Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EXAUD S. KIGAHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema aliyetujalia uzima kukutana hapa leo tukiwa na afya njema. Pili, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, lakini zaidi, pamoja na Makamu wa Rais, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, zaidi Waziri Mkuu wetu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ambaye leo na mimi napata nafasi kuchangia katika hotuba yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia katika nchi hii kwa kuweka miradi mingi ya kimkakati, tukianza na SGR ambayo kwa kweli sote ni mashahidi, inasaidia kukuza uchumi na hasa katika sekta ya usafirishaji hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, pia katika sekta ya usafirishaji viwanja vya ndege lakini na ndege zenyewe pamoja na sekta ya usafirishaji katika bahari kwa maana ya maji, bandari lakini zaidi kwenye barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia kwa kuhakikisha miradi mingi ya kimkakati inaendeshwa vema bila kusahau sekta ya nishati, mradi mkubwa ule wa Mwalimu Nyerere ambao sasa umekuwa mkombozi kwetu sote katika masuala ya umeme, nadhani sasa sote tunaona umuhimu na umahiri wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia hii iliyojengwa katika nchi hii pia Jimboni kwangu imefanyika. Nichukue nafasi hii pia sasa kuwashukuru sana wananchi wenzangu wa Jimbo la Mufindi Kaskazini ambao walinichagua kwa heshima kubwa kuwa kiongozi wao. Kule tumeweka historia kwa mara ya kwanza katika Jimbo la Mufindi Kaskazini kuanza kuwa na barabara za lami tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Sasa haya yote ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo katika barabara tu, pia katika sekta ya maji, elimu, afya. Zaidi ya vituo vitano vya afya vipya vimejengwa ndani ya miaka minne ya uongozi wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hili ni jambo kubwa ambalo wananchi wa Mufindi tunamshukuru sana, katika mawasiliano pia kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hizi ni shukrani, lakini pamoja na hayo, nikiwa nachangia hotuba hii ya Waziri Mkuu, kuna mambo ambayo bado tunamwomba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake, kuna mambo machache tunamwomba katika maeneo mahsusi. Moja, kama ambavyo wachangiaji wengi wamesema ni kwenye barabara za vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Wizara zake zote. Vijijini huko tuna changamoto kubwa. Sisi Jimbo la Mufindi Kaskazini ni wakulima. Tulianza kuhamasishwa kulima pareto miaka hiyo, na ndiyo maana unakuta kuna viwanda vingi na kiwanda cha pareto kiko Mufindi, kiko Mafinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wale kwa sababu ya changamoto kubwa na hasa kwenye miundombinu ya usafirishaji, sasa pareto imekufa na kiwanda kile kinahangaika kutafuta malighafi. Tukahamasisha zao lingine la chai. Chai nayo sasa inasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya changamoto ni ya barabara, na mambo mengine. Sasa hivi tumehamasisha kulima maparachichi. Ninaamini, kama miundombinu hii ya usafirishaji, hasa barabara itakuwa ni changamoto, ninaamini nayo yataanza kudoda kama ambavyo yamedoda mazao mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira kuu ya Wana-Mufindi Kaskazini ni kilimo. Sasa ninaomba, moja, tuone namna gani ya kuweka bajeti mahususi kwa TARURA kama ambavyo tulivyoweka kwenye REA, kwenye umeme. Umeme sasa umesambaa kwenye vijiji vyote, tunaenda kwenye vitongoji na mitaa. Tuone ni namna gani ya kuanza na mfuko maalum wa kuchangia kuhakikisha kuwa TARURA wanapata fedha za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi vijijini zipo chini ya TARURA; na mimi kwangu kule barabara nyingi ni hivyo. Wananchi wangu kule wamejiajiri. Sisi changamoto ya ajira tulishaanza kuitatua miaka ya zamani, tangu miaka ya 1970 wakati tunalima pareto na miaka ya 1980. Kwa hiyo, tunachotaka kuwezeshwa ni miundombinu wezeshi, na hasa barabara, ili tuweze kushafirisha mazao yale kupeleka katika viwanda na masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu hiyo, moja, tutafute namna kuwawezesha TARURA kupata fedha za kutosha ili tuhame kutoka kuwa na barabara za udongo tuseme kiwango cha chini kabisa cha barabara katika nchi yetu iwe angalau ya Changarawe. Hii itatusaidia kukuza uchumi katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, sisi kule ni wakulima wa misitu. Sasa baraka hizi za misitu zinaenda na changamoto pia. Barabara nyingi katika jimbo langu zinaharibika kwa sababu ya kusafirisha malighafi kubwa ya magogo, mbao, na bidhaa nyingine zinazotokana na misitu. Sasa wenzangu wa TFS ndio wanufaika wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili watafute namna ya kuwafanya TFS nao kuanza kurejesha kama shukrani kwa wanachi ambao tulitoa maeneo yale bure kwa ajili ya kupanda miti. 60% ya misitu inayolisha viwanda vyote katika Wilaya ya Mufindi inatoka Jimbo la Mufindi Kaskazini. Tuone namna gani TFS nao wanaweza kuchangia, kutengeneza, na kukarabati, kama Mheshimiwa mmoja alivyosema hapa kuhusu barabara zetu, ili wasafirishe malighafi hizo ambazo wanauzia wateja ikiwemo kiwanda kile cha Mufindi Paper Mills (MPM).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara hizi za lami tumeweka viwango kwamba isizidi tani kadhaa. Sisi barabra zetu kule hata tani 10 haziwezi kubeba, lakini yale magari yanabeba zaidi ya tani 40. Utaona ni namna gani Jimbo la Mufindi Kaskazini barabara zake zinachakaa kwa sababu ya kusafirisha mzigo mzito uliozidi uwezo wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan ametujengea barabara ya lami kilomita 14 Mtili – Ifwagi – Mkuta ambayo ninaamini itasaidia sana kusafirisha malighafi hizi kwa sababu imejengwa kwa viwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo inachangia sana maendeleo ya nchi hii ni nishati ya umeme. Sisi kule katika Jimbo langu la Mufindi Kaskazini ambalo lina kata 11, kati ya kata hizo 11 kata sita zinahudumiwa na Mwenga Hydropower. Hawa ni sekta binafsi waonazalisha umeme na kuusambaza katika Jimbo la Mufindi Kaskazini kwenye zaidi ya vijiji 35. Ninavyoongea hii leo wananchi wenzangu wale kuna wakati mwingine wanapata umeme siyo zaidi ya masaa sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenga Hydropower tuliwashukuru sana walipoanza. Ni sehemu ya Kampuni ya Rift Valley, walikuwa wanazalisha ule umeme kwa ajili ya kulisha kiwanda cha chai Itona, pale Stone Valley. Kwa sababu umeme ulikuwa mwingi, tunashukuru walisaidia baadhi ya vijiji, lakini sasa wamepata changamoto, wakapata mkataba wa kulisha vijiji hivyo kata sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wizara ya Nishati, EWURA tutafute namna ya kuwapunguzia mzigo Mwenga Hydropower. Wanazalisha takribani Megawatt nne. Wakati wanahudumia vijiji vichache waliendelea kuwauzia TANESCO, sasa wamezidiwa hawawezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, EWURA na Nishati wawape mkataba wa kuwauzia TANESCO moja kwa moja, halafu vile vilivyobakia vihudumiwe na TANESCO badala ya Mwenga Hydropower ambao wameshindwa. Mimi hata kwangu ukiomba hata mita unaweza kuchukua mwaka mzima usipate Mwenga Hydropower.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumbani kwangu sina umeme, nimewaomba kuingiza umeme Kijijini kwangu Nundwe hadi leo bado wanasuasua, wanasema subiri Mheshimiwa. Sasa kama kwangu mimi wanasema hivyo, je, wananchi wengine watapata huduma wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wizara ya Nishati wawasaidie Mwenga Hydropower. Kama nilivyosema, sisi Jimbo la Mufindi Kaskazini suala la ajira kwa vijana, vijana wetu wanajiajiri sana kwenye shughuli za kilimo na kwenye misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyonayo, moja, barabara; pili, umeme ambao unasaidia kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi; na tatu, mikopo hii ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema, tuwasaidie vijana ili waweze kujiajiri, tupunguze changamoto ya kuomba ajira. Kila siku wanalia ajira, na mwingine akasema hadi waseme connection kwa ajili ya kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuhakikisha ninachangia kwenye hotuba hii. Ili tusiwakatishe tamaa wananchi wa Mufindi Kaskazini, moja, tuendelee kuboresha miundombinu ya barabara. Kama nilivyosema, tuwaongezee bajeti TARURA, lakini pili, Mwenga Hydropower wasaidiwe mkataba ule wao wawauzie umeme TANESCO badala ya wao kusambaza vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, nakushukuru sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)