Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nakushukuru sana kwa kuniona na kuniita niweze kutoa mchango wangu katika hii Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya hatimaye leo tumeweza kukusanyika mahali hapa. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo kwa kweli, ameendelea kutupigania na kututumikia Watanzania. Tunamshukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa ni mbeba maono ya Watanzania. Leo hii tunaona anatuchukua Watanzania kutoka kwenye uchumi wa chini anatupeleka kwenda kwenye uchumi wa kati wa daraja la juu. Tunamshukuru sana kwa jitihada hizi anazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, jambo hili siyo jepesi, ni jambo kubwa linalohitaji ujasiri na umakini wa hali ya juu, ambao Mheshimiwa Rais wetu amejaliwa na Mwenyezi Mungu. Katika hilo, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mheshimiwa Rais wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawatia shime Watanzania, Waheshimiwa Wabunge pamoja na wafanyakazi wote, sasa tusimame na Mheshimiwa Rais kuona kwamba, maono aliyonayo yanatekelezeka na yanafika kwenye nchi ambayo tunaikusudia, ambayo ndiyo nchi ya asali na maziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba wafanyakazi tusimame vizuri, tufanye kazi zetu vizuri, lakini wakulima, wafanyabiashara pamoja na wanafunzi tunapokuwa vyuoni pamoja na kule shuleni, tuwe na kaulimbiu yetu kwamba sasa tunaenda mwezini na mwezini kwetu ni kwenda kwenye uchumi wa kati wa daraja la juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila tutakalokuwa tunalifanya Watanzania tuseme kwamba Watanzania tuna jambo letu, Watanzania tunaenda mwezini na mwezini ndiyo huko kwenye uchumi wa kati wa daraja la juu. Kwa kweli hilo na mimi nasema kabisa kwa dhati ya moyo wangu, Wabunge wenzangu tusimame na Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri Mkuu, kwa kweli kwa kipindi kifupi toka ameapishwa mpaka hivi sasa hakika Waziri Mkuu amejitambulisha pasipokuwa na mashaka yoyote kwamba hakika yeye ni mtetezi wa wanyonge na wala hiyo haina mashaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu tunamsubiri kule Tabora tunaamini kwamba atafika na tutakuwa na furaha kubwa kweli kweli. Nami ninaamini kwamba mwenye macho na mwenