Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Henry Charles Kabeho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. HENRY C. KABEHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha sisi Wabunge wote kupata nafasi hizi na kuingia leo hapa Bungeni tukiwa na afya njema kabisa. Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninamshukuru sana Mwenyekiti wa Chama changu Cha Mapinduzi, daktari bingwa wa changamoto na matatizo ya Watanzania, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kamati kuu yake kwa kuniteua kugombea nafasi hii katika jimbo langu baada ya kuongoza kura za maoni. Ahsanteni sana Kamati Kuu na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri za ulinzi, usalama na maendeleo ya nchi hii, kwani muda wote halali, anafikiria usalama na maendeleo ya nchi yake. Ninamwombea maisha marefu yeye na familia yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwa kutumikia vyema nafasi yake ya Umakamu wa Rais kumsaidia Mheshimiwa Rais, ninampongeza sana. Pia, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwani Uchumi wa Buluu tunauona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki nisipomshukuru au kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kazi nzuri za usimamizi wa Serikali. Kazi zake tunaziona, akipambana na wezi na wazembe, akizunguka mikoani bila kuchoka kumsaidia Mheshimiwa Rais. Pongezi nyingi sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau watu muhimu kabisa, wananchi wangu wa Jimbo la Igunga, bila wao pia nisingekuwepo hapa, walinipa ushindi mnono wa 91%, ahsanteni sana. Nitawatumikia bila kuchoka ndani ya miaka mitano Mwenyezi Mungu akipenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, imeonesha kujitegemea kwa fedha nyingi za shilingi trilioni 26. Pesa hizi ni nyingi, lakini sisi Waheshimiwa Wabunge tunaomba zioneshe reflection kwenye barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ndiyo tatizo kwenye majimbo yetu, kila Mbunge analia na barabara. Fedha hizi baadhi ziwekwe TARURA. Kwa hii bajeti ya TARURA ipelekwe kwa wakati na zipelekwe za kutosha kuweza kusaidia barabara majimboni kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba, jimboni kwangu kuna barabara ya kutoka Igunga – Mwalala – Lugubu – Itumba, tunaomba tupate fedha ikarabatiwe. Barabara za Mjini Igunga, tuliahidi kwenye Ilani, nazo zitengenezwe. Pia, kuna Daraja la Isugilo kwenye Kata ya Igunga. Watu wa Isugilo wametenganishwa kwa daraja hili. Limeharibika siku nyingi, wanafika kwa tabu kwenye Kata yao ya Igunga ili wasione wametengwa. Ninaomba tulitengeneze hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya maji, kuna Tanki la Bulenya. Tanki limejengwa, lakini wakati fulani kazi ilisimama muda mrefu. Baadaye nikaongea na Waziri wa Maji, Mheshimiwa Aweso, mtu mstaarabu na msikivu sana, ameanza kupeleka fedha na tumepata mabomba, na yameanza kufungwa kwenye Kata ya Mwamakona kuelekea Kata za Kiningi’inila na Isakamaliwa. Pia, tunaomba safari hii, fedha zifike na miradi isisimame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Madiwani wana mishahara midogo, lakini ninajua uwezo wa nchi na tuna miradi mingi na hali siyo nzuri sana na wafadhili hawatupatii fedha za kutosha. Kwa hiyo, ninaomba au ninashauri halmashauri na Serikali zichangie. Serikali itoe na halmashauri, Wakurugenzi wajibane kidogo, wawape Madiwani fedha kidogo, ni watu muhimu sana kwenye maendeleo ya majimbo yetu na kata zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamkumbusha Mheshimiwa Waziri Shemdoe, tuliongea pembeni kuhusu ambulance. Alisema siku nyingi ambulance itakuja, haijaja. Sasa, leo ninamkumbusha mtani wangu, ni mtu mwema, rafiki yangu sana, ninaweka kwenye Hansard ili tupate ambulance moja hapo Igunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Igogo – Igurubi kuna mradi wa maji umesimama. Ninaomba nao uletewe fedha tuweze kwenda vizuri. Pia, tunaishukuru Serikali kwa kutuletea umeme vitongoji 69. Nguzo zimemwagwa kama mchanga, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia, Mwenyezi Mungu amsaidie kuishi maisha mazuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani yake ya mwaka 2025/2030...

MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. HENRY C. KABEHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliahidi na ametekeleza. Pia, kuna barabara ya kwenda Igurubi kutoka Igunga, Mheshimiwa Rais ameleta fedha kiasi, imeanza kutengenezwa, panapitika vizuri, tunamshukuru sana. (Makofi)

MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. HENRY C. KABEHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata dawa na vifaatiba kwenye zahanati zetu, tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia. (Makofi)

MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. HENRY C. KABEHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wangu, Mheshimiwa Paul Chacha. Ninamshukuru Mheshimiwa Said Mkumba, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa kusimamia Serikali vizuri katika mkoa wangu...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Henry.

MHE. HENRY C. KABEHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninawashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote walionichagua. Kamati za siasa zote na mabalozi kwa kazi nzuri ya kunichagua na nitawatumikia kwa nguvu zangu zote. (Makofi)
MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Henry, kuna taarifa.

TAARIFA

MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpa taarifa mzungumzaji wetu mzuri kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inaendelea kuzingatia utekelezaji na kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi yote ya maendeleo nchini. Jimbo lake ni moja kati ya maeneo ambayo tunaamini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninampa hiyo taarifa ili aendelee kuchangia vizuri. (Makofi)

MHE. HENRY C. KABEHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaipokea taarifa yake nzuri na wananchi wa Igunga wanasikia...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Henry, kwa mujibu wa Kanuni, Mbunge akikupa taarifa inabidi Kiti kikutaje kwanza kama unapokea au unakataa taarifa hiyo ndiyo uendelee kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Henry, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. HENRY C. KABEHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaipokea. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya, malizia mchango wako.

MHE. HENRY C. KABEHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaishukuru familia yangu, maana yake nimeisahau kabisa. Walikuwa hawalali, tunapambana pamoja kupata nafasi hii, na mwaka 2020 niliongoza kura ikawa bahati mbaya sikuteuliwa. Kipindi hiki nimeteuliwa, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia na kamati kuu yake na familia yangu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ninaunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)