Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami ya kuchangia hotuba, mpango, na bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu sana kunifikisha siku ya leo na hata kunipa ujasiri na kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia mchango kwenye mpango huu na bajeti hii mahususi ambayo ni kama jumuishi tu ya wizara nyingi ambazo zinafanya chini ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kabisa ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa sana ambayo Rais amefanya. Kwa kweli tunasema kutoka kwenye dhati ya mioyo yetu ya kwamba amefanya kazi iliyotukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka kabisa alipoanza tu Urais, alihutubia wanawake wa Tanzania nzima kupitia wanawake wa Dodoma, akasema; “Jukumu hili ambalo nimepewa, tumepewa sisi wanawake wote. Hivyo basi twendeni tukafanye kazi kwa bidii, tuthibitishe uwezo wetu kwamba wanawake tunaweza.” Kweli kabisa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kabisa na chenji imebaki. Shukrani nyingi nampa na kumpongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine za pili, basi ziende kwa Waziri Mkuu. Waziri wetu Mkuu toka alipoteuliwa amefanya kazi nzuri na hasa hapa juzi juzi ambavyo amepita kwenye ziara zake za kila halmashauri akisikiliza kero, na kubaini kero kwenye halmashauri mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona watu wengi, makundi ya watu yakijitokeza wenye matatizo, kweli ametoa msimamo sasa kwa watendaji wote wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa haki. Yeye kama Msimamizi Mkuu wa Serikali, ametoa dira kwa wafanyakazi wengine wa Serikali kuendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani nyingine nazipeleka kwa Mawaziri wote na Naibu Mawaziri, wamefanya kazi kubwa kwa siku hizi 100 za utendaji wa Rais kwa awamu hii ya pili ambayo amefanya. Tumewaona, mimi Kamati yangu ya Utawala, Katiba na Sheria, tumezunguka na Mheshimiwa Ridhiwani kwenye ziara tulikuwa pamoja kila mahali. Kongole nyingi sana kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalize shukrani kwa Mwenyekiti wangu wa UWT wa Taifa, Mheshimiwa Mama Mary Pius Chatanda, ni Mbunge mwenzetu, lakini kwa kweli imetufurahisha sana Mbunge huyu kuwa miongoni mwetu sisi wanawake. Tumejisikia faraja kuwa na mwenyekiti wetu mahali hapa. Hivyo, inaonekana tuna nafasi kubwa wanawake kufanya maendeleo kwa niaba ya wanawake wenzetu Tanzania nzima kwa kuwa na mwenyekiti wetu hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, ninaomba sasa nitoe hoja zangu kupitia hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tumefurahishwa sana, kama nilivyosema, na utendaji kwa miaka hii minne ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, madarasa mengi yamejengwa, na shule zimejengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka takwimu zimetolewa hapa karibu madarasa 78,000 yamejengwa, lakini shule nyingi sana. Watoto wetu walisoma kwenye shule mbovu sana, lakini sasa tuna shule za kisasa mpaka vijijini. Hii ni fahari kubwa sana kwa nchi yetu ya Tanzania hasa kwenye sekta ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo na kwenye sekta ya afya, Rais amefanya na Serikali imefanya vizuri sana. Zahanati mpaka vijijini kabisa, lakini vituo vya afya, siyo hivyo tu, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa, hospitali za rufaa, vifaa kwenye mahospitali yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi kwa Serikali yangu kwa kazi kubwa sana ambayo imefanyika. Mpango huu ambao umewakilishwa mahali hapa, tunaenda kufikia level nyingine Watanzania wenzangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo kwenye uchumi wa kati, sasa tunaenda kwenye uchumi wa kati lakini wa juu. Kwa maana tunaenda kupanda kwa kutoa mipango mikubwa ambayo imepangwa kama itatekelezwa na kufuata kama tulivyopanga. Niseme tu kwamba, tunaweza kwenda kwa pamoja hivyo, sambamba na maendeleo yote pamoja na miundombinu, pamoja