Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninaungana na waja wema kumshukuru sana Mwenyezi Mungu wingi wa rehema kwa kutujalia baraka ya uzima na afya na hatimaye kuweza kuwa kwenye jengo hili Tukufu kwa ajili ya kujadili mustakabali wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia niungane na wenzangu kuwa sehemu ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye amewasilisha hapa Bungeni. Kwa kuanza kabisa ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uwasilishaji na mpangilio wa vipaumbele vya kitaifa ambavyo yeye kama msimamizi wa shughuli za Serikali hapa Bungeni na msimamizi wa shughuli za Serikali nchini ametenda haki inayotosha kabisa kutupa matumaini kwamba tunakwenda kupata matokeo chanya kutokana na hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza moja kati ya hotuba yake wakati tukipitisha jina lake kwenye Bunge hili, alipokuwa anawasilisha salamu zake za awali za shukrani na mwelekeo wa namna atakavyomsaidia Mheshimiwa Rais kazi, aliweka wazi hotuba iliyoakisi huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limekwenda kujionesha pasi na mashaka yoyote alipokuwa akifanya ziara zake nchini kwa kuyafikia matatizo ya watu pengine na kuyatatua kabisa kwa wakati muafaka na kuleta matumaini mapya. Hii ni dira njema na huu ni mwelekeo ambao sisi tunaufurahia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika hotuba yako ume-quote vizuri kabisa Kitabu cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Mwaka 1974 kinachoitwa, Mtu na Maendeleo, katika nukuu ya kitabu hiki kinasema: “Maendeleo ya kweli huanza pale wananchi wanapoanza kuzalisha chakula cha kuwatosha wenyewe”, msingi wangu katika kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kuona umuhimu wa sekta ya uzalishaji nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele na msisitizo mkubwa sana wa kuongeza uzalishaji kupitia ongezeko la mbolea na ruzuku zinazotolewa katika pembejeo mbalimbali za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye hotuba imeweka wazi kabisa jumla ya tani 1,000,000 za mbolea zimetolewa na kupelekwa kwa wananchi na jumla ya wakulima zaidi ya 500,000 wamenufaika kwa fedha za kitanzania shilingi trilioni moja, hii ni ishara tosha kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametazama sekta ya uzalishaji kama ndiyo kichocheo muhimu kitakachotuvusha na kutupa uchumi wa uhakika nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunajua Serikali haiwezi kuchoka kuhudumia, Serikali haiwezi kuchoka kutengeneza matajiri na Serikali yetu haiwezi kuchoka kutengeneza uzalishaji wenye tija utakaotoa matokeo ndani na nje ya nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwenye maeneo mawili kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, moja...
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Zuberi Mfaume.
TAARIFA
MHE. ZUBERI Y. MFAUME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vema tukakinukuu kwa usahihi Kitabu cha Mwalimu Nyerere hakuna kitabu cha Mtu na Maendeleo bali ni Binadamu na Maendeleo. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Fadhili Liwaka, unapokea, taarifa hiyo?
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea. Ninashukuru kwa masahihisho hayo mazuri na nukuu yetu iko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango kwenye maeneo mawili, eneo la kwanza, ili tuweze kuboresha na kuhakikisha uzalishaji wa watu wetu unakuwa stahimilivu ni muhimu tukatazama eneo la wanyama waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niweke record yangu vizuri kabisa Tanzania inielewe, Afrika inielewe na dunia inielewe. Mimi sina shaka na rasilimali za wanyama pori hususani ndovu walioko nchini. Kwanza, ninaipongeza Serikali yangu kwa kuweza kupambana na ujangili na kuweza kusaidia ongezo la wanyama hawa wenye thamani kubwa dunia, ninatoa pongezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ni mmoja kati ya mabalozi wazuri wanaotaka wanyama hawa walindwe, lakini utakubaliana nami hata mwili wa binadamu ukiongezeka uzito ni sumu. Hivyo, basi wanyama hawa sambamba na jitihada kubwa na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu alijibu swali la papo kwa papo kwa usahihi kabisa kwa kulinganisha kwamba wanyama hawa wanaingia kwenye sura ya mikataba ya kimataifa, lakini sisi kama nchi tunaomba jitihada ziongezeke katika kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanabaki salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoka Jimbo la Nachingwea, Jimbo la Nachingwea pekee yake takwimu za uzalishaji mwaka 2023/2024 tulizalisha tani 140,535, mwaka 2024/2026 tumezalisha tani 103,470 kuna upungufu wa tani 37,065.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini, kuna upungufu huu? Kwa sababu wakulima moja, wameacha kulima kwa kiwango kikubwa kwa kuhofia ndovu waliopo kwenye maeneo yetu. Wameacha kuweka jitihada kwa sababu hata wakiweka kwa ekari nyingi bado wanyama waharibifu wanakwenda kuharibu mazao yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itazame nyongeza ya jitihada za kuhudumia maeneo haya: moja, waongeze hizi ndege nyuki kazi nzuri inafanyika; pili, kuongeza vituo vya askari wa wanyama pori; na tatu, elimu iendelee kutolewa wakati tunaangalia njia bora za kiteknolojia ya dunia ya sasa katika kukabiliana na hawa wanyama (ndovu).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwenye eneo hili, ni kuomba fidia kwa wakulima waliopata madhara. Serikali imefanya kazi kubwa wanatoa fidia, lakini bado fidia hii haiwezi kuwafikia wote. Hivyo tunaomba usimamizi na speed katika kulipeleka jambo hili ili wananchi wetu waweze kupata manufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili pia la uzalishaji tuna jambo la migogoro ya wakulima na wafugaji: ninaomba Serikali ilichukue jambo hili kwa uzito mkubwa na bahati nzuri sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mbobezi katika eneo hili la utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji, alifanya hivyo kwa miaka iliyopita na sasa ninaamini anao uwezo wa kusimamia sekta zilizopo ili tatizo hili liishe. Tusiwe na jambo la uadui kati ya wakulima na wafugaji bali tuwe na maelewano na uzalishaji unaofaa sambamba na jitihada ambazo zinafanywa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nimalize mchango wangu kwa jambo moja na hapa niruhusu tu nizungumze kwa rika yangu ya ujana. Sisi vijana tuliolelewa kwenye misingi ya Chama cha Mapinduzi ambao tuko ndani ya Bunge na tuko nje ya Bunge huwezi kutushauri chochote juu ya kumpigania, kumsemea na kumsimamia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikuhakikishie kwa umri wangu nimeanza kuipenda siasa mwaka 2005 wakati Rais wa kwanza akiwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, nilimsemea, nilimpigania na nilikuwa form two na alivuka salama hiyo ni kazi ya kijana wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 aliingia Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, nilikuwa Mjumbe wa NEC nilimsemea, nilimpigania, nilimwombea kura mpaka Mungu alipoamua, bado nilikuwa ninamsemea kwa nguvu kubwa na nina ujasiri wa kusimama mbele ya Bunge lako bila uwoga wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 akaingia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tunaye mpaka sasa, ninataka nikuhakikishie tutamsemea, tutamsimamia, tutamshauri. Hatutaogopeshwa na majina yanayoitwa mara chawa au tunaitwa majina ya kujipendekeza, huu ni wajibu wa msingi kwa kijana aliyepata malezi ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalize kwa kusema jukumu hili hatujipi ili tulipwe, jukumu hili tunajipa kwa sababu tunamtaka Mama Mheshimiwa Dkt. Samia tunapomsemea na kumtia moyo akajenge mabweni ya watoto wetu wasitembee umbali mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tunapomsemea Mheshimiwa Dkt. Samia akawatue mama zetu ndoo kichwani watembee na maji kwenye ndoo kutoka jikoni kwenda kuyaweka ndani. Tunapomsemea na kumlinda Rais wetu hatutaki malipo tunataka Mama huyu aimarishe diplomasia ya uchumi watu wa Mataifa waendelee kumwamini na nchi yetu izidi kupata heshima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, ninakushukuru sana kwa nafasi na Mungu awabariki. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)