Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa ninapenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipa kibali. Kwa sababu toka Bunge la Kumi na Tatu limeanza leo ni mara yangu ya kwanza kusimama kuchangia. Kwa hiyo, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu, bila yeye nisingekuwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikishukuru sana chama changu, Chama cha Mapinduzi, kikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Mwenyekiti wetu kwa vikao vyote vilivyofanyika kututeua na kuniteua kuwa miongoni mwa wagombea na baadaye kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Rais, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Alitembea Tanzania nzima, akinadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi, nini atakifanya. Pia, aliahidi ndani ya siku 100 kuna mambo manne ambayo atakwenda kuyafanya, katika yale mambo manne ambayo aliahidi kwamba atakwenda kuyafanya yamekwishaanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni suala zima la kuwawezesha wananchi kiuchumi. Katika suala la kuwawezesha wananchi kiuchumi, mikopo ya 10% kwa mkoa wangu wa Shinyanga, tumefanya vizuri. Rais amefanya vizuri kwa sababu alitoa maelekezo, alitoa ahadi na wale watendaji wa Mkoa wa Shinyanga wameyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, dada yangu Mboni Mhita, lakini niwapongeze watendaji ambao ni Wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizopo katika Mkoa wa Shinyanga pamoja na Wakuu wa Wilaya kwa kusimamia, kuhakikisha kwamba ule utekelezaji, ile ahadi ambayo Mheshimiwa Rais, aliahidi inatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninawapongeza? Kwa Mkoa wa Shinyanga mpaka kufikia Januari, 2026 tayari halmashauri zote kwa ujumla wake zimetoa mikopo ya shilingi bilioni 3.4. Siyo fedha ndogo lakini haitoshi kila halmashauri imejitahidi kutoa mikopo kwa makundi maalum. Wanawake wamekopeshwa shilingi bilioni moja, watu wenye ulemavu wamekopeshwa shilingi milioni 56, vijana wamekopeshwa zaidi ya shilingi milioni 985. Siyo jambo dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vikundi 269 vimekopeshwa. Kwa hiyo tunaona ni jinsi gani maono na mipango ya Mheshimiwa Rais inavyotekelezwa kwa wakati. Aliahidi na kweli ametekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na kukopesha, mbali na makundi haya kupata mikopo, lakini kuna changamoto. Mwanzoni hizi fedha zilikuwa zinakopeshwa moja kwa moja kutoka halmashauri, lakini sasa hivi kwa ile mikoa ambayo imepewa kipaumbele kuweka majaribio ya ukopeshaji kuna changamoto. Sasa hivi wanatumia mfumo, unakuta kuna kikundi ambacho toka mikopo imeanza kinakopa na kurejesha, lakini kinashindwa kuja kupata mkopo mwingine baada ya kuwa wamemaliza rejesho kwa sababu tu mfumo hauwasomi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwenye suala zima la mfumo kuna haja ya kuangalia ni kitu gani kifanyike kuweza kuboresha hii mifumo. Kuna changamoto nyingine, watu wengine vikundi vingine wanawake wanakosa mkopo kwa sababu tu kwenye kile kikundi kuna watu hawana NIDA, kosa ni la nani? Wameshajiandikisha, wameshasajili kwa ajili ya kupata NIDA, lakini NIDA haipatikani, wanatumia muda mrefu, wakienda hata kuomba zile namba za NIDA sasa kwenye Ofisi za NIDA wanaambiwa mtandao haufanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wanakata tamaa, vijana wanakata tamaa, watu wenye ulemavu wanakata tamaa. Tunaomba Serikali, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kuhakikisha kwamba, vile vigezo ambavyo vimewekwa visiwe na vikwazo vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo ambayo imepangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ulikuwa mchango wangu wa kwanza. Mchango wangu wa pili katika mambo ambayo Mheshimiwa Rais alisema atayatekeleza ni suala zima la bima ya afya kwa wote. Ni ukweli usiopingika mpango huu wananchi wameupokea kwa shangwe na nderemo. Tukiangalia Mheshimiwa Rais, toka ameahidi siku 100 tayari zaidi ya wanufaika 1,400 na zaidi wameweza kunufaika, sawa na kaya 276,000, siyo jambo dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa bima kwa wote umepokelewa vizuri, niiombe Serikali kusimamia sasa upatikanaji wa dawa. Haipendezi mtu ana bima ya afya, anakwenda hospitali, anahudumiwa, anamwona daktari, anakwenda kwenye vipimo, inapofika kwenye suala la dawa anaambiwa hii dawa haipo nenda ukanunue, hii dawa siyo ya bima ya afya, lakini mtu akija na cash anapata ile dawa; haipendezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kumchonganisha Mheshimiwa Rais, ambaye amerahisisha huduma za afya kwa kuhakikisha kwamba Sheria ya Bima ya Afya inaanza kutumika Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaombe sana mamlaka ambazo zinahudumia, hasa kwenye ngazi ya afya ya msingi; kwenye vituo vya afya, kwenye zahanati na kwenye hospitali za wilaya ambazo zipo chini ya TAMISEMI, tuwaombe sana bima ya afya tunahamasisha kama Wabunge, tunatoa elimu ya afya, elimu kuhakikisha kwamba kila mtu anajiunga na bima ya afya kwa wote, itakapofika kwenye huduma basi apate huduma ambazo amezitarajia, ambayo ni matamanio ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba watu wake wote wanatibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuwalipia watu wanaopata magonjwa yasiyoambukiza wasio na uwezo ikiwemo saratani, kisukari na magonjwa mengine ya mifupa. Siyo jambo dogo ni jambo kubwa na niwaombe Waheshimiwa Wabunge, sisi Wabunge tunatumia muda mwingi sana kukaa humu Bungeni, toka asubuhi tunakuja mpaka sasa hivi bado tupo tumekaa, tufanye mazoezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magonjwa yasiyoambukiza yanazuilika, ni wewe mwenyewe kuamua unataka uwe na kisukari, unataka uwe na magonjwa yasiyoambukiza mengine ni suala la kufanya mazoezi, ni suala la kuamua uishi vipi. Kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wote, tumeshaanza mazoezi karibuni kwenye mazoezi, mazoezi yanafanyika Jamhuri na viwanja vingine, ili tuweze kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, ninaunga mkono hoja, ni hotuba nzuri iliyosheheni matamanio ya Watanzania, ni hotuba nzuri inayokidhi matarajio ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwatekelezea mahitaji yao Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)