Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mariam Anzuruni Mungula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami ya kuchangia katika Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora, Wizara yenye Jimbo langu la uchaguzi nikiwa kama Mwakilishi wa Wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunifikisha siku ya leo nikiwa mwenye afya njema na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba kumshukuru mtumishi wetu namba moja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpongeza sana, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoendelea kuchapa kazi kwa bidii na kutupa moyo sisi watumishi wengine wote tunaomsaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Dkt. Samia anafanya kazi, wazungu wanasema above and beyond her call of duty. Kwa hiyo, tunampongeza sana na tunazidi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu afya bora, afya njema, hekima zaidi na utulivu ili aendelee kutuletea maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuipongeza sana Wizara ya Utumishi na Utawala Bora chini ya Waziri wetu Ridhiwan Kikwete na taasisi zake zote na watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi njema wanayoifanya, wanayo kazi kubwa sana, lakini wanaendelea kutuwakilisha Watanzania vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ninaomba kuwapongeza watumishi wote wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka. Utumishi ni kazi ya kujitolea zaidi na kwa kweli watumishi wetu wote wanafanya kazi kwa bidii kwa kiasi kikubwa sana na Mwenyezi Mungu azidi kutubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitauelekeza zaidi katika upande wa utumishi wa umma. Ninaomba kuanza kama nilivyosema, nikiwa kama mwakilishi wa watumishi mengine ninaweza nikaongea ambayo tayari Wabunge wameshayapitia, lakini nimetumwa na watumishi niyasemee. Kwa hiyo, ninaomba nitayarudia wanivumilie kidogo kwa ufupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la uajiri, ninawapongeza sana Wizara ya Utumishi kupitia Sekretarieti ya Ajira kwa kuendelea vile vile kututolea ajira mpya. Tunayo changamoto moja ndogo ambayo imenifikia wakati wa usaili wa waajiriwa wa wapya, pale tunakuta kwamba obviously, wale wanatoka maeneo tofauti, wanatoka sehemu mbalimbali mikoani pengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtu anafika pale amesahau labda cheti cha kuzaliwa anarudishwa anaambiwa hataweza kushiriki kwenye ile interview (usaili), lakini huyu unamkuta ana kitambulisho cha NIDA. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba watumishi kuwe kuna angalau ile customer care iwe kuna hali ya utu fulani wa kuwaangalia hawa watumishi. Wengine wame-struggle miaka mingi hana kazi, halafu anaona hii labda ndiyo chance ya yeye kupata ajira, lakini mambo yanaenda ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru pia Serikali kwa kuendelea kupandisha mishahara na stahiki za watumishi. Vilevile ninaomba kwenye hili suala la mikataba ya hali bora, ukweli ni kwamba hii mikataba ya hali bora inatakiwa kuboreshwa kila baada ya miaka mitatu, lakini unakuta taasisi nyingine hazijaiboresha hii mikataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi nyingine nyingi hususani za binafsi bado hazijaingia hii mikataba ya hali bora. Hii mikataba ya hali bora kwa kiasi kikubwa inachangia kuleta utofauti wa mishahara na watumishi kuamua kwamba labda nitoke niende nikafanye kazi sehemu fulani, kwa ajili ya kwenda kufuata tu yale maslahi mazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba Wizara iangalie uwezekano wa kuhakikisha kwamba taasisi zote zinaingia hii mikataba ya hali bora na inakuwa up to date. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa vilevile tuna suala la mabaraza ya wafanyakazi. Kwenye haya mabaraza ya wafanyakazi ndiyo sehemu ambayo mfanyakazi anakwenda kutoa nyongo yake, tunaweza tukasema, kama ana lolote anaweza kwenda kuongelea hapa kwenye Baraza la Wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inalifahamu kwamba kuna baadhi ya taasisi nyingi huwa hazifanyi haya mabaraza ya wafanyakazi na yako pale kisheria. Kwa hiyo tunaomba Wizara ihakikishe kwamba taasisi zinatekeleza hili jukumu au Maafisa Masuuli wanafanya haya mabaraza ya wafanyakazi. Katika hili ninaomba Waziri wakati akija kuhitimisha atuambie ni taasisi zipi au ngapi ambazo hazifanyi haya mabaraza ya wafanyakazi na Wizara inawachukulia hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba vilevile kwenye hili suala la watumishi wanaojitolea ninaipongeza Wizara imeshachukua hatua.

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Wizara kwa kuchukua hatua kwa watumishi wanaojitolea lakini hizi hatua walizozichukua wao kwa kuweka mwongozo na kutenga bajeti zisambae katika Serikali nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninaomba kuliongelea hili. kuna watumishi ambao...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha. (Makofi)

MHE. MARIAM A. MUNGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)