na huduma za kijamii ikiwemo hizo huduma za elimu, huduma za afya na miundombinu ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaenda vizuri zaidi tukienda na huu uchumi shirikishi ambao tunashirikisha wanaume na wanawake kwenye maendeleo twende pamoja. Siyo hivyo tu, lakini tunaposema kwamba uchumi jumuishi, ni sekta zote zishirikiane kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama ni maji, wawe na kipande cha maendeleo; kama ni elimu, wawe na kipande cha maendeleo; kama ni afya, wawe na kipande cha maendeleo; kama ni kilimo ambacho ndiyo tunategemea Tanzania nzima, uchumi wetu utakuzwa na kilimo kwa 85%. Hata hivyo, sekta binafsi hatuwezi kuisahau ambako tunategemea katika Dira yetu ya 2025 mpaka 2050, private sector wana-contribute 75%. Huo ndio utakuwa uchumi shirikishi maana tunaenda wote kwa pamoja bila kuachana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema hivyo, ninamlenga mwanamke. Sasa mwanamke lazima ashirikishwe kuanzia ngazi ya kupanga, kwenye utekelezaji, na pia ashirikishwe kwenye tathmini. Tukimwacha nyuma mwanamke, maendeleo hayataenda. Kwa hiyo, twende pamoja na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, contribution ya mwanamke katika maendeleo haya ni 80%, na ukimwendeleza mwanamke, moja kwa moja umeendeleza familia na moja kwa moja umeendeleza jamii. Hivyo basi, mipango yetu na bajeti yetu imhusishe mwanamke moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite katika kile kipengele cha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Kuna mipango mingi imepangwa na ikiwemo hizi 10% za halmashauri. Ndugu zangu ni kitu ambacho kimekuwa faraja sana kwa wanawake, kama ukisikia michango mingi ya Wabunge, kila mtu amegusia kuhusu 10%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu hiki ni mtaji, wanawake wanahitaji mitaji kwa ajili ya biashara zao, kwa ajili ya miradi. Hivyo basi, Serikali i-pay attention na kitu hiki, na kukiangalia, na kukifuatilia kwa karibu sana ili kuona kama kweli kuna ugawaji sawa wa hizi 10%, na kuna ufuatiliaji wa karibu ili wale watendaji wanaokiuka kitu hiki, basi waweze kuchukuliwa hatua ili hao wanawake wapokee hiyo faraja yao ya 10%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna hizo shilingi bilioni 200 ambazo zimetengwa kwa ajili ya wajasiriamali ambazo zimewekwa benki. Hata hii pia ni faraja kubwa sana kwa wanawake. Uwekwe utaratibu mzuri wa kuhakikisha walengwa wanafikiwa na hii hela ili wanawake waweze kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu ukweli, mchango mkubwa ambao sisi wanawake tunataka katika Serikali yetu, la kwanza kabisa, wanawake wanahitaji hiyo mitaji. Hili ni hitaji la kwanza la wanawake. Pili, wanawake wanahitaji masoko. Wauze wapi biashara zao? Wanawake wafundishwe tu, wanaweza. Ukimfundisha mwanamke jinsi masoko yanavyopatikana au namna hata ya kusafirisha bidhaa nchi za nje, wanawake wanaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kuwe na link ya utengenezaji wa bidhaa na usafirishaji wa bidhaa, au kuwe na link ya utengenezaji bidhaa na masoko ili wanawake wakitengeneza bidhaa zao ziwe na ubora, lakini pia zipate masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ambalo wanawake wanahitaji, ni elimu. Elimu inayotakiwa ni elimu ya fedha, elimu ya ujasiriamali. Pia wanawake wapewe skills ndogo ndogo tu, jinsi ya kuwa na wazo la biashara na namna ya ku-develop wazo la biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wafundishwe hata skills ndogo za kuandika business plan. Mwanamke ajifunze vitu hivyo ili ajue ya kwamba mradi wake ambao anaenda kuufanya utakuwa na faida au hauna faida? Hapo ndipo mwanamke apewe mkopo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. Ninaomba nimalizie kwa kusema kwamba wanawake watapata faraja kubwa sana wakipata hii mikopo na kama shida ni dhamana, ufunguliwe mfuko wa dhamana ambao utawasaidia wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)