Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Jasmine Chesco Ng'umbi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JASMINE C. NG’UMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Sasa, kwa kuwa leo ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge lako Tukufu, ninaomba kuanza na shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti wangu wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Samia Suluhu Hassan; yeye pamoja na vikao vyake vyote kwa kunipitisha na mwishowe kuwa Mbunge wa Vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kutoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akionesha imani kubwa sana kwa sisi vijana katika suala zima la utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua na wewe utakubaliana na mimi, hata katika hili Bunge lako Tukufu, asilimia kubwa ya Wabunge ni vijana. Kama hiyo haitoshi, hata katika Baraza la Mawaziri tunaona sasa Mheshimiwa Rais amewaamini vijana na kuwapa Uwaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea sana sana kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa ambayo anatuonesha sisi vijana. Wapo Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi katika taasisi mbalimbali na katika Wizara hii ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambao ni vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninapenda kumwambia Mheshimiwa Rais kuwa imani aliyotupa sisi vijana ni kubwa sana na kwa imani hiyo sisi vijana tupo tayari kumwonesha matokeo ya imani aliyotupa. Tunaahidi tutaendelea kumpa ushirikiano wa hali na mali kuhakikisha imani aliyotupa haipotei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Ridhiwani Kikwete, kwa hotuba nzuri aliyoiwasilisha leo hii. Kwa kweli hotuba yake ni nzuri, imebeba maono lakini imezingatia Dira ya 2025 - 2050. Sambamba na hilo, hotuba ya Mheshimiwa Waziri imezingatia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2025 - 2030. Hii inaonyesha ni namna gani Wizara imejipanga na inatamani kuona mabadiliko ya hali ya juu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ninaomba nielekee katika kuchangia hotuba hii. Hotuba hii imeelezea kiundani kuhusu suala la ajira kwa vijana na kama nilivyosema mwanzo mimi ni Mbunge wa vijana. Ninaomba nijikite katika suala zima la ajira kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua katika Tanzania yetu kuna vijana wengi sana wanaojitolea, lakini hawa vijana wanaojitolea ni nguvu kazi kubwa sana. Ninaendelea kuwapongeza vijana wanaojitolea kwa sababu kujitolea ndugu zangu siyo kazi rahisi. Kujitolea huku kunaonyesha uzalendo wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yangu sikivu ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iwaangalie hawa vijana wanaojitolea kwa jicho la tatu. Vijana hawa wanafanya kazi kubwa mno. Linapokuja suala la ajira, zinapotokea fursa, ninaomba hawa vijana wanaojitolea ikiwezekana wapewe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la NIDA, tunatambua kuna changamoto ya upatikanaji wa NIDA, lakini unakuta ajira zimetangazwa, vijana wanatamani kwenda kuomba fursa hizo ambazo zimetangazwa, lakini kigezo namba moja unakuta unaambiwa kijana lazima awe na NIDA. Sasa, unajiuliza, huyu kijana mpaka kuwa na NIDA unakuta ufuatiliaji wa NIDA unaweza ukachukua mwezi na muda mwingine mpaka zaidi ya mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaiomba Wizara na Serikali yangu sikivu ya Awamu ya Sita iangalie namna ambayo itasaidia vijana hawa kupata NIDA kwa wakati ili zitakapotokea fursa za ajira hawa vijana nao waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niendelee kuchangia katika suala zima la upatikanaji wa taarifa au fursa za ajira ambazo zinatokea. Tunaona muda mwingine kuna fursa ambazo zinatokea, tunakubaliana sisi wote humu ndani teknolojia ni kweli ipo, fursa zinatangazwa kwenye mitandao, lakini kuna vijiji vingine, kuna vijana wengine wapo mbali na teknolojia. Teknolojia bado haijawafikia, hawapati taarifa kwa wakati. Wakija kupata taarifa unakuta muda wa kuomba nafasi katika hizo fursa zilizojitokeza umekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali yangu iangalie namna nzuri ya kuwafikia hawa vijana wote kwa umoja wao wapate taarifa. Serikali yetu ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan uzuri wake ina uongozi kutoka ngazi ya vijiji na kata, ikiwezekana hawa viongozi washirikishwe, waambiwe kama kuna fursa za ajira zimejitokeza kwani wao wanajua kwenye vijiji vyao...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. JASMINE C. NG’UMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)