Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Kwanza ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunijaalia kuwa hapa katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani yake kubwa kwangu, kwa kuniamini na kuniteua kuwa sehemu ya wasaidizi wake. Pia ninachukua nafasi hii kumpongeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwa kuwa msaidizi wa Rais, kwa kumsaidia kwa karibu kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kufanya kazi nzuri ya kuendelea kuhakikisha Tanzania inasonga mbele. Sisi kama wasaidizi wake tunaendelea kujifunza mengi kupitia kwake na hakika anatuonesha njia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wangu, kwa namna ya pekee ameendelea kunilea, kuniongoza na kunishauri. Hakika nimepata mlezi na mwalimu. Ninaendelea kukushukuru Mheshimiwa Waziri, ninaendelea kujifunza mengi kupitia kwako na hakika nitaendelea kukusaidia kufanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia watumishi wote wa Wizara nikianza na Katibu Mkuu, Ikulu, Bwana Mululi Mahendeka; Katibu Mkuu Utumishi, Juma Mkomi; Naibu Katibu Mkuu, Bwana Daudi na Wakuu wote wa Taasisi na watumishi wetu wote wa Wizara kwa namna wanavyonipa ushirikiano ili niweze kutekeleza majukumu yangu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kwa namna ya pekee kuwashukuru wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Manyara wakiongozwa kitaifa na mama yetu Mary Chatanda, Mwenyekiti wa UWT – Taifa kwa namna anavyotuongoza. Pia, ninawashukuru zaidi wanawake kwa sababu wamenipa kura nyingi za kishindo zilizonifanya kuwa katika ukumbi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na si kwa umuhimu, ninaishukuru familia yangu. Ninamshukuru mume wangu na watoto wangu, kwa kipindi chote wamekuwa wakinipa ushirikiano mkubwa, lakini wamekuwa wakiniombea katika majukumu yangu na kunivumilia pia pale ambapo ninakuwa katika majukumu yangu na kuwa mbali na familia yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani na pongezi hizi sasa ninaendelea kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu. Ninaanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wote kwa umoja wetu hapa ndani tutakubaliana kwamba kwa kipindi kifupi Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia tu madarakani, kwa muda mfupi sana alitekeleza miradi mingi katika maeneo yetu. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea miradi katika elimu, afya na miradi mingine. Kwa kutekeleza miradi hiyo, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona ile miradi inakwenda kufanya kazi na kuwanufaisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Dkt. Samia Suluhu Hassan baada tu ya kuapishwa mwezi Novemba kazi ya kwanza alianza kutoa ajira kwa vijana na Watanzania wote. Kwa kipindi kifupi kabisa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa ajira 25,235 toka Novemba – Aprili 13, 2026. Ajira hizi zimeelekezwa katika kada ya elimu ambapo ameajiri vijana wa Kitanzania 9,431. Katika afya alitoa ajira 10,786 na kada zingine 5,018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kauli ya Rais ya kuendelea kujali sera yake ya kusema Kazi na Utu hakuwasahau kundi la walemavu. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ajira hizo amewapa walemavu 238. Katika ajira zote zinazotolewa walemavu wamekuwa wakipewa kipaumbele. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ajira hizi ili zile shule alizozijenga na vituo vya afya vilivyojengwa vianze kutoa huduma na Watanzania waendelee kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia Kazi na Utu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuweka tabasamu kwa watumishi wa nchi hii. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka wa fedha 2025/2026, amelipa malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 9,999 yenye thamani ya shilingi 23,011,513,238.13. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo alitoa promotion kwa watumishi 98,430. Pia, hakusahau kuweka nyongeza ya mishahara, kipindi chote kila mwaka Mheshimiwa Rais amekuwa akitoa nyongeza ya mshahara, lakini ameendelea kuboresha mazingira rafiki kwa watumishi wa umma wa nchi hii ili waweze kutoa huduma iliyo bora kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu ya muda ninajielekeza kujibu hoja chache za Waheshimiwa Wabunge. Kwanza ninapongeza sana Waheshimiwa Wabunge waliopata nafasi ya kuchangia. Wapo Waheshimiwa Wabunge 14 walioweza kuchangia kwa kuongea na wapo Waheshimiwa Wabunge wawili ambao wameleta mchango wao kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo hoja ambazo zimetolewa humu ndani, nitajibu chache lakini mengi atajibu Mheshimiwa Waziri wakati anakwenda kumalizia hoja. Kuna hoja inayohusu ajira kwa wale wanaojitolea. Kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti ya Ajira na Utumishi wa Umma, Toleo la Pili, 2008 imeelekezwa kwamba ajira zote za nchi hii zitatolewa kwa ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa kwamba wapo watumishi ambao wanajitolea, wanafanya kazi katika mazingira yetu na katika taasisi zetu. Wizara imekuja na mwongozo ambao unaelekeza namna ya kupata vijana wa kwenda kujitolea, au watumishi wanaopenda kujitolea katika taasisi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya hivi kwa sababu, si wote wanaweza kupata fursa ya kujitolea na ndiyo maana tumesema ajira ziwe za ushindani ili kuleta usawa, ili kuleta mazingira rafiki na ili kuleta utaifa na umoja. Ajira hizi zitolewe kwa ushindani ili wale wenye sifa na wenye uwezo, wanaweza kuingia kwenye ajira hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ambapo ajira hizi zinatolewa kwa kuangalia wanaojitolea, wapo watu ambao walikuwa wanakosa nafasi hizo kwa sababu kulikuwa na upendeleo mwingi. Ili mtu aweze kujitolea, wanaangalia anafahamiana na nani, ni mtoto wa nani; lakini kwa sasa hivi ajira hizi zinatolewa, kwamba wote watachaguliwa kwenda kufanya usaili na kushiriki usaili ili ukifaulu kwa kuangalia vigezo, basi unapata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweka sheria humu, kwamba tuwe na chombo kinachoweza kusimamia masuala ya ajira kwa watumishi wa umma. Sekretarieti ya Utumishi wa Umma imeendelea kutengeneza mazingira rafiki katika kuhakikisha kwamba watu wanaomba ajira hizi na baadaye wanachaguliwa kwenda kufanya usaili. Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira imeweka mfumo wa uwazi, mfumo ambao kila mtu anapata haki ya kushiriki katika usaili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kufafanua kuhusiana na usaili huu, kwa sababu kumekuwa na hoja mbalimbali za kusema kwamba mtu anaenda kwenye usaili anakutana na mitihani au na maswali tofauti na masomo yake. Kwenye ule usaili wa mchujo (aptitude test), maswali yanayoulizwa mle kwenye ule mtihani wa mwanzo kabisa, kwanza ni kupima uwezo wa mhusika, uwezo wa asili wa mhusika; lakini pia yako masuala ya jumla na pia yako masuala ya current issues ambayo yule msailiwa anapaswa ayafahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, 60% ya mtihani ule inahusu taaluma, 40% ndizo zinakwenda katika kupima yale masuala ya jumla na masuala ya current issues. Kwa hiyo ninawatoa hofu Waheshimiwa Wabunge, kwamba mitihani ambayo inatumika kuwapima vijana wetu wanapoenda kwenye usaili ni mitihani rafiki ambayo humfanya mtu ajibu maswali, apate asilimia zile zinazotakiwa. Kutokana na hii asilimia kubwa wanafaulu. Tunachoangalia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ya mwisho?

MWENYEKITI: Ndiyo.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi. Niendelee kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia sisi kipindi chote tunapofanya kazi. Nasi tunawaahidi, kwamba tutakuwa wanyenyekevu, tutaendelea kufanya kazi pamoja nao, nao waendelee kutupa ushirikiano mkubwa ili tusonge mbele katika kulisukuma gurudumu hili la utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)