Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba hii muhimu ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye mchango wangu nitumie fursa hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania. Nitumie fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anaiongoza nchi yetu hasa kwa mujibu wa Katiba, Sheria na kanuni ambazo zimepitishwa ndani ya Bunge letu Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kama tutakumbuka wakati anachukua kijiti cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuta nchi hii mikutano ya hadhara yote imefungwa, alikuta siasa hazifanyiki, lakini kwa lile lengo lake la Utawala Bora na kutaka kuongoza kwa mujibu wa Sheria na Katiba yetu alifungulia mikutano ya hadhara na Vyama vya Siasa vyote vilianza kufanya siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya utawala bora ni pamoja na ulinzi wa rasilimali. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tumeona amefanya hilo kwa mfano, hivi tumeshuhudia amemaliza kuzungumza kaka yangu pale Mheshimiwa Swalle (Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria) namna ambavyo Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeburuza watu Mahakamani wale ambao walikuwa wanajaribu kuteteresha rasilimali za nchi hii. Serikali imechukua hatua na tumeshuhudia kwa macho yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawakumbusha Waheshimiwa Wabunge suala la utendaji wa PCCB, imefanyika hata ndani ya chama chetu. Tumetoka kwenye uchaguzi tumeona ni namna gani PCCB wamefanya kazi yao kubwa katika uchaguzi, lakini hata baada ya uchaguzi. Tumeshuhudia mpaka sasa pale Chato wapo Wabunge wenzetu wanatoa ushirikiano pale, TAKUKURU wamewafikisha pale. Ule ni utawala bora, ni utawala bora upi tunaouhuitaji kwa mfano? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anafanya katika kuiongoza nchi yetu kwa mujibu wa utawala wa sheria. Hili tumeliona siyo tu ndani ya Serikali na hata ndani ya chama chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala hapa la utekaji na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani namna ambavyo ametoa mwongozo. Ifikie mahali Serikali yetu ishughulike na wale ambao wanajiteka, wapo watu ambao wanajipoteza hawaonekani. Tumeshashuhudia watu wa aina tofauti tofauti wamepotea katika mazingira ya kanisani, au misikitini, baadaye wameonekana, kumbe walikuwa na agenda zao za kifamilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku mtu anaweza kuja na hoja nyepesi akadhani kwamba kuna utekaji ambao uko rasmi wakati kumbe ni utekaji ambao hauko rasmi na kila mtu amefanya kwa mujibu wa uwezo wake wa kufikiria. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali iwashughulikie wale wote ambao wanasambaza taarifa za uongo juu ya masuala hayo ya utekaji ili kuilinda nchi yetu na kuilinda Serikali yetu juu ya watu wenye nia mbaya ya kuichafua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa niende kwenye mchango wangu wa siku ya leo. Mwaka 2015 - 2020, Serikali ilizuia kabisa vibali vya kutoa ajira nchini. Kipindi cha miaka mitano hivi baadhi ya maeneo ajira hazikutoka kabisa, lakini baada ya mwaka 2021 kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mpaka 2025, Serikali ilitoa vibali vya kuajiri maeneo mengi katika sekta nyingi. Hii inathibitisha kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kutoa ajira kwa Watanzania na kwa vijana wa Watanzania kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme jambo moja, nimejaribu kufanya tathmini katika mfumo wetu wa ajira nchini. Ukiangalia wanafunzi wanaohitimu vyuo vikuu nchini, elimu ya juu peke yake ni takribani wanafunzi 49,000 kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wanaohitimu elimu ya kati ni takribani wanafunzi 150,000 kila mwaka. Kwa hivyo, kila mwaka tuna wahitimu takriban 200,000 mpaka 210,000 hivi. Serikali yetu ina uwezo wa kuajiri wahitimu takribani 45,000 mpaka 55,000 yaani 25% mpaka 30% ya wahitimu wa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kutoa ajira kwa Watanzania, ni lazima sasa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Menejimenti nzima ya Wizara hii, tufikirie namna ya kutengeneza ajira nyingi tena rasmi, nje ya ajira za Serikali. Bunge lilileta mjadala katika Bunge lililopita, tulikuja hapa tukashauri tukasema, kwa sababu uhitaji wa ajira ni mkubwa, hatuajiri siyo kwa sababu hatuna gaps (hatuna uhitaji), hapana. Hatuajiri sababu ya uwezo wa kuajiri wa Serikali. Bajeti ya ajira bado haina uwezo wa kuajiri wote wanaohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ndivyo hivyo, tulishauri uwepo wa mwongozo wa ajira kwamba, wale wanaojitolea wote warasimishwe kwa utaratibu maalum, watengenezewe namna ya posho au kitu cha namna hiyo ilimradi kukimu maisha yao. Kwa sababu kwanza, watakuwa wamepunguza gap la watumishi katika maeneo wanayokwenda kujitolea. Pili na wao watakuwa wamepata sehemu ya kukimu maisha yao wakati wanasubiri ajira rasmi zitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, mtaalam yeyote akienda kuwekwa kwenye eneo ambalo siyo la kitaalam kwa muda mrefu, utaalam wake unafifia au unapotea. Mtu yeyote ambaye amesomea, kwa mfano, mimi nimesomea ualimu, ni mwalimu by professional, lakini zaidi ya miaka 15 sipo darasani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo huwezi kuniajiri ukaniambia nifundishe watoto halafu utegemee matokeo mazuri, haiwezekani. Haiwezekani kwa sababu professional lazima uiishi, lazima ujifunze kila siku, lazima u-practice (ufanye mazoezi). Sasa kwa sababu hiyo, tukaja hapa na ushauri katika Bunge lililopita tukasema, hawa watu waliohitimu, kwa sababu tunawahitaji, isipokuwa kwa sasa hatuna uwezo wa kuwaajiri, tuwawekee internship wakae huko wajifunze waendelee kujinoa, waendelee kuwa watumishi wazuri. Ukifika muda wa kutumika iwepo na sehemu ya kwenda kuwachota na kwenda kuwaajiri bila kutumia taratibu hizi nyingi ambazo tunazitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ulikuwa ushauri namba moja. Ushauri wa pili… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba dakika moja niweze kuhitimisha. Nihitimishe kwa kusema hivi, tutatatua changamoto ya upungufu au tatizo la ajira kwa kuimarisha mifumo ya sekta binafsi iweze kuajiri kwa kuweka mazingira wezeshi ya wote ambao wanazalisha ajira. Serikali ikiwaunga mkono, ikaweka mazingira mazuri, basi wakianza kuajiri huko tutatatua kwa urahisi tatizo la ajira Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana,na ninaunga mkono hoja. (Makofi)