Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hii hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi ya Urais siyo kazi ndogo ni kazi kubwa sana. Kwanza kabisa Rais analinda amani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote Rais yeyote anayekuwepo madarakani kazi yake kubwa ni kulinda amani ya nchi yake. Rais amelifanya hivyo, anaendelea kulifanya, tunamwombea aendelee kulinda amani ya nchi yetu, nasi tuendelee kupata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri Mkuu, ana kazi kubwa sana, kila kipindi cha uchaguzi kunakuwa na hofu, mtu anapokuwa anafanya kazi wanasema huyu anaomba Urais. Sasa anayo kazi kubwa sana, sijui ni wapi ambapo watasema hataomba Urais, kwa sababu yeye ni Waziri Mkuu, anakaa na Baraza la Mawaziri, ana vikao, anakaa na Party Caucus vikao, ukienda mikoani yeye ni Kiongozi wa Chama, atakutana na wanachama. Sasa sijui ni wapi watasema? Kwa hiyo, anafanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishaambiwa siku moja hapa kwamba hotuba hii ni Waziri Mkuu. Kwa hiyo, Wabunge wanapokuwa wanaongea, awe anatusikiliza basi. Sasa tukiongea na Waziri Mkuu halafu hatumwoni, nayo inakuwa kazi ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumwomba Waziri Mkuu afanye kazi bila kuangalia kwamba anasema wapi? Atende yale ambayo Katiba inasema, atende yale ambayo kiongozi wake mkuu wa juu anamwelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Mawaziri wote waandamizi wa Wizara hizi, Mheshimiwa Prof. Shemdoe, Mheshimiwa Sangu na Mheshimiwa Profesa Kabudi. Mheshimiwa Prof. Mdoe ni mtu na nusu, yaani huyu ni mtu na nusu, sijawahi kuona Profesa ambaye hata leo ukisema bwana mimi nakuteua kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri, anarudi tena kwa sababu aliwahi kuwa Mkurugenzi huko. Anafanya kazi vizuri na watendaji wake wote, Manaibu wazuri, Makatibu wazuri na Watendaji wote wa Wizara, tunawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti nianze na maombi ya Jimbo la Bunda. Naomba sana Profesa na wote wanaohusika Shule ya Msingi Nyamswa A, Ikizu B, Tingirima, Mariwanda, Ikomarilo A na B hizi shule zimetitia kutokana na maji na hali ya wanafunzi wanakaa chini, wengine hali ni mbaya madarasa mengine zaidi ya matano manne tumeyabomoa. Tunaomba mfanye kazi nzuri ya kwenda kutusaidia kwenye hizo shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo shule mbili za sekondari. Shule ya Sekondari ya Tingirima, ni shule mpya, haina maabara, walijenga majengo yakabaki wazi maabara zote tatu. Tunaomba waende wakajenge yale maabara, wamalizie. Pia Shule ya Sanzati ni mpya, lakini haina jengo la utawala, ina hali mbaya sana. Walishasema wanaenda kuiona, waende wakaiangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Unyali pamejengwa majengo, lakini hakina theater. Jengo la upasuaji halipo, wakamalizie kituo kipya cha Mihingo, wametupatia shilingi milioni 250, watu wamemaliza fedha, naomba warudishiwe, ili wakipata hela waweze kumaliza kama ahadi ya Serikali ilivyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia hali ya maliasili na utalii kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, kwenye Bunge lililopita, Bunge la Kumi na Mbili tulisema kwamba maliasili na utalii, watu wa TANAPA, taasisi ya TANAPA, TAWA na TFS tuwape fedha zao. Taasisi zile ni kubwa, zinalinda maliasili ya nchi yetu, tukakubaliana warudishe 50%. Sasa hivi wanawapa 51% na wanapata 49%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo fedha bado ziko Serikalini, wanaenda tena wanakusanya, wanawaletea ndiyo mnawarudishia. Tunaomba kwa kuanzia, waacheni wao wakusanye halafu ninyi ndio mchukue. Mtavunja, mtaua hizi taasisi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema leo tuna watalii wameongezeka kutoka milioni moja mpaka milioni mbili, wanaongezeka, tuna bilioni tano zimeongezeka mpaka shilingi 5,000,900,000/=. Sasa kama hatuwezi kukusanya hizo fedha zilinde hiyo maliasili, tutaporomoka