na Bunge hili Tukufu kutakuwa ni chachu katika utulivu wa nchi, maboresho ya kiutendaji katika watumishi wa umma, kuimarisha utawala bora na uendelezaji wa utendaji kazi wa Serikali kwa weledi, maarifa, stadi na tija za rasilimali iliyopo katika watumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hii italiwezesha Taifa kupata matokeo chanya wakati wa kutekeleza malengo ya kitaasisi, kisekta na Taifa kwa jumla, ikiwa ni pamoja na kufikia malengo ya Dira ya 2050 hususan kwenye kipaumbele cha kwanza kinachoeleza kujenga uchumi imara jumuishi na shindani kwa kufanya mageuzi ya kiutendaji wa taasisi na kuimarisha utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanikisha dhamira hiyo, Serikali imeandaa programu ya maboresho ya muundo na mfumo wa watumishi wa umma na wa Serikali kwa jumla wenye malengo kwa wananchi yaani (Citizen Centric Programs). Kupitia programu tajwa, sera za utawala, utumishi wa umma, mifumo na miundo ya uendeshaji wa Serikali na usimamizi wa rasilimali katika utumishi wa umma itafanyiwa mapitio ya kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, utekelezaji wa programu hii utaweka msingi na uhalali wa Serikali wa kusimamia upatikanaji wa huduma bora kwa maendeleo na ustawi wa watumishi wa umma ili kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, programu inalenga matokeo makuu ya mabadiliko ya mtazamo wa wafanyakazi watumishi wa umma katika kuhudumia wananchi wetu. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza vibali vya ajira mpya kwa taasisi mbalimbali za umma. Kwa dhati tunamshukuru sana; kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri, kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2025, Serikali imetoa ajira zaidi ya 91,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ajira hizo za kawaida, Mheshimiwa Rais alitoa ahadi, kwamba ndani ya siku zake 100 za mwanzo ataajiri wafanyakazi katika idara ya afya 5,000 na watumishi wa kada ya elimu 7,000. Ninafurahi kuwa kazi hiyo tumeikamilisha kwa ustadi mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia ninataka kulieleza Bunge lako kuwa, katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imepanga kuidhinisha nafasi 45,000 za ajira kwa kada mbalimbali. Hongera Mheshimiwa Rais, Watanzania tunamshukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea michango ya Waheshimiwa Wabunge, ikiwemo ya vijana waliojitolea katika taasisi za umma ili wapatiwe kipaumbele katika nafasi za ajira. Nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, ameeleza vizuri juu ya mchakato mzima wa ajira. Hata hivyo, nami ninataka kuongeza neno kidogo ili kuweka rekodi sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kujitolea ndugu zangu au Waheshimiwa Wabunge wenzangu halikuwahi kuwa na mwongozo na utaratibu mzuri ambao unasimamiwa. Sasa, ofisi yangu imekamilisha utoaji wa Mwongozo wa Kujitolea katika Utumishi wa Umma wa mwaka 2025. Mwongozo huo umeweka sifa, utaratibu wa kuwapata vijana wa kujitolea, haki na wajibu wa wanaojitolea, utendaji wao, pamoja na utaratibu mzima unaosimamia vijana wanaojitolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo huu umesambazwa katika taasisi zote za Serikali kwa ajili ya utekelezaji. Nitumie nafasi hii kuwaelekeza na kuzieleza Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Taasisi za Umma, Mashirika ya Umma, Sekretari za Mikoa, na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia na kuelekeza ipasavyo juu ya mwongozo huu ili uweze kuleta tija inayokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Waheshimiwa Wabunge wako, wito wao wa kwamba elimu itolewe juu ya mwongozo huu tumeisikia. Ninamwelekeza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Utumishi kuandaa taratibu hizo kupitia Ofisi ya Mheshimiwa Spika ili pale tutakapokuwa tumekubaliana, Bunge lako Tukufu kupitia kupitia Kamati yetu ya inayosimamia Utawala, Katiba na Sheria, Bunge lako