Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Jacqueline Chrisant Mzindakaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JACQUELINE C. MZINDAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza, kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipata kibali cha kuwepo mahali hapa ikiwa ni mara yangu ya kwanza katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda vile vile, kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu, lakini pia na Chama changu Cha Mapinduzi. Hata hivyo, kipekee ninaomba niwashukuru wapiga kura wangu wa Mkoa wa Rukwa (wanawake) walioweza kunipigia kura na kupata ushindi wa kishindo, ninawaahidi sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba niendelee kwa kumpongeza kwanza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameweza kuifanya na ambayo anaendelea kuifanya. Sote ni mashuhuda katika siku zake 100 yale aliyoahidi katika kampeni za uchaguzi na ameweza kuyatimiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia niendelee kwa kumpongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambaye ameanza kwa kasi kubwa. Sisi Mkoa wa Rukwa amepita katika mkoa wetu, nami kwa niaba ya Mkoa wa Rukwa ninaomba nifikishe salamu za wakazi wa Mkoa wa Rukwa kwa kile ambacho umeweza kukifanya kwa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wakazi wa Mkoa wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea kufanya ziara hizo katika mikoa mingine, hakika Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hakukosea kupendekeza jina lake na Waheshimiwa Wabunge hatukukosea kumpa kura za kishindo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ninawapongeza sana, lakini nimtakie Mheshimiwa Waziri Mkuu kila la heri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na hapo, nitakwenda kupeleka mchango wangu katika maeneo mawili na maeneo hayo nitagusa eneo la afya; lakini vilevile nitagusa eneo la kilimo kwa kutambua mchango wa mkubwa wa Serikali yetu katika afya kwa kuboresha huduma ya mama na mtoto katika wodi ya wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Rukwa umeweza kupunguza vifo vya mama wajawazito kutoka vifo 128 katika vizazi hai 100,000 hadi kufikia vifo 60 katika vizazi hai 100,000. Vifo vya watoto wachanga vilevile katika Mkoa wetu wa Rukwa vimeweza kupungua kutoka vifo 11 katika vizazi hai 1,000 hadi kufikia vifo saba katika vizazi hai 1,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni mapinduzi makubwa na hii yote inatokana na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa na tumeona alipatiwa tuzo ya kitaifa kupitia Gate Foundation ambayo ni The Gate Goal Keeper Award ambayo aliipata mwaka jana 2025, lakini hivi juzi tumeona mwezi Februari alipokuwa Addis Ababa ametunukiwa kuwa kinara wa kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, tunatambua pia mchango mkubwa wa Serikali katika Mkoa wa Rukwa katika sekta ya afya ambapo tumeweza kujengewa hospitali za wilaya nne na vituo vya afya 39 na zahanati 219. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali hizo za wilaya, kuna Hospitali ya Wilaya ya Kalambo ambayo Serikali ilielekeza shilingi bilioni nne katika ujenzi wa hospitali hiyo ya Wilaya ya Kalambo. Hospitali hiyo ya Kalambo ina changamoto ya wahudumu wa afya ama watumishi wa afya kwa 70%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaomba Serikali sikivu katika dira ya maendeleo ili kupitia TAMISEMI waweze kulisimamia hilo na wahudumu hao au watumishi hawa wa afya waweze kuongezwa: hususan, madaktari wa upasuaji wa wanawake wajawazito, ambao katika kutimiza azma na dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kupunguza vifo ya wanawake wajawazito na watoto tutakwenda kwa kiasi kikubwa kusaidia kwa kupeleka madaktari hao wa upasuaji wa wanawake wajawazito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ninaomba nizungumzie Kituo cha Afya cha Kasu: Kituo hicho cha Afya cha Kasu, tumeona kimetengewa shilingi bilioni 1.3 katika ujenzi na Serikali na kinatoa huduma zote za afya ikiwepo huduma ya wodi ya mama na mtoto, OPD, vifaa tiba na kadhalika. Kituo hicho kina changamoto kubwa ya barabara na Mbunge wa Nkasi Kusini, kaka yangu jana alizungumzia hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ziara yake alielekeza barabara hiyo kupitia TARURA watupatie shilingi milioni 500 ili barabara hiyo iaanze kujengwa na kusababisha wananchi wa Nkasi na eneo la Kasu kupata urahisi wa kufika katika kituo hicho cha afya na kupatiwa matibabu na kuimarisha ustawi mzima wa afya ya Wanankasi na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba nijikite katika sekta ya kilimo, Mkoa wetu wa Rukwa uti wa mgongo wa uchumi wetu ni kilimo. Hata hivyo, tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kusaidia programu mbalimbali za maendeleo ya kilimo ikiwepo skimu za umwagiliaji sita ambazo zimejengwa katika Mkoa wa Rukwa. Vilevile, kwa Serikali kuendelea kununua mazao kupitia Wakala wa Hifadhi ya Mazao wa Taifa (NFRA). Pia tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ruzuku kwa pembejeo za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu: ninaomba Serikali ituangalie kwenye suala la ulipaji wa NFRA kwa mazao hayo ambayo wamenunua kwa wakulima waweze kuwalipa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba pia kiwango cha ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima kiongezwe; kwa sababu uzalishaji ni mkubwa sana, lakini kiasi cha mazao kinachonunuliwa hakikidhi, hivyo wakulima kubaki na mazao mengine bila soko. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iliangalie hilo katika mipango ya dira ijayo, ili kubaini namna bora ya kuongeza ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima wa Mkoa wa Rukwa, waweze kujikwamua kiuchumi, kwa kuwa sisi Rukwa tunategemea kilimo kama uti wetu wa mgongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, tunaomba pia kupitia skimu za uwagiliaji ziweze kuongezwa ili tuwe na kilimo endelevu tusitegemee tu msimu wa kilimo ili vijana wa Mkoa wa Rukwa na wanawake wa Mkoa wa Rukwa wazidi kujiajiri katika kilimo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba pia kwa mfano, kuhusu Skimu ya Umwagiliaji ya Katongoro ambayo Serikali ili elekeza shilingi bilioni 60. Tunaomba skimu hiyo ya umwagiliaji ambayo ilianza toka mwaka 2023 mpaka leo haijakamilika. Hivyo, tunaomba Serikali itusaidie ili skimu hiyo ya uwagiliaji ya Katongoro iliyopo katika Wilaya ya Nkasi, ikamilike na wakazi wa Mkoa wa Rukwa waweze kujiajiri na kujinyanyua kiuchumi kupitia kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja kwa 100%, lakini vilevile ninasema katika falsafa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kazi na utu, tunasonga mbele, tuendelee kupiga kazi na kuthamini utu wa Mtanzania, ahsante sana. (Makofi)