Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninampongeza Mheshimiwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya. Mheshimiwa Waziri Mkuu, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masuala matatu au manne hivi. Kama muda utanijalia kufanikisha kumaliza, la kwanza ninaishukuru Serikali kwa kukamilisha Uwanja wa Ndege ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini na Mkoa wetu wa Rukwa. Uwanja ule umekamilika na muda wowote sasa ndege zitaanza kutua na hatimaye Rukwa yetu itakuwa imefunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongea humu ndani kuhusu barabara. Kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama hapa ameongelea barabara, siyo barabara za TARURA wala za TANROADS. Hii mifuko miwili tulitenga plan humu ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Road Fund ambayo ni mfuko wa barabara, tumetenga fedha ziwe zinakwenda kule. Fedha zile zinapatikana na tozo za mafuta ili ziweze kila mwaka kuweza kuboresha barabara zetu ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ninaposimama hapa, 80% ya barabara tulizozitangaza na tukapata wakandarasi mpaka leo zimesimama. Kuanzia Rukwa, Mpanda na maeneo yote yale ndani ya Tanzania hii 80% ya barabara zimesimama. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kila mkandarasi aliyeshinda tenda alipewa site, akapewa advance payment. Baada ya hapo, hakuna mkandarasi hata mmoja aliyepokea fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini hasara zake? Mkandarasi anapokuwa ameshinda na amekwenda site, amepewa advance payment na hatuna fedha za kumlipa, yule mkandarasi ataendelea kutu-charge siku hadi siku mpaka pale atakapokuwa amemaliza kujenga barabara. Sasa natoa mfano, mkandarasi ameshinda labda tenda moja au Barabara ya kutoka Muzi – Ntendo kwa shilingi bilioni 52, lakini mpaka leo hii Barabara ya Ntendo – Muzi ina miaka minne haijawekwa hata kilometa moja ya lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo mpaka barabara ikamilike ndani ya miaka mitano mingine ijayo au miaka minne tutakuwa tumelipia barabara ile kwa shilingi bilioni 100, zaidi mpaka shilingi bilioni 110. Sasa tuna barabara ngapi kiasi hicho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali, bajeti hii ya mwaka huu tusiwe na mradi wowote mpya, twende tukakamilishe miradi ya zamani kwa wananchi wetu hawa kwa sababu, tumewaahidi kujenga barabara, angalau hata tungejenga kilometa kumi kumi, wangeona kuliko sasa hivi, mkandarasi yuko site, na hakuna hata kilometa moja ya lami iliyoweza kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata hasara kubwa, lakini hili nataka kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu, najua ni mzalendo, tunapoteza fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, TARURA. Wote humu ndani wanaipongeza TARURA, nami ninaipongeza TARURA, lakini fedha hawana. Barabara za mwaka 2025, tenda za mwaka 2025, tumeziahirisha. Nataka tena kumwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali inapokuja, basi tukubaliane zile barabara ambazo tulizipitisha mwaka 2025 twendenazo mwaka huu ziweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza ni mwaka 2025 huo huo tumetenga fedha tukasema sasa tuongeze kodi kwenye mafuta, zile fedha zikipatikana ziende TARURA. Tukajenga kuna kitu kinaitwa ringfence, mimi hiyo ninaamini, sasa hivi siyo ringfence, ni open fence.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambazo tunazitenga ziende kwa ajili ya barabara, haziendi, sasa tunakaa humu Bungeni tunatafuta source ya fedha, tunakubaliana kwamba, fedha hizi sasa ziende TARURA ili kujenga barabara zetu. Fedha zile haziendi, zinakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo yanasikitisha sana. Bajeti ya mwaka 2025, nikiwemo humu ndani, tumepitisha kwamba, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa itajengwa, tumepitisha shilingi 2.5 billion hapa, mpaka ninaposimama hapa leo hata senti tano moja haijaenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waheshimiwa Wabunge wanielewe kidogo. Kuna habari Wizara ya Afya inataka kukopa fedha, shilingi 1.4 trillion, kwa ajili ya ukarabati Muhimbili. Nawaambia Waheshimiwa Wabunge, hili jambo tusilikubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama lipo kwenye Wizara ya Afya huko, limeshakuja kwenye Kamati, kuna lobbying zinafanyika. Naomba Bunge hili nendeni mkafanye research, tusikubali kwenda kujenga Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kwa shilingi bilioni 1,400, haiwezekani. Nami niko hapa...

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa. Mheshimiwa Dkt. Samizi.