liweze kupatiwa elimu juu ya mwongozo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chote cha uongozi wa awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluh Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Idara yetu au taasisi yetu ya TAKUKURU imeendelea kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya kuzuia, kupambana na rushwa katika sekta za umma, mashirika na sekta binafsi kwa kuchambua mifumo ya utendaji na kutoa huduma. Majukumu haya yanafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329. Katika kipindi hiki TAKUKURU imebaini na kufungua kesi 3,186 za rushwa mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAKUKURU ni moja ya chombo kinachosimamia utawala bora. Hili ninataka lifahamike vizuri. Kati ya kesi hizo, 43 zilifunguliwa katika Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi ya Mahakama Kuu ya Tanzania. Aidha Mahakama ilitoa maamuzi katika kesi 2,838 za rushwa ambapo Jamhuri imeshinda kesi 2,040. Hii ni rekodi ya kipekee tangu Nchi ya Tanzania ilipopata uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa Mheshimiwa Rais Samia anaonesha ushupavu wake katika kupambana na rushwa; na tunapozungumza juu ya vitendo vya Mheshimiwa Rais anavyoonesha katika kupambana na rushwa, huu ni mfano mmojawapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAKUKURU imeokoa jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 300 ikiwa ni fedha taslimu. Aidha, matumizi yasiyostahili ya shilingi bilioni 25.75 na dola za Kimarekani 620,000 yalidhibitiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapambano dhidi ya rushwa nchini yatadhibitiwa kwa mambo mengineyo, ikiwemo taarifa za utafiti inayofanywa sasa, ambapo katika taarifa ya Transparency International ya mwaka 2025 na matokeo yake ambayo yalitangazwa Februari, 2026, taarifa inaonyesha kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kupata alama 40 na kushika nafasi ya 84 katika nchi 182 zilizofanyiwa utafiti. Kwa majibu hayo, Tanzania imeendelea kushika nafasi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki na nafasi ya 15 katika nchi za Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuchukua hatua muhimu za kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji usimamizi wa matumizi ya rasilimali za umma katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Mengine yameelezwa na wajumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka katika nukta hii, kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati yetu na Wajumbe wa Kamati yetu kwa ufasaha wa kueleza juu ya kazi kubwa inayofanywa na TAKUKURU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajumbe wameeleza na kutoa mfano wa Nyang'hwale, jinsi kazi nzuri ilivyofanywa na TAKUKURU katika kuhakikisha kwamba nyumba za watumishi na ofisi zinajengwa. Ninataka kutoa taarifa katika Bunge lako, siyo tu Nyang'hwale. Katika miaka mitano ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi 56 imefanywa yenye thamani ya bilioni 20. Kati ya hiyo, majengo 35 ya ofisi na nane yakikarabatiwa, ni sehemu ya mfano wa kazi kubwa inayofanywa kusimamia miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha huu unaokuja tumeomba tuthibitishiwe shilingi bilioni 9.23 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mbili za mikoa na ofisi 10 za wilaya. Ninatambua kwamba mahitaji bado ni makubwa, lakini tutajitahidi kadri fedha zinavyopatikana tuweze kufika katika wilaya zote ambazo hazina Ofisi za TAKUKURU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2026/2027, itaendelea kujenga uwezo kwa viongozi na kuwakumbusha viongozi wajibu wao wa kuwatumikia wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili na kushirikiana nao kutambua fursa za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Serikali mtandao katika nchi yetu umeonesha dhahiri mafanikio makubwa na kutambua kikanda na kimataifa. Zawadi nyingi zimepatikana na kwa