Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Pascal Lucas Lutandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PASCAL L. LUTANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami niungane na wachangiaji wengine; niaanze na kumshukuru sana Mungu mwingi wa rehema aliyenijaalia mimi mtoto wa mama ntilie niseme nanyi Watanzania jioni ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema Fungu Takatifu la Biblia; Wagalatia 4:16, Mtume Paulo anasema: “Nimekuwa adui yenu kwa sababu ya kuwaambia ukweli?” Hili ninaanza na swali. Kwa nini nimeanza na swali? Ninataka niseme, hakuna nchi nzuri kama Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi; hakuna nchi ambayo ni nzuri inawaandaa viongozi katika Taifa hili kuwa viongozi wa kuwatumikia watu, ni Tanzania peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Mheshimiwa Rais, Mama huyu Dkt. Samia nianze kwa kumshukuru sana. Ninataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, watakubaliana nami, kwenye tikisiko hili la mafuta; mimi ni mfanyabiashara, mimi ni mchimbaji; kwa siku ninatumia mafuta zaidi ya lita 1,400. Kuna rafiki zangu nje ya nchi wananiuliza wewe mitambo yako inaendelea na kazi? Ninawaambia mama mafuta yapo ya kutosha, kazi zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanapanga foleni hawaoni mafuta. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa suala la mafuta, nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimshukuru sana Makamu wa Rais ambaye muda wote ameendelea kumshauri Rais kufanya mambo yawe mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kabla ya mchango wangu, ninamshukuru sana Mkuu wa Mkoa wangu kaka yangu Mheshimiwa Martin Shigela. Kwa kweli Rais alituletea mtu sahihi. Sisi Geita tunajivunia tuna Mkuu wa Mkoa tofauti na wengine, msimwombe Wabunge kuja kwenye mikoa yenu. Mama atuachie Geita bado tuna kazi naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mkuu wa Wilaya yangu Bura; kwa kweli muda wote amekuwa akinisaidia kazi zangu za kibunge, nikiwa sipo jimboni. Ninamshukuru sana kaka yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana vilevile Mkurugenzi wangu wa Wilaya ya Chato. Aaah! huyu bwana hapana, apewe maua yake. Sasa, ninawashukuru sana wananchi wema wa Chato Kusini. Watu wema, watu waungwana, watu hawa rahim sana, walikubali mimi niwe sauti yao humu ndani ya Bunge, walikubali mimi niwe mwakilishi wao. Ninajua wananisikia. Ndugu yangu Toyi mahali alipo, ndugu yangu Masamaki; hawa ni wapambanaji. Wamenishika mkono; ninaendelea kuwapongeza. Nitakuwa nao na nitawatumikia katika siku zote za utumishi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kwa sababu ya muda ninaomba nianze kwa kuchangia sehemu kubwa tatu. Nianze na mifugo kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wafugaji inaonekana leo kwenye hili Taifa sisi si watu wa kuzungumziwa mazuri. Shida ni nini? Wachangiaji wote wanalalamika tunavamia mashamba. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na naomba niulize, hawa wataalam wanaowasaidia Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wana mpango gani na sisi wafugaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mpaka leo hawawezi kututafutia maeneo ambayo sisi wafugaji tutachunga bila kugombana na wakulima? Kweli inaingia akilini miaka 60 ya Uhuru? Mfano mdogo tu, Mheshimiwa Rais Samia, alipoingia madarakani aliwaambia watu wa madini, Waziri wa Madini yupo hapa, dhahabu haziwezi zikaliwa na simba; waachieni Watanzania wachimbe, leo tumeongeza uchumi wa Taifa mpaka 10% kwa sababu tumeruhusiwa kuchimba kwenye hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niwaulize watu wa Wizara ya Mifugo, wameshindwa kutengeneza mpango kwenye hili Taifa, wameshindwa kuja na wazo la kumshawishi, hata kulishawishi Bunge tukazibadilisha hizi sheria kwenye hizi TFS (haya mapori tu ambayo hata fisi hayana), wakatumegea sisi wafugaji vipande vipande, wakatupa masharti tusikate miti, tusiue swala, wameshindwa kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu sisi Watanzania nani ameturoga? Hawa wataalam wanawaza sisi wafugaji tupunguze mifugo; tukipunguza mifugo baadaye itazaliwa nini na wanajua sisi wasukuma hawa ng’ombe ndiyo tunatolea mahari na mwanamke anapokuwa mweupe ndiyo tunaongeza kutoa mahari ya ng’ombe nyingi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli hawaoni sababu ya kutuongezea kipato cha ng’ombe? Sasa leo tumalize ng’ombe zetu zote, watoto wetu wataolewa na nini? Ninataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, mtakubaliana na nimefanya utafiti, ndoa nyingi zinazovunjika ni wale waliopeana zawadi na mahari za fedha za ng’ombe hazivunjiki. (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waje na mpango wataalam wasaidieni Waziri na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ni watu wazuri, waje na mpango wa kutusaidia sisi wafugaji tusigombane na wakulima. Tupo tayari kuchangia pato la Taifa, hizi hela wanazolalamika, vyumba vya madarasa, wafugaji tuna ng’ombe unauza ng’ombe 10 unailipa Serikali, unakatiwa kitalu chako unachunga, unalinda mtu asikate mti, unalinda mtu asiue swala na lenyewe limekuwa shida mpaka profesa tu ndiyo wanamkubali? Aaah!

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nichangie hotuba ya ndugu yangu Waziri Mkuu, nilikuwa sijaanza ndiyo naanza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimshukuru sana Waziri Mkuu, anafanya kazi nzuri, nimeona akizunguka kila mkoa. Hii kazi anayofanya ni kazi iliyotukuka. Ninataka nimwambie kwa namna anavyokwenda ndiyo namna tunayotaka Watanzania. Watanzania story na maneno tulishapigwa mno, nimwombe Waziri Mkuu, aendelee na style hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi, sisi Wasukuma tuna kilimo tunalima na ngoma moja inaitwa bugobogobo. Ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu, hawa wasaidizi wake wasimfanye kuwa yeye ni ngoma ya bugobogobo. Ngoma hii unaweza ukapiga ngoma mwenyewe, ukacheza mwenyewe, ukalima mwenyewe, hapana! Awachezeshe kwata, akigeuka nao pia wageuke. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudie, wanaweza wakamfanya yeye kuwa na ngoma ya bugobogobo, anapotoka kwenye mkoa wanalala wote, akienda huku tena wanaamka. Awachezeshe zile kwato za kwenye harusi, hawa wasaidizi kuanzia mikoani na humu ndani, mpaka kule kwenye vijiji na kata, haiwezekani kesi ya mpaka nayo hadi aje Waziri Mkuu, kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu wanampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye ni mzuri, nadhani anafananishwa na Sokoine, hawa watoto wa Gen Z wanamjua Sokoine? Aanze naye wamjue kwanza yeye, akiwachezesha ile ngoma ya kwato ninayoionaga kwenye harusi, akigeuka huku wanageuka nao, ukigeuka huku, halafu wewe utaangalia nani anakosea style, hiyo ndiyo kazi tuliyomwamini sisi Wabunge humu, tukampigia kura zote za ndiyo, tunataka afanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikwambie ukweli, unajua ukweli hata Mtume Paulo aliusema kwa Wagalatia kwamba, mnaniona adui kwa kusema ukweli, hawa watu ukisema ukweli unaweza ukazoa uadui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimwambie Mungu wa Mbinguni atasimama na yeye na Mungu hatampunguzia na bahati nzuri ninataka nimwambie mimi ni mtoto wa mamantilie, nilikuwa ninaanza kuwaza kwa nini Waziri Mkuu anafanikiwa, kumbe pembeni yake kuna mamantilie, kwa kweli mamantilie wa Mwigulu naye apigiwe makofi jamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio haya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. PASCAL L. LUTANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, aaah! Namalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho; wananchi wangu wa Chato Kusini, Waziri Aweso, alituahidi maji kutoka Buzilayombo kuja Chato Kusini, hatujayaona na muda mwingi amekuwa akisema, wali wa kujaa unaonekana kwenye sahani. Rafiki yangu Mheshimiwa Aweso, wananchi wangu wa Chato Kusini, hata sahani hawajaiona, tunataka maji, tofauti na hapo maneno yake ya wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani, Chato Kusini hatuelewi, tunataka maji, tunataka maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa Mbunge wa kulialia, ninataka nione matokeo, wananchi waliniamini, nitawapelekea maendeleo, ndiyo mzee wa mitambo ya greda, mimi kwangu hakuna kulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)