Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LUCY EDWARD MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi kuongea jioni hii katika hoja ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa kibali cha afya na uzima. Pia, kwa upekee kabisa ninapenda kumpongeza mtumishi mwenzetu namba moja, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Rais kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi pamoja na kujali wafanyakazi. Kwa jitihada zake kubwa ninaomba pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha anaongeza ajira katika sekta zilizo rasmi na zisizo rasmi yaani informal sector na formal sector. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umahiri mkubwa, Mheshimiwa Rais amehakikisha anaimarisha bima ya afya kwa watu wote lakini pia afya ya wafanyakazi ambao wanaishi na maambukizi ya VVU. Kwa kupitia Menejimenti ya Utumishi wa Umma wafanyakazi hawa wanafanya kazi kwa uhuru, amani na bila ya kunyanyapaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia kwa upekee nimpongeze mfanyakazi mwenzetu namba moja wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia amekuwa kinara kwa kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanaboreshwa ikiwemo mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amehakikisha anatengeneza mazingira bora kwa wafanyakazi ambao wanaingia kwenye ajira mpya na hasa ameandaa mpango maalum kwa ajili ya kuboresha makazi bora ya wafanyakazi ambayo yanasimamiwa na Shirika la Nyumba la Zanzibar – ZHC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upekee tena ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Naibu Waziri wake ndugu yetu, Regina Ndege, ambaye anamsaidia kazi kwa umakini na tumemuona alikuwa akijibu maswali mengi, dada huyu yuko makini na siku zote wanawake wanaweza. Kwa hiyo, ninampongeza sana dada Regina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 10 – 12 wa randama, imeonyesha mafanikio makubwa yaliyopatikana kutoka mwezi Julai, 2025 mpaka Februari, 2026. Katika mambo ambayo yameweza kushughulikiwa na Menejimenti ya Utumishi wa Umma ni pamoja na vibali vya ajira 43,806. Pia, kuweza kulipa deni la watumishi zaidi ya shilingi bilioni 23 katika taasisi mbalimbali pamoja na Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia imeanzisha mobile clinic katika kutafuta changamoto za mfumo wa usimamizi kupitia utendaji kazi (e-utendaji). Pia, kuna mfumo ambao waliweza kuuendesha kwa mafanikio, mfumo wa e-msawazo kwa ajili ya kugundua upungufu wa watumishi ambao wamefanikiwa kupata upungufu wa watumishi zaidi ya 200,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upekee ninaomba kukiri kuwa mimi ni Mbunge wa Viti Maalum kupitia kundi la wafanyakazi. Sasa ninaomba nianze kutoa mchango wangu. Mchango wangu wa kwanza ni kupitia vyama vya wafanyakazi. Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni haki ya mfanyakazi au mtumishi wa umma kikatiba kujiunga kwa hiari kupitia vyama vya wafanyakazi. Pia, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004 inathibitisha haki hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, baadhi ya taasisi za umma zimekuwa zikiwaingiza wafanyakazi kwenye vyama vya wafanyakazi kwa lazima bila ya hiari yao. Baadhi ya taasisi za kazi zina vyama zaidi ya kimoja lakini ilikuwa ni vyema kuwashauri wafanyakazi wanapoingia katika ajira Serikalini kujiunga na vyama vya wafanyakazi ambavyo wanavihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumzia pia suala la uhamisho. Ninaipongeza Serikali kwa hatua zake zinazoendelea kutekeleza kwa ajili ya ajira za wafanyakazi hasa kupitia Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa 2018 ilipotoa agizo kwa taasisi za kazi kutokuhamisha wafanyakazi bila ya ridhaa au kuhamisha bila kuwa na fedha ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taasisi za kazi zinapotoa uhamisho kwa wafanyakazi wanatakiwa waongee na wafanyakazi kujadiliana kwa pamoja ili mfanyakazi mwenyewe awe na hiari ya kwenda kule anapotaka kwenda au hiari ya kwenda bila ya kulipwa hizo fedha kwa wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie pia upande wa kupandishwa madaraja. Wafanyakazi wanachelewa kupandishwa madaraja, malalamiko ya wafanyakazi kutopandishwa madaraja ni mengi. Kwa hiyo, tunaomba kwa mujibu wa sheria pale mfanyakazi anapohitajika kupandishwa daraja apandishwe daraja kwa wakati. Ninaomba niishauri Serikali kusimamia eneo hilo katika taasisi za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wafanyakazi ambao wanakaimu kwa muda mrefu. Wafanyakazi wanakaimu kwa zaidi ya mwaka mmoja katika taasisi. Ninaiomba Serikali hasa kupitia Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuhakikisha taasisi hizi zinazowakaimisha wafanyakazi au Wizara na idara zinazokaimisha wafanyakazi au watumishi wahakikishe watumishi hao wakizidi zaidi ya mwaka mmoja wathibitishwe pale inapoonekana wana uwezo, vigezo, uzoefu na uadilifu. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa smuda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. LUCY EDWARD MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja. Niwaombe wafanyakazi wenzangu wa taasisi zote za Serikali, endapo itatokea na sisi kufanya kazi, tuwe waadilifu. Wajibu wetu ni kufanya kazi, lakini na Serikali ni haki yetu kutupa stahiki zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)