kweli sisi kama wizara au kama Serikali tunafarijika kwa kazi nzuri kubwa inayoendelea kufanywa, ikiwemo ya kuendelea kuunganisha mifumo, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kuboresha mazingira yote ya biashara, kuhakikisha matumizi ya rasilimali fedha, watu na miundombinu inafanyika kwa tija ya maendeleo. Mifumo inayotumika Tanzania leo kwa zaidi ya 90%, imeundwa na vijana wa Kitanzania wanaofanya kazi kupitia Taasisi yetu hii ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kusimamia maadili. Kama ambavyo wajumbe wako wamesema na kutoa maoni yao, tutayazingatia na yale ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi haraka, Katibu Mkuu Utumishi amewasikia wajumbe. Tuendelee kusimamia ili Serikali iendelee na shughuli yake ya kuboresha mifumo ya kielektroniki kwa lengo la kuwafikia wadau wake kwa haraka, ufanisi na urahisi zaidi. Maoni yaliyotolewa na Kamati na wajumbe wako, tumeyasikia na tunakwenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kumbukumbu na nyaraka; Serikali itatumia kumbukumbu katika maamuzi ya uendeshaji wa Serikali, hivyo zinatakiwa kutunzwa kwa weledi. Historia za waasisi wetu zinatakiwa kutunzwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa, vijavyo na kwa ajili ya kujenga uzalendo na uendelevu na maamuzi bora kwa mustakabali wa Taifa letu. Hivyo bajeti yetu itasaidia usimamizi na uratibu wa utekelezaji wa majukumu ukizingatia sera, sheria, kanuni na taratibu za utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika taasisi za umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ikiidhinishwa na Bunge hili, itasaidia kukusanya na kuhifadhi nyaraka muhimu kutoka kwenye taasisi za umma, vitu vya waasisi wa Taifa, sekta na watu binafsi ili kulinda historia na urithi andishi wa nchi yetu pamoja na kuweka mifumo ya utunzaji na kumbukumbu na nyaraka, ikiwemo kidigitali ili kuwezesha utoaji wa maamuzi sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nguzo ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 inalenga kuwa jamii yenye utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya uendeshaji wa biashara, kuongeza kipato na pia kuimarisha hali za maisha. Ofisi yangu kupitia Watumishi Housing…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: … inasimamia Mfuko wa Uwekezaji wa pamoja ambao ni mfuko wa uwekezaji katika milki unaoitwa Mfuko wa Pamoja, ambao unalenga kukuza mtaji na utamaduni wa watumishi wa umma kuwekeza kidogo kidogo ili kuboresha maisha, ikiwa pamoja na kumjengea uwezo na kununua nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi yangu kupitia Watumishi Housing Investment imepanga kujenga nyumba 132 kama tulivyoeleza, ambazo zitajengwa tofauti na zile nyumba zilojengwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 ambazo zilikuwa 54 na mwaka wa fedha 2025/2026 ambazo zilikuwa 78.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuishukuru Serikali kwa mpango wa awali kama mtakumbuka kupitia Kamati yetu na pia ninapenda kumshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati kwa miongozo yake ambapo Serikali iliidhinisha ujenzi wa nyumba 78, lakini kwa msukumo na push kubwa iliyotokea kwenye Kamati. Serikali ilikubali kutuongezea fedha na sasa tunakwenda kujenga nyumba 132. Mazungumzo juu ya upatikanaji wa fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kumaliza ninaomba nichukue nafasi hii kukushukuru wewe, Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano na miongozo mliyotoa kwa Ofisi yangu. Kwa heshima na tahadhima, Ofisi yangu imepokea maoni, ushauri uliotolewa wakati wa mjadala na nitoe ahadi mbele ya Bunge hili kwamba masuala yote yatafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ninaomba sasa kutoa majibu na ufafanuzi kwa maswali na hoja chache kwa baadhi ya wachangiaji waliozitoa katika hotuba yetu ya bajeti kutokea Ofisi ya Waziri Mkuu mpaka Ofisi yetu ya Rais