Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake, lakini na Serikali nzima. Ninashukuru kwa mchango wa dada yangu ambaye amemaliza wa watumishi kujinyoosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea utawala bora siyo jambo jepesi kama tunavyoliongelea hapa Bungeni. Tunaongea tukichukua component moja ya utawala bora, utawala bora is holistic by nature, yaani inahusisha mambo yote ambayo Serikali inayafanya, pamoja na kujinyoosha. Mimi nina mawazo tofauti kidogo, sisi ambao tunatoka mikoa ya pembezoni mwa nchi, haya yote tunayoyaongelea kuhamisha watumishi, sijui kufanya nini, juzi hapo walifungua kidogo na ninashukuru Mheshimiwa Waziri waliiona mapema wakafunga lile dirisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa ninaongea na watu wilayani kwangu pale, wanasema kwa kipindi kifupi ambacho waliruhusu watu kuhama, Wilaya kama Muleba tumepoteza wafanyakazi wengi. Kwa hiyo, kuongoza nchi siyo jambo jepesi la lele mama, ni jambo nyeti na ni jambo gumu na niwapongeze Wizara ambayo imeleta hoja yao leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba hili jambo tuliangalie kwa umakini. Nchi yote ina taasisi za umma, ina taasisi za Serikali, lazima zihudumiwe na wafanyakazi ambao wameajiriwa na nchi hii. Ambacho ninapendekeza, tuangalie utaratibu mzuri kwa mikoa ambayo iko pembezoni na Wilaya yangu ya Muleba ikiwemo. Hawa wafanyakazi ambao tunawatuma kule, kutokana na mazingira yao magumu, tutengeneze package.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu, hii Wizara ipewe bajeti kubwa sana kuliko hii tuliyonayo, tunayoipitisha leo. Tuwatengenezee motisha ambayo itawavuta kutoka huko mijini wakapendelea kufanya kazi huku pembezoni mwa nchi. Hili lilikuwa ni angalizo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekretarieti ya Ajira wanafanya kazi nzuri na ninampongeza Katibu wetu pale na watumishi wote, wanafanya kazi ya kusaili vijana wetu, kuwaingiza kwenye mfumo na kupata ajira. Ukiangalia bajeti waliyo nayo, vitendea kazi wanavyovihitaji, hawa watu kwa kweli, kwa kazi wanayoifanya tunahitaji kuwapongeza na tunahitaji kuwapa bajeti. Kila mwaka tuwaongezee ili waendelee kufanya kazi yao kwa umahiri na kwa umakini mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia vijana wanaokwenda kufanya usaili, siku hizi wanatembea na vyeti kama tulivyokuwa tunatembea navyo miaka ya 2020, nyakati zimebadilika, majira yamebadilika. Ninaomba tuiwezeshe hii Sekretarieti ya Ajira ili wafanye kazi kwa umahiri na umakini zaidi, tuwape pesa kwa ajili ya kununua vifaa vya TEHAMA. Badala ya vijana wetu kutembea na vyeti, wa-scan, watume, wanakwenda kufanya usaili waende wakiwa wanatembea kama tunavyokuja Bungeni. Ni kazi nzuri wanaifanya na niwapongeze kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja, tunafanya usaili kila inapotangazwa nafasi na vijana wanatembea kutoka mikoa mbalimbali na wengine wanatoka mbali, ninashukuru wameanza kufanyisha kwenye mikoa yetu. Ninaomba wanapofanya usaili, badala ya kuwa kila nafasi inapotangazwa vijana wanaleta maombi, wanakuja kufanya usaili, wanapata wachache, wengine wanabaki. Niombe tuwe na utaratibu wa kuwa na benki ya vijana ambao wanafanya usaili kwenye nafasi moja. Nafasi inapotokea siyo lazima tuwaite tena kuja kufanya usaili ila tunaweza tukaangalia kwenye benki tuliyokuwa nayo huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tume ya Maadili ya Umma; ninawashukuru wanafanya kazi nzuri, kama nilivyotangulia kusema, taasisi zote zinafanya kazi nzuri na bila hii Wizara, mjomba ninakupongeza. Hii ndiyo Wizara ambayo ni engine ya maendeleo na usalama wa nchi. Tofauti na hapo, mengine tunaweza tukasema, bila usalama hatuwezi kusonga mbele. Ninawashukuru kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maadili ya Umma; kila mwaka tunajaza taarifa zetu na tunapokwenda mwezi Desemba ambapo tunapaswa kujaza taarifa zetu, sisi ambao tunapaswa kujaza na ni kazi nzuri lazima tuifanye, lakini tunakuwa na jam pale mwezi Desemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali yangu, huu mfumo wa kujaza taarifa za wanaopaswa kujaza kwenye hii Tume, ninaomba uendelevu, kama wanaweza tufungue mwezi Oktoba tuanze kujaza taarifa zetu, kama nimenunua, kama nimeuza niiondoe. Kuliko ule mwezi Desemba tunaanza kupambana, kama msemaji wa pili alivyosema kwamba, tunapoteza muda mwingi kwenye kujaza hizo taarifa. Wakati mwingine mifumo haifanyi kazi kwa sababu ya wingi wa watu wanaopaswa kujaza taarifa zao kwenye mfumo. Ninashauri tufanye liwe endelevu, hata kama tunasema mwaka mzima, miezi 12 iwe wazi, kwa ajili ya kujaza taarifa zetu na wao watatuambia ni nini tunachopaswa kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TASAF; ninapongeza, nimeona kazi ambayo wanaifanya, lakini ninaomba nishauri kwenye hili; TASAF tumekuwa tukiwapa pesa wanafanya maendeleo yao, lakini ninaona wamekuja na mkakati mzuri sana. Tulipokuwa pale Mwanza nimeshuhudia vikundi vya akina mama ambao wamepewa pesa wakaanzisha viwanda vidogo vya kusindika matunda, ni mkakati na approach nzuri. Ninaomba tuendelee nayo nchi nzima badala ya kuwapa pesa, wengine wanakwenda kuolewa, kuoa, wengine wanakwenda kulipa mahari na wengine wanakwenda kujinyosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa tuje na mkakati kama ambao nimeuona Mwanza, tuupeleke nchi nzima. Badala ya kuwapa pesa, tuwanunulie kuku wakafuge, tununue mbuzi wakafuge, vitu ambavyo vinachochea maendeleo ya familia na kipato cha mtu mmoja mmoja katika ngazi ya familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TAKUKURU; ninawashukuru TAKUKURU wanafanya kazi nzuri na nimeangalia nchi nzima wanajitahidi kujenga nyumba na infrastructure za wafanyakazi wetu. Baadhi ya wilaya hatujafika kuwajengea majengo yao, inawezekana ndiyo chanzo cha malalamiko ya ndugu yetu pale. Moja ya wilaya ambazo hatujafika na Mkurugenzi aliahidi ni Muleba, hatuna nyumba na makazi ya TAKUKURU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona wamefanya kazi nzuri katika baadhi ya wilaya na mkakati unaendelea wa kuwajengea miundombinu kwenye wilaya mbalimbali. Ninaomba kipaumbele tuweke Wilaya ya Muleba kwa sababu, nimekuwa kwenye Kamati hii huu ni muhula wangu wa pili na wameahidi kufanya hiyo kazi. Nimeangalia majengo wanayoishi, sijui kama Mheshimiwa Waziri amewahi kufika pale?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika pale ukaingia ndani, jengo lao halifai. Kwa hiyo, ninaomba mwaka huu mjomba tukajenge Jengo la TAKUKURU, Wilaya ya Muleba. Kwa kazi nzuri ambayo inafanywa na Wizara yake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niunge mkono hoja ambayo iko Mezani kwetu. Ninashukuru sana.