Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninapenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyenijalia kusimama leo katika Bunge lako hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba niseme kwamba, mimi ni sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria. Ninaomba niungane na maneno mazuri ambayo ameyasema Makamu Mwenyekiti wa Kamati na kwa uzuri wa maneno ambayo amesema na hasa kuelezea dhana ya utawala bora, ninaomba nisiharibu ule utamu, niunge mkono na hii ibaki kwenye kumbukumbu kwamba ninakubaliana na maneno mazuri ambayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nimpongeze Waziri, Ndugu yangu Ridhiwani Kikwete, Naibu Waziri na watendaji wote katika hii Wizara. Kama nilivyosema kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati. Miongoni mwa Wizara ambazo tunafanya nazo vizuri kwenye Kamati ni pamoja na hii Wizara. Hata pale ambapo tumegundua kama kuna tatizo, sisi kama Kamati tunapotoa ushauri, Wizara hii imekuwa ikisikia na kwenda kufanya marekebisho. Ninakupongeza sana ndugu yangu Ridhiwani na viongozi wote kwenye Wizara. Tunathamini na tunaheshimu kazi kubwa ambayo wameifanya kupitia hii Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, kwa Waziri na Viongozi wa Wizara, lakini ninaomba nipongeze kwa upande wa TAKUKURU. TAKUKURU ni miongoni mwa taasisi ambazo sisi kwenye Kamati yetu tunafanya nao kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utakumbuka kabla ya kikao hiki cha Bunge sisi Wabunge tulienda kutembelea miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na taasisi hizi ambazo zinaitika kwenye Kamati zetu. Miongoni mwa taasisi ambayo inafanya vizuri ni pamoja na TAKUKURU. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kukagua miradi ya maendeleo, miradi ambayo Serikali hii inapeleka pesa kwa ajili ya kujenga majengo mbalimbali. Tumethibitisha kwa maeneo yetu kazi ambazo zinafanyika. Ninaomba nizungumzie mradi mmoja tu. Tulitembelea Mkoa wa Geita, kwenye Wilaya ya Nyang’hwale kama nitakuwa sijasahau. Kuna ujenzi ambao umefanyika pale wa ofisi ya TAKUKURU. Zimetumika pesa zaidi ya milioni 380 na kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nipongeze, mradi ule ni mzuri sana na maelezo ambayo yametolewa katika mradi ule hata sisi Wabunge tumeridhika sana na kazi inayofanywa na Taasisi ya TAKUKURU. Ninaomba nimpongeze Mkurugenzi, lakini niwapongeze na watumishi wote kwenye hii Taasisi ya TAKUKURU kwa kazi nzuri wanayoifanya na nimesema nisirudie maneno mazuri ambayo yameelezwa na Wabunge wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi kwa taasisi hii ya TAKUKURU, ninaomba sasa nijielekeze kwenye michango yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumze kwa suala la TASAF, wanufaika wa TASAF. Tunaishukuru sana Serikali yetu na kwa kweli lengo la Serikali na kupitia hii Miradi ya TASAF ni kusaidia kaya maskini. Tukizungumzia kaya maskini ni zile ambazo tunazo sisi kwenye maeneo yetu ambayo tunayawakilisha. Ninaomba nishauri kwenye hili eneo na hasa kwenye suala la uhakiki wa wanufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hivi karibuni wamepita kuhakiki wanufaika. Kama kweli tunakusudia kusaidia kaya maskini, ikiwemo na wale maskini ambao wapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na Mkoa wangu wa Ruvuma. Ninaomba niishauri Serikali tuendelee kufanya uhakiki kwa sababu kuna udanganyifu ambao unafanyika, tunawaacha wanufaika tunakwenda kuchukua watu wengine, hii haileti afya kwa lengo la mradi wetu. kwa hiyo, niombe kupitia hii Wizara, pamoja na kazi nzuri ambazo wanafanya twendeni tukahakiki hawa wanufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, kwenye huu Mradi wa TASAF wasimamizi wanakuwa Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji na wajumbe wao na sisi sote tutakuwa mashahidi kwamba wale wajumbe wanafanya hizi kazi hata hao wenyeviti hawalipwi chochote. Sasa itakapotokea kwamba mjumbe wa Kamati (Mwenyekiti wa Kijiji, wa Kitongoji au wale viongozi wengine) kama wana haki kuwa sehemu ya wanufaika, waingizwe kwa sababu inaleta kero sana pale kwenye maeneo yao katika utekelezaji ukiwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kijiji, huruhusiwi kuingia kwenye TASAF hata kama una vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, waende wakarudie, wakaangalie kwenye maeneo ambayo yanaleta changamoto, kama wapo viongozi, kwenye hili tuondoe hiki kikwazo. Kwa sababu ninataka nikwambie Mheshimiwa Waziri ni kweli kabisa wapo watu hawana uwezo hata wa kupata milo mitatu. Sasa lazima tuangalie, tuendelee na dhana ya huu mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niliona nisisitize na ninao ushahidi wa haya maeneo ambayo yapo na hao watu ambao nina uhakika kabisa, lakini mwisho wa siku ninakuta wale hawapewi wanaenda kuingiza watu wengine. Kwa hiyo, niliona niliseme hili kwenye suala la uhakiki wa wanufaika wa TASAF. Tuangalie kaya zile ambazo zina shida kabisa, unaweza ukakuta kwenye kaya kuna mlemavu, kuna mtoto amechaguliwa kwenda kujiunga na shule, lakini anashindwa kwenda kwa ajili ya uwezo. Hii TASAF inasaidia sana, imeondoa watu katika umaskini. Watu wamekuwa na miradi mbalimbali kupitia TASAF. Sasa twende tuangalie ili tuendane na malengo ya huu mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitamani nichangie kwenye hili eneo, ni suala la uhamisho. Uhamisho ni haki ya watumishi, lakini kuna maeneo tunapata changamoto na hasa nizungumze kwa upande wa wanandoa. Ninapata shida sana kwa sababu nakuta wanandoa wengine ni vijana, wanashindwa kuvumilia matokeo yake tukiwaacha wanaishi peke yao, tunashangaa tunaongeza watoto wa mitaani ni kwa sababu hatujazingatia kwenye haya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe kama yule mwanandoa anayekaa kwenye eneo linalohusika, pengine ni mtumishi ametimiza miaka mitatu anapoomba kuhama, aidha, kumfuata mume wake au mke wake tuwaruhusu waende. Matatizo ni makubwa, mimi leo ninayezungumza hapa nina takriban miaka 60, ninaelekea kwenye miaka 60, inawezekana ningekuwa mtumishi uvumilivu ungekuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vijana wanashindwa kuvumilia, lazima atafika mahali atatafuta maeneo ya kujinyoosha. Akijinyoosha mwisho wa siku tunapata watoto, tunalalamika tuna watoto wa mitaani, lakini wakati mwingine tunachangia. Niliona nilisema hili sana na nisisitize, haki ya uhamisho ni haki ya kila mtumishi. Wanapotaka kuhama basi tuhakikishe tunawapa uhamisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie jambo dogo, suala la nyumba za watumishi. Mheshimiwa Waziri kwenye taarifa yake amesema, tunakusudia kujenga nyumba 132, ninaomba zile nyumba na Tunduru tuzipate, wapo watumishi wanapanga na mtumishi mwingine anashindwa kufanya kazi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)