inayosimamia Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo Wajumbe wamegusia ninataka nigusie maeneo machache kwanza ni eneo la succession plan. Serikali imeelekeza kupitia maelekezo ya kikanuni kuwa ni lazima kila ofisi itengeneze succession plan na succession plan inao watu wanaoisimamia siyo jambo ambalo ni lazima Ofisi ya Rais, Utumishi ije kuiambia ofisi fulani au taasisi fulani kwamba muda sasa umefika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo yangu kwa Maafisa Rasilimali Watu na wale Waajiri waendelee kuzingatia mpango wa succession plan ambao umeandaliwa na ofisi zao na siyo jukumu letu kama Ofisi ya Rais, Utumishi kuja kuwashurutisha na kuwalazimisha kufanya mambo ambayo wameweka katika plan zao. Kwetu sisi kama Ofisi ya Rais, Utumishi tutakapopokea malalamiko ya watumishi ambao hawajaingizwa katika mpango huu, basi hatua za kinidhamu dhidi yao zitachukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia yamezungumzwa maeneo makubwa, ambayo ni maeneo ya kupongeza. Pia ninashukuru kwamba kupitia mpango wa TASAF sasa tunaenda kuanza utekelezaji wa mpango wa TASAF III. Maana nimesikia wengi wakisema mpango wa TASAF IV, lakini huu mpango wa TASAF III. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikwishakamilisha mpango ule wa mwanzo na sasa tunakwenda kuanza utekelezaji wa mpango mwingine. Mpango huu ndugu zangu, Wabunge wenzangu tunakwenda kuangalia maeneo ambayo yana changamoto kubwa katika maeneo ya mazingira. Pia maeneo ambayo tunatakiwa tufanye shughuli zitakazosaidia kubadilisha maisha ya watu kupitia kipato, lakini pia kimaisha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makubaliaono ambayo tumekwishayamaliza ninapenda kushukuru sana, ameeleza Mwenyekiti wa Kamati yetu kuwa Serikali na World Bank siku nne zilizopita tumefanikiwa kupita katika makubaliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kusema hili kwa taratibu ili wale ambao wanadhania kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa siyo mwongeaji katika maeneo haya, basi kwamba labda amelala, hapana, World Bank inathibitishia Watanzania kuwa Dkt. Samia anakubalika na matendo yake yanaheshimika duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kuthibitisha na kutuletea dola za Kimarekani milioni 300 kwa ajili ya Mradi wa TASAF ni moja ya alama nyingine kwamba Tanzania inakubalika katika sura ya kimataifa. Ninachowaomba Watanzania wenzangu watambue tunaye Rais bora anayetakiwa kuungwa mkono, tusimbeze tumpe moyo aende kutukomboa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kuhakikisha kwamba Taasisi yetu ya TAKUKURU inafanya kazi zake kwa weledi na kusimamia utaratibu mzuri. Wameeleza Wajumbe na sitaki kurudia, lakini matendo yanayotekea, kesi zilizotokea nyingine zikitugusa sisi Waheshimiwa ni wazi kuwa Rais Dkt. Samia hana mzaha katika jambo la rushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombeni tena Watanzania wenzangu hasa sisi viongozi tumtie moyo Rais wetu, tusimbeze, tumtie moyo aendelee kupigania maendeleo ya Watanzania yale. Pamoja na hilo pia ameeleza kwa sauti nzuri, lakini nimemwelewa Mjumbe mwenzetu Bi. Lucy Kombani, juu ya maeneo ambayo tunatakiwa tuyaangalie hasa katika maeneo ya rufaa, juu ya maeneo ya Sera za Ajira, za Utumishi wa Umma. Pia wengine wameelezea jinsi ambavyo Tume inatakiwa kuangalia mustakabali mzima wa wananchi, pay as you earn kuondolewa kwa wenzetu walemavu.
MheshimiwaMwenyekiti, ninataka niwahakikishie ndugu Wajumbe kama nilivyoeleza katika maelezo yangu ya mwanzo, sisi tumesikia michango yenu yote ile ambayo tunatakiwa tuandike kwa maandishi, tutaijibu kwa maandishi na mengine ya kuchukuliwa kwenda kufanyiwa kazi. Ninapenda kukuahidi kwa Bunge lako kwamba Mheshimiwa Rais amekwishatuelekeza Waajiri wetu, Mabosi zetu ni wananchi na wananchi kupitia Wabunge hawa wamezungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kutoa hoja. Ahsanteni. (Makofi)