Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Tunduru Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kuniona ili niweze kutoa mchango wangu katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Utawala Bora na Utumishi. Nina mchango kwenye maeneo kadhaa. Maeneo mawili ya mwanzo yanajikita katika eneo la utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumradhi, nimeisikiliza Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Ridhiwani Kikwete, hasa kule mwishoni. Kule mwishoni, Mheshimiwa Waziri anatoa commitment kwamba wataendeleza utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, utawala bora haudondoki mbinguni, utawala bora unataka misingi: misingi ambayo lazima uifuate, usipoifuata ahadi, kwamba utawala bora utakuwepo inabaki kuwa ni maneno matupu. Kwa ajili ya muda nitaitaja misingi miwili muhimu; msingi wa kwanza ni mahusiano baina ya utawala bora na kuimarisha uwazi na harakati ya kupinga rushwa na ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mahusiano ya moja kwa moja baina ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika Serikali. Kwa maoni yangu; nikitazama mwenendo hasa kwa kuiangazia taasisi yetu ya TAKUKURU, ninaona bado tuna safari ndefu sana. Kwa mfano sisi ACT-Wazalendo huwa tunafanya uchambuzi wa kina wa report za CAG. Kwenye kila report moja ya eneo ambalo tunalitazama huwa tunaangalia ni fedha kiasi gani tunazipoteza kutokana na rushwa, kutokana na uzembe, kutokana na ubadhirifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi wetu wa Taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2023/2024 inaonesha kwamba fedha ambazo tumezipoteza kutokana na ubadhirifu pamoja na uzembe ni takribani shilingi trilioni 2.5. Hii kwa wakati ule ni zaidi ya asilimia tano ya bajeti nzima ya Serikali, lakini ukitazama kiwango cha fedha ambacho TAKUKURU wanasema wanakiokoa kila mwaka, nimetazama mwaka uliofuata baada ya ile taarifa fedha ambazo tuliziokoa ni takribani kwa taarifa yangu ni shilingi 14,000,000,000.
MHE. JOSEPH E. TAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa inatoka kwa nani? Haya karibu.
TAARIFA
MHE. JOSEPH E. TAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba nimpe tu taarifa mchangiaji kwanza kwa kuheshimu kanuni angekaa. Hapa tunajadili hotuba ya Wizara ya Utumishi wa Umma, hatujadili taarifa ya CAG.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji amesema ameisoma hotuba, ukienda ukurasa wa 17 mpaka wa 22 imeeleza vizuri kazi zilizofanywa na TAKUKURU.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado Shaibu Ado, unaipokea taarifa hiyo.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jambo ambalo linabidi litazamwe kwa kina kwa heshima ya Bunge ingawa taarifa zinaruhusiwa ni kwamba taarifa zinazokuja ziwe na msingi zisije kwa lengo la kumpotezea muda mzungumzaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninakwenda huko huko ndiko ninakokwenda nimetoka 2023/2024 unakuwa na ubashiri gani kwamba sitokwenda 2025/2026, niachwe nizungumze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Wizara kwenye hotuba yake inaonyesha progress ya bilioni 102 zilizookolewa. Nikifanya uwiano wa kiwango cha fedha tunachokipoteza na ile product tunayoipata kwa jitihada za TAKUKURU, hitimisho ninaloweza kuweka ni kwamba sioni jitihada za dhati za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kupambana na rushwa na ufisadi hasa rushwa kubwakubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaona hivyo nitakapoona yale masuala makubwa yanayobeba upotevu wa mabilioni ya shilingi, TAKUKURU ielekeze nguvu zake huko badala ya kuweka mkazo mkubwa kwa upotevu mdogo wa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni msingi wa mahusiano baina ya utawala bora na haki za binadamu hasa hali ya kuishi. Bila haki za binadamu hakuna utawala bora. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu mwaka jana kilitoa taarifa yake ambayo ina orodha ya watu wengi ambao wamepotea hawajulikani waliko ama wametekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa hiyo ilitanguliwa na taarifa ya Chama cha Wanasheria Tanganyika. Baada ya hapo mpaka sasa viko visa mbalimbali wanaopotea, watu wanaotekwa. Nilitarajia kwa sababu hii ni Wizara ya Utawala Bora, ni lazima tupate pia commitment kwamba kutakuwa na usalama dhidi ya visa vya watu kupotea na kutekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali; orodha ya watu wanaotajwa Balozi Humphrey Polepole, ndugu yetu Mlay na wengine wote waliotajwa katika ripoti zile kwa ajili ya muda siwezi kuwataja wote, ni lazima tupate majibu ya Serikali. Pawe na uchunguzi huru dhidi ya watu wote waliopotea na kutekwa Tanzania. Hilo ni la pili ambalo nilitaka kulisema.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ujumbe wangu wa kuhitimisha ...
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Katambi, taarifa.
TAARIFA
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge na nikiheshimu pia taaluma yake. Amezungumzia kuhusiana na masuala ya kesi za TAKUKURU na vivyo hivyo amezungumzia kuhusiana na mwenendo wa kesi za jinai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpe taarifa nikitambua kwamba pia ni wakili msomi, yapo mashauri ya jinai yanayoendelea kwenye Mahakama zetu yanayohusiana na ubadhilifu na upotevu wa fedha za Serikali. Kwa sababu ya muktadha wa takwimu pale atakapohitaji tutampatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, kwenye tuhuma na shutuma za watu kutekwa na kupotea. Zipo kesi ambazo tayari ziliripotiwa polisi hatua za upelelezi zinaendelea, lakini, zipo kesi ambazo watu walionekana kusema wametekwa na baadaye ikagundulika ndivyo sivyo. Zipo shutuma nyingine nzito za kijinai ambazo Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi nazo na kwa kushirikina na vyombo vingine vya kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye haya masuala ikiwa ni pamoja na kesi zilizopelekwa Mahakamani, unafahamu msingi wa sheria unatutaka kwenye mashauri ambayo yanaendelea Mahakamani hayawezi kuzungumziwa pamoja na kutambua kwamba tuna Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, lakini yapo mambo ambayo kwa hatua yalivyo na nature yake kwa sababu yapo kwenye hatua ya upelelezi, kwa sasa hayawezi kuwa public kwa sababu kuna taratibu za kiupelelezi. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ado Shaibu Ado, unapokea Taarifa hiyo?
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa hiyo. Nitahitimisha kwa ajili ya muda, ninaamini kwamba nitalindwa. Nahitimisha dakika moja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei kwa sababu hoja yangu siridhiki na uchunguzi wa kawaida wa kijinai. Ninataka pawe na utaratibu wa Judicial Commission of Enquiry (Uchunguzi Huru) ili tujue Polepole yuko wapi, tujue Deus Soka yuko wapi. Sasa ujumbe wangu...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ujumbe wangu nimeongea kwa dakika tatu nikisimamishwa, dakika moja ninaomba ili nitoe ujumbe. Ujumbe wangu kwa wale wanaodhani...
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea kwa dakika tatu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa
MHE. ADO S. ADO: Ninaomba kwa heshima, ninatoa ujumbe tu...