Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii na ninaomba ku-declare interest kwamba ni Makamu Mwenyekiti wa Wizara hii ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwanza nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ridhiwani Kikwete, Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kwenye hii Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niwapongeze Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu na Wakuu wa Taasisi mbalimbali chini ya Wizara hii. Ninataka nianze kwa kuchangia eneo muhimu sana hasa eneo la Utawala Bora. Ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu ninafanya kazi kwenye hii Kamati, kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Waziri imeeleza mambo mengi ya msingi kuhusu Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya eneo ambalo limesemwa ni juu ya kazi nzuri inayofanywa na Taasisi ya TAKUKURU nchini. Ninaomba nirejee takwimu, nimemsikia mdogo wangu Mheshimiwa Ado, amezungumza hapa ameamua kutafuta habari nzuri kaacha taarifa nzuri ya kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye taarifa kuhusu mapambano ya rushwa, TAKUKURU imeendesha kesi 664 na imeshinda kesi 260, kesi 300 zinaendelea Mahakamani. Kwenye kesi hizo TAKUKURU wameokoa zaidi ya bilioni 102. Pia kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri TAKUKURU wamepitia miradi mbalimbali ya majimboni kwetu Waheshimiwa Wabunge miradi 885. Katika hiyo miradi, miradi 13 imebainika kuwa na kasoro na TAKUKURU imeokoa zaidi ya trilioni 1.3 kwa ajili ya faida ya Serikali ya walipakodi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi taarifa imesema uko msemo unasema “Usiboziba ufa utajenga ukuta.” Lakini pia, kuna msemo unasema “Samaki mkunje angali mbichi.” TAKUKURU wamefanya kazi kubwa sana ya kuunda klabu za rushwa za shule ya msingi na sekondari zaidi ya 4,000 nchi nzima ya Tanzania ili kuwaelimisha Watanzania wachukie rushwa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nitumie nafasi hii kama kuna jambo Mheshimiwa Rais amelifanya kwa weledi mkubwa ni kuwezesha TAKUKURU iweze kufanya kazi yake vizuri. Ili uone dhamira hiyo, sisi kwenye Kamati tulipitia miradi mbalimbali ukiona miradi ya TAKUKURU inavyojengwa kwa viwango vya mfano utaamini kwamba TAKUKURU ni chombo ambacho kinaisaidia sana hii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie pia wako watu mahali fulani waliwahi kupuuza uwezo wa polisi kwenye nchi yao. Ninataka nikwambie polisi wasipofanya kazi yao ndiyo utajua umuhimu wa polisi. Kwenye hii nchi yetu TAKUKURU wasingekuwepo na kufanya kazi nzuri wanayoifanya ndiyo ungejua umuhimu wa TAKUKURU hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa Mheshimiwa Ado jana kwenye Wizara ya Mipango na Uwekezaji tumesomewa hapa, nchi yetu ya Tanzania kwa hivi sasa inaongoza kwa kuvutia uwekezaji Afrika Mashariki. Kwa muda wa miezi nane Tanzania uwekezaji wamesajili miradi ya uwekezaji 611, tafsiri yake ni kwamba nchi yetu inaaminika na utawala bora unakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri hapa imesomwa tarehe 31 Machi, juzi tu nchi yetu imeidhinishiwa fedha zaidi ya dola milioni 300 na Benki ya Dunia kwa ajili ya TASAF hii ni kazi nzuri ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama hilo halitoshi, utawala bora maana yake ni nini? Utawala bora una mambo mengi. Juzi hapa Mheshimiwa Waziri wa Bunge, Sera na Uratibu Chief Whip alisema ndani ya Bunge hili akapongeza uteuzi wa Eveline Munisi kuwa Mbunge kwenye hili Bunge kutoka Chama cha NCCR Mageuzi. Hiyo ndiyo maana ya uongozi jumuishi, ndiyo maana ya utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo lingine kuhusu uwazi. Kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri hapa imesemwa vizuri sana, sasa hivi miradi yote nchini ili kudhibiti rushwa na ubadhirifu tenda zote zinaombwa kwenye Mfumo wa NeST siyo kwa upendeleo, huo ni uwazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ili kuimarisha uwazi hapa nchini Serikali imeunda Mfumo wa E-Mrejesho. Sasa hivi wananchi wanaruhusiwa kuongea na viongozi wao moja kwa moja kuanzia Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa mpaka Wakuu wa Wilaya. Hii ndiyo maana ya utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo lingine la muhimu sana. Ukifanya tathmini ya kazi ambayo TAKUKURU inafanya kazi ambayo vyombo vingine kama vile Mahakama inafanya, wote wanashuhudia Waheshimiwa Wabunge huu ni mfano muhimu ninaoutoa sasa, juzi wameshuhudia Mahakama ya Rufani imeifungulia CHADEMA kufanya siasa nchini, huu ni utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi mama Samia amesema ndani ya Bunge hili, kwamba anataka kurejesha tabasamu kwa Watanzania na amekuja na 4R. Nami nikiwa Mbunge wa Awamu ya Pili humu ndani ninafahamu katika jambo Mheshimiwa Rais amekusudia kulifanya ni kuimarisha Mfumo wa Haki Jinai ambao Mheshimiwa Ado anauzungumzia ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye taarifa Mfumo wa Haki Jinai ambao utakuja kuleta mabadiliko ya sheria mbalimbali zitakuja ndani ya Bunge ili kuboresha utawala wa Haki Jinai na Kutenda haki mbalimbali kwa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote ni muhimu sana kwenye hiki kipindi kwa kazi ambayo mama Samia anaifanya kwa nchi hii tuendelee kumuunga mkono, mama anaipenda Tanzania, mama anapenda vyama vyote, mama anampenda kila mtu. Tukimuunga mkono kwenye ndoto aliyonayo, nina uhakika nchi hii tutazidi kwenda mbele vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri hapa, utakuwa shahidi, kwa muda huu wa miaka mitano ya mama Samia Suluhu Hassan hata manunguko ya watumishi maeneo mbalimbali yamepungua sana. Madaraja yamepandishwa, mishahara imepandishwa, tumeona hapa kwenye mpango wa Watumishi Housing, nyumba za watumishi pia zinajengwa kwenye wilaya, halmashauri, mikoa ili kupeleka tabasamu kwa watumishi na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kama Mjumbe wa Kamati hii ninaomba tuitie moyo Kamati, tuiunge mkono bajeti hii, tuipitishe kwa kishindo ikatekeleze majukumu ya kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ninataka nimhakikishie Waziri,sisi kama Kamati tumepitia miradi mingi, tumepitia taarifa nyingi za TAKUKURU na mamlaka mbalimbali. Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mnyonge mnyongeni, haki yake apewe, lakini wizara hii inafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha. Ninataka nitoe rai Mheshimiwa Waziri kwamba kazi yako ni njema, tunaliunga mkono Bunge na kwa sababu hii Wizara iko chini ya mama Samia Suluhu Hassan tunamuunga mkono na kumtakia kila la kheri kwa utumishi wa nchi yetu. (Makofi)