Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii niweze kuchangia katika Wizara hii mahususi, Wizara muhimu kwa maslahi ya Taifa letu. Ninaseme tu hii ndiyo Wizara ambayo inaweza kuleta tumaini kubwa kwa Watanzania wote; kila mmoja katika Bunge hili, kila mmoja kwenye nafasi yake na kila mwananchi popote alipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani hii ndiyo Wizara ambayo tunatakiwa kuitazama kwa jicho la kipekee na kuona ni namna gani inatutoa tulipo twende sehemu ambayo ni salama zaidi. Kiukweli ninapochangia Wizara hii ninamwomba Mwenyezi Mungu aniongoze, ili niweze kusema yale ambayo yataendelea kulijenga Taifa langu kwa maslahi ya wananchi wote wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuipongeza Wizara, sina mashaka na kaka yangu Mheshimiwa Ridhiwani, sina mashaka na rafiki yangu Mheshimiwa Regina, sina mashaka na viongozi wote wanaoongoza Wizara hii, lakini zaidi ya yote ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameendelea kuifanikisha Wizara hii iweze kufanya kazi vizuri. Leo ninatamani nijikite kwenye eneo la TAKUKURU, however kuna maeneo mengine ambayo ningependa niyazungumzie, lakini ninatamani sana nijikite kwenye eneo la TAKUKURU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mungu nina uelewa wa kutosha kuhusiana na mambo ya rushwa. Nina uelewa wa kutosha kwa namna ambayo TAKUKURU inafanya kazi kwa kuwa, nimekuwa mtumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tu ninawapongeza TAKUKURU kwa namna ambavyo wamekuwa wanaendelea kupambana kufanya kazi yao. TAKUKURU ndicho chombo ambacho kina majaribu mengi; kina kazi ngumu ya kuwakamata watu ambao ukitazama wengine hawakamatiki, kina kazi ngumu ya kuhakikisha kinasimamia watu wapate huduma, kama inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika, sasa hivi rushwa imekuwa ipo juu sana, hata kama tutakuwa tunafanya unafiki wakati mwingine, hata kama tutakuwa tunafanya kufumba macho, hata kama tutakuwa tuna-deny the reality, ukweli ni kwamba, huko kwenye jamii yetu hali siyo nzuri rushwa ipo juu. Sasa basi, tunafanya nini kuhakikisha hali hii ya rushwa kwa wananchi wetu inapungua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tu kabla sijasahau, ninaendelea kumpongeza DG ambaye yupo, Ndugu Crispin Francis Chalamila, watumishi wake wana amani na yeye, wana furaha na yeye na kiukweli wanafurahia ziara anazozifanya kwenye maeneo yao kufuatilia kero zao. Kwa hilo tu ninampongeza DG huyu kwamba, aendelee kuwa karibu na watumishi wake hadi ngazi za chini ndipo ataweza kupata ushirikiano mzuri kwenye kazi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili pia, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, kabla sijasahau, kwa kuweza kupeleka magari kwenye wilaya zote, kwenye mikoa na hata vile vituo maalum vya Tunduma tumepata. Momba tumepata na Mkoa wangu wa Songwe wote kwa ujumla tumepata hayo magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili pia ninaendelea kumpongeza DG na ninampongeza Mheshimiwa Rais, ambaye ameamua kuridhia fedha hizo ziende na vyombo vya usafiri vikaweza kununuliwa. Hiyo inaonesha kwamba, kweli wamedhamiria kuweza kuboresha utoaji huduma katika idara hii ya TAKUKURU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea pia kuishukuru Wizara kutenga fedha, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha TAKUKURU, Momba na pia, kuendelea kujenga Majengo ya Watumishi Momba. Ninawashukuru sana, kwangu hilo angalau ni faraja, lakini ninafahamu wametenga fedha mwaka huu, kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya TAKUKURU kwa Mkoa wa Songwe. Kwa hilo pia, ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba isiwe ahadi ya kwenye maandishi iwe kwenye vitendo, tuweze kupata Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Songwe na uzuri wake ramani zao ni nzuri sana, kwa hilo pia, ninaendelea kuwaomba wasisahau Wilaya zangu za Songwe, Ileje na Mbozi, watujengee majengo, Ofisi ya TAKUKURU inahitaji privacy, Ofisi ya TAKUKURU inahitaji watu wasio accessibility kirahisi, sasa wanapokuwa wamepanga mitaani humo inakuwa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, ombi langu maalum kwa Wizara hii, ninamwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, Tunduma ifanyike kuwa Wilaya Maalum ya TAKUKURU, Mkoa wa Songwe. Kwa sababu gani ninaongea Tunduma; Tunduma ni sehemu ambayo ni sensitive, ina mahitaji makubwa na ina viashiria vingi vya rushwa kwa hiyo, wakiifanya ikawa wilaya maalum, nitaweza kufarijika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa ajili ya maombi ya mkoa wangu, ninaendelea pia, kuishauri Serikali yangu; katika kusomasoma kwangu nimemwona DG wa TAKUKURU na nimemwona Mrajisi, Bwana Benson Ndiyega, wanaingia mkataba wa makubaliano ya kufanya kazi kwa pamoja kudhibiti rushwa katika SACCOS; nimefarijika kuona yale makubaliano, ukweli ni kwamba, kwenye vyama vya ushirika hali ya rushwa ni kubwa. Wananchi walio kwenye vyama vya ushirika wengi wanahujumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili tu ninaendelea kuipongeza Wizara, kumpongeza Mkurugenzi wa TAKUKURU na huyu Mrajisi kwa kufanya maamuzi hayo ya kuingia makubaliano. Ipo haja ya TAKUKURU kuwa karibu na vyama vya ushirika, kufuatilia kila kitu kinachoendelea kwenye vile vyama vya ushirika, wananchi wetu wasiweze kuibiwa. Ninamwomba pia Dkt. Benson Ndiega, huyu Mtendaji Mkuu wa TCDC, awe aggressive kwenye kusimamia hivi vyama vyake vya ushirika, hali ni mbaya kwenye vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarejea kwenye taasisi zetu hizi za Halmashauri, lakini ukiacha halmashauri kuna maeneo mbalimbali ambapo kumekuwa na waajiriwa ambao wanaajiriwa kwa mapato ya ndani. Sijajua TAKUKURU hapa wanasimamiaje, ili hii ya uajiri wa watumishi kwa mapato ya ndani isije ikawa pia, ni chanzo cha kutoa mapato ya Serikali kwa njia zisizo rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani hapa ninataka kusema kwamba, isiwe chachu ya wizi wa fedha za Serikali kwa kupitia hawa waajiriwa wanaowaajiri kwa mapato ya ndani kwenye maeneo mengine. Ufanyike utaratibu maalum wa namna ya kuajiri watumishi wa muda kwenye taasisi mbalimbali za Serikali. Tulienda kwenye ziara, unakuta watumishi karibu 100 ni wa muda, wanalipwa kwa mapato ya ndani; how sure are you kwamba, watu wote wapo na hakuna utaratibu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yote ninamaliza kwa kusema pia, Tume ya Maadili haitutendei haki kwa namna ambavyo inapewa fedha nyingi; wamepewa shilingi bilioni 16, mwaka jana umepita, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante muda wako umekwisha.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe. Ni mashauri 120 tu wamefanyia kazi, wametoa semina kwa watu 15,000; kwa nini hawakuweka malengo na hao watu 15,000 waweze kuleta mashauri ambayo yataweza kusaidia nchi? Kwa hiyo, mimi nasema hela inayoenda kwenye Tume ya Maadili kwa kweli, inanipa changamoto…