Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Kwanza kabisa, ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuwepo mahali hapa leo tukiwa na majukumu makubwa katika nchi, ili kuweza kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nichukue fursa hii kwa moyo wa dhati kumpongeza Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa katika Taifa letu na namna ambavyo ameendelea kufanya kazi kwa kugusa maeneo mbalimbali ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, pamoja na yote haya tumeona kuwa amekuwa ni Rais wa kwanza kuhakikisha kabisa Taifa linakuwa na mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa mwaka 2050. Hili ni jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza watendaji wake wote ambao ni wasaidizi kuanzia Makamu wake wa Rais, Mheshimiwa Nchimbi, pia Mheshimiwa Waziri Mkuu na watendaji wote katika Wizara zote, bila kusahau watendaji katika nafasi mbalimbali za mikoa, wilaya hadi huku chini, na sisi Waheshimiwa Wabunge kwa namna moja au nyingine tumekuwa tukimsaidia Rais kuhakikisha kwamba maono haya yanafikiwa kama ambavyo amepanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipitia kwa kina hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, imesheheni data katika kila eneo. Hiki ndicho kinachotakiwa kufanyika tunapokuwa tukitoa taarifa mbalimbali. Kwa maana hiyo, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameonyesha hili na amegusa maeneo yote. Sekta mbalimbali zimeonekana na namna ambavyo output zinaonekana kwa kila eneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu yeye ndiye anaye-facilitate haya yote kuhakikisha yanafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nitakuwa na mambo machache ya kuongea. Nitaongea kwenye sekta ya elimu, eneo ambalo pia nimekuwa ni Mbunge mwakilishi wa kundi la vyuo na vyuo vikuu, kwa namna ambavyo nchi imekuwa na mwelekeo katika kuboresha sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni msingi wa dira ya mwaka 2050. Sambamba na malengo mengine ya muda mfupi, na hata ya muda wa kati, kwa nini tuboreshe elimu? Ni katika elimu hii ndipo tunapata nguvu kazi yenye ujuzi. Ni katika elimu ndipo tunapata wahitimu mahiri ambao wanaenda kukabiliana na changamoto za karne za 21. Ni katika elimu, endapo itaboreka ndipo tutapunguza suala la umasikini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja hayo, ninapongeza juhudi kubwa ambazo zimefanyika na Serikali. Tumeona mageuzi makubwa katika elimu ya msingi, elimu ya sekondari na elimu ya juu, kwa maana ya vyuo na vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mikopo imeongezeka, miundombinu imeboreshwa, na mambo kama hayo, yamesaidia vijana wetu kusoma katika mazingira ambayo ni rafiki kwa ajili ya masomo yao. Uwekezaji huu ni muhimu ili kujenga Taifa lenye watu wenye ujuzi, lenye watu wenye maarifa na uwezo wa kujitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo nchi Barani Afrika ambazo zimewekeza katika elimu na wamefika mbali. Kuna nchi ya Rwanda wamewekeza katika elimu ya msingi, na pia katika elimu ya TEHAMA. Hivi sasa tunavyoongea Rwanda inaongoza katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunayo nchi ya Botswana, wao wametenga fedha inayopatikana kutoka katika sekta ya madini na kuiwekeza kwenye elimu. Mambo kama hayo yanaleta tija kwa sababu elimu inapoboreka ndipo ambapo tunapata wanafunzi au wahitimu mahiri ambao watakuwa na faida katika Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada zote hizi, kuna changamoto moja ambayo binafsi kama mtaalamu na mtafiti nimeendelea kuiona. Changamoto hii ni kuhusu ubora wa elimu sambamba na ujuzi wa wahitimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona namna ambavyo Wabunge wamekuwa wakichangia na kuona kabisa kwamba kuna changamoto ya ajira, kuna changamoto ya vijana wengi kuwa katika mitaa, na kadhalika na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zinaonyesha kuna changamoto ya ubora wa elimu na ujuzi wa wahitimu. Eneo hili ni muhimu sasa Serikali iliangalie. Mheshimiwa Rais amefanya mageuzi makubwa sana kwenye miundombinu na kwenye mambo kama hayo, lakini bado eneo la ubora wa elimu ni changamoto katika nchini yetu, sambamba na ujuzi wa wahitimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yangu iliangalie eneo hili, na lipo katika maeneo mawili. Tunaposema ubora wa elimu, kuna wanafunzi au wahitimu, lakini pia kuna waalimu au wahazili. Kila mwaka takribani wahitimu 50,000 hadi 70,000 wanahitimu kutoka katika vyuo vikuu. Hapo bado hatujaweka watu au wahitimu wanaotoka kwenye Vyuo vya VETA na kwenye vyuo vya kati. Sasa hawa wote wanatengeneza zaidi ya 50% ya wahitimu wetu kukosa ajira, iwe ni za kujiajiri au zile ajira ambazo ziko katika mfumo rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize, ni kwa nini vijana wengi wanakosa ajira? Kwa nini vijana wengi wako mtaani? Sasa basi, ni muhimu Serikali kutafuta ufumbuzi katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali tuangalie pia wahadhiri au waalimu ambao wamekuwa wanafundisha, hasa katika eneo la vyuo vikuu. Kumekuwa na changamoto. Juzi tulikuwa na ziara katika baadhi ya vyuo vyetu nchini, tumekuta mtu ambaye amepata demotion kwenye taasisi fulani anapelekwa kwenda kufundisha. Hii haikubaliki kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kabisa taasisi hizi zina vigezo vya namna ambavyo zinapaswa kupata wahadhiri au waalimu. Mtu ambaye amepata demotion, anaendaje kufundisha mwanafunzi? Hii haikubaliki kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuangalie ujuzi wa vitendo au ubunifu wa hawa vijana wetu, namna ambavyo wako katika eneo hilo vizuri. Pia uwiano wa ujuzi na uhitaji wa soko la ajira ukoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba Wizara zinazohusika ziliangalie suala hili. Pamoja na uwekezaji mkubwa katika eneo hili, kuna haja ya kuangalia ubora wa elimu, ili tuweze kupata products ambazo zitakuwa ni nzuri za kuweza kuajirika na pia kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nisemee upande wa wahadhiri. Mheshimiwa Waziri wa Elimu yuko hapa ananisikia. Kuna changamoto moja ambayo wahadhiri wamekuwa wanakutana nayo. Tuna vyuo vikuu ambavyo viko chini ya TCU, pia kuna taasisi nyingine ambazo ziko chini ya NACTVET.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa TCU retirement age ni miaka 65, lakini upande wa NACTVET retirement age ni miaka 60. Sasa nimekuwa nikifanya ziara mbalimbali kuonana na wadau hawa. Wengi wanaomba retirement age iwe sawa, TCU pamoja na NACTVECT, kwa maana ya miaka 65 kwa wote wanaofundisha katika hizi taasi zetu. Hiyo itasaidia kuendelea ku-maintain wahadhiri ambao wana uzoefu ili waweze pia kuendelea kutoa huduma hiyo kwa wanafunzi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine amblo ninataka niliongelee, ni kuhusiana na vyuo vyetu vya kati. Mheshimiwa Rais amewekeza sana, hadi sasa tuna vyuo vya VETA takribani nchi nzima, lakini vyuo hivi bado havina programs ambazo zinahusu eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano, kule ninakotokea mimi, Wilaya ya Ukerewe tuna Chuo cha VETA. Katika chuo hiki 99% ya watu wa Ukerewe tuna-depend kwenye uvuvi, lakini cha kushangaza Chuo hiki cha VETA hakina program yoyote ambayo inahusiana na masuala ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukilipigia kelele jambo hili. Vyuo hivi mahali vilipo viendelee kutoa programs ambazo zitawanufaisha wale walengwa au wanaokaa maeneo husika. Nina imani kabisa kuwa ushauri huu utafanyiwa kazi ili tuweze kuwa na wanufaika wanaotoka katika maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo moja ambalo nitaomba niligusie kidogo kuhusu ajira kwa vijana. Tumeona kabisa kila Mbunge anapiga kelele kuhusu ajira, lakini uwekezaji mkubwa umefanyika. Ninaomba coordination ya miradi mbalimbali ya vijana ambayo Mheshimiwa Rais ametenga iweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, na ufuatiliaji. Tumeona mambo ya ufuatiliaji yakiwa raised na watu, na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali hapa. Kwa hiyo, ninaomba Bunge lako Tukufu liweze kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa vijana na kuondoa changamoto kubwa ya vijana ambayo inaonekana kuwa tatizo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)