TAARIFA

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa mchango wake mzuri sana. Naomba kumpa taarifa tu, ili kwa uelewa wa jambo linaloendelea, kwa ajili ya Muhimbili siyo ukarabati, ni ujenzi wa Muhimbili mpya. Ni kweli kabisa ujenzi huo utatumia shilingi trilioni 1.2 na ni mkopo, lakini lengo ni kutaka Muhimbili iwe Hospitali bora kwa sababu, imeshindwa kupata ithibati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo ya Muhimbili ukiyaona yamesambaa sana, yametumia eneo kubwa. Mpango huo ni mahsusi kwa ajili ya kujenga Muhimbili mpya, Muhimbili ambayo itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 1,300. Ni ujenzi wa hospitali pamoja na usimikaji wa mitambo yote ya Muhimbili; na itajengwa kwa awamu ya miaka saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kuweka vizuri tu, siyo ukarabati wa Muhimbili, lakini ni ujenzi wa Muhimbili mpya. Naomba kuwasilisha. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Aeshi unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Waheshimiwa Wabunge sidhani kama wataipokea, hainiingii akilini. Tuiache, tuna mzigo mkubwa bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mingi imesimama, tuna mikopo mingi, tunalipa madeni mengi, kwa nini tukaongeze mzigo zaidi na Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili bado ipo? Twendeni jamani na kimoja kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende tukamalize SGR yetu, twende tukamalize barabara zetu, twende tukakarabati meli zetu. Kule Kigoma, leo ni bajeti ya mwaka wa tano tunasema tunajenga meli, meli haijajengwa mpaka leo. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, inawezekana ni mkopo, lakini nendeni kwenye mikoa mingine, hospitali za rufaa za mikoa hazijajengwa. Kwa nini twende tukabomoe kitu ambacho sasa hivi kinafanya kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, una gari bado zima, acha kwanza liendelee, endelea kufufua mengine. Hizi hela ni nyingi, tunaenda kukopa na tutalipa na mwisho wa siku tutaendelea kuwa na madeni. Ninaishauri Serikali kwa nia njema, tuachane na hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama fedha hizo tumeenda kuzikopa tayari, basi ziende zikajenge hospitali za rufaa kila mkoa, ili kupunguza mzigo wa wagonjwa kwenda Muhimbili, yako maboma kule. Mimi nataka kushauri sana, ninaamini Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mzalendo, liangalieni jambo hilo. Najua litakuja Bungeni, tutapigwa siasa, tutaweza kulipitisha. Ninaomba sana liangalieni mara mbili mara tatu. Yaani kwa sasa hatuna uwezo huo wa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kwa bilioni zote hizo. Twendeni kidogo kidogo tutafika, lakini tukienda haraka hatutaweza kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ndani ya Bunge, na ninaamini katika hili ipo siku mtanikumbuka, nilisimama hapa nikashauri hili. Tusiweke mzigo mzito kwa wananchi tukashindwa kuendelea. Mheshimiwa Waziri Mkuu, twende tukasimamie na kukarabati miradi mingine ambayo haijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mradi wa Meli, Lake Tanganyika. Nimesimama hapa mwaka wa saba, hapa Liemba imekufa, Mwongozo imekufa, tukaambiwa inajengwa meli mpya hapo, hiyo meli ni hadithi, mpaka leo hatuna meli hata moja. Matokeo yake Waheshimiwa Mawaziri wa Uchukuzi wanatuchukua sisi Wabunge kwenda kushangaa meli za Mchina ambazo ziko kule Lake Tanganyika! Siyo meli zetu zile. Meli zetu lini zitajengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia Waheshimiwa Wabunge wa kutoka Mkoa wa Rukwa, Kigoma na Katavi, wananchi wanakufa sana, wanazama sana na hawana usafiri. Tukasema, basi twendeni tukakarabati angalau meli moja, wakanijibu hapa tukarabati Mv. Sangara; Mv. Sangara inabeba mafuta, haibebi watu. Kwa hiyo, kule usafiri wa Lake Tanganyika wanasafiria maboti ya mbao, kila siku wanazama, wanapotea. Nakuomba sana, Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi anapokuja hapa na bajeti yake, aje kutuhakikishia lini meli inajengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia. Kuna karakana ya meli kule Kigoma, wameingia mkataba na mkandarasi miaka minne iliyopita, wamempa asilimia tano sijui, asilimia kumi ya ule mradi, kama advance payment.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo hawajatoa zile fedha, mradi umesimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani kidogo namalizia. Kwa uelewa kidogo wa Waheshimiwa Wabunge...

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii advance payment inayotolewa kwenye miradi ni hela za watu. Ikishatolewa advance payment mradi hauendelei, umekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini nitakuja tena baadaye. Namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli, akipata nafasi tuongee, tujadili kwa ajili ya maslahi ya nchi yetu. Ahsante. (Makofi)