kwa vyovyote vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA na TAWA ndiyo wanalinda wanyamapori, na sisi kwenye vijiji vyangu zaidi ya 11 toka miaka 20 hawalimi mazao yao yote, yanaliwa. Naomba tafadhali sana Mheshimiwa Waziri Mkuu hili jambo mlichukue, tulizungumze, tuwekeeni fensi, kwa sababu Botswana, South Africa, Kenya wameweka fensi. Tupeni fensi ili wakulima wa maeneo ya Maliwanda, Kunyari, Kihumbu, Kyandege na Tingilima wapate kupata mazao yao ya kilimo wanacholima, tafadhali sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mifuko ya kijamii. Mifuko ya kijamii, tunayo NSSF, PSSSF, WCF na hata OSHA, tuipeni nguvu hii mifuko kwa sababu sasa hivi ina shilingi trilioni zaidi ya 24. Tuipeni nguvu hii mfuko ili iweze kuongeza ajira kwa wananchi. Kwa hiyo, tunaomba tuipe nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mafuta, bei ya mafuta nchini tusifanye mzaha, hapa Wabunge wameongea mambo mengi sana. Naomba cha kwanza, punguzeni zile tozo ambazo siyo za lazima, punguzeni zile tozo. Jambo la pili tuna ule mfumo wa bulk wa kuagiza mafuta kwa pamoja, turuhusu sasa watu binafsi nao waagize mafuta tuweke mara mbili kama walivyofanya wenzetu Wakenya. Ni lazima tufanye kila namna ili tuweze kuweka mafuta ya bei iwe nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama ni kupunguza mapato, tuna maeneo mengi ya Wizara mbalimbali ambayo yana bajeti ya vinywaji. Tupunguze huko kwenye bajeti ya vinywaji tupate nafuu ya wananchi kwenye mafuta, tutaumiza wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali, tafadhali, Waziri Mkuu afanye kila namna kwa sababu sasa hivi tunatumia bulk, tumeshaagiza yale mafuta, yatakuja kwenye mwezi mzima kwa sababu hatuna mfumo wa watu, private sector, maana yake tutaenda mpaka mwezi mzima, itatuumiza. Ni lazima tufike wakati tufanye nafuu, tuagize mafuta kwa watu binafsi au tupunguze bei wenyewe ili mafuta yawe nafuu kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna misemo mingine ya Serikali inaumiza. Kuna maelekezo ya Serikali yanayotamkwa kila siku, lakini yanaumiza. Leo tunaambiwa Rais ameanzisha Wizara ya Vijana na ametoa shilingi bilioni 200 kwa vijana, lakini ukija kwenye lugha nyingine unakuta hii fedha shilingi bilioni 200 mara imeenda kilimo, mara sijui imeenda wapi? Imeenda sijui Wizara ya Ustawi wa Jamii! Tunaomba tafadhali, hii shilingi bilioni 200 ni ya vijana. Hii Wizara imeanzishwa na vijana waliipokea vizuri mno, kwa shilingi bilioni 200 ibaki kwenye mawazo ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunao msemo tunasema elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, lakini leo ukienda kwenye sekondari mtoto anayeingia sekondari na anayeingia darasa la kwanza, michango 240 kidogo. Shilingi 200,000, shilingi 300,000, shilingi 400,000 mpaka shilingi 600,000, lakini sekondari hizo zinapokea ruzuku ya karo shilingi bilioni 20. Kwa mfano, kuna watoto 500 unazidisha mara 20,000 unapata hela zake, lakini kuna grant zinatolewa. Hela hizo zinaenda wapi? Ream kila siku, jembe, koleo, tuangalie hii mifumo ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi tunapeleka shilingi bilioni zaidi ya 24 kwa mwaka, lakini ukienda pale mtoto anachanga kila kitu mpaka muhuri wa kupigia shati anatoa anapigiwa muhuri. Tunatoa wapi vitu? Tuangalie mifumo yetu hii kama inafanya kazi vizuri, kama haifanyi kazi vizuri tuangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za afya, leo ukienda zahanati, zahanati tunajua pale kuna Nesi, maeneo mengine hakuna Mganga, lakini kwenda pale kutibiwa lazima utoe shilingi 5,000. Hivi mwananchi wa kawaida ataitoa wapi?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, anaitoa wapi shilingi 5,000 ya kuchanga? Ukienda Benjamin kutoka Jumatatu mpaka Ijumaa ni shilingi 25,000 lakini ukienda Jumamosi, Jumapili ni shilingi 70,000. Wananchi wataumia. Kwa hiyo, tuangalie mifumo yetu ili tuweze kujenga nchi yetu vizuri. Ahsante. (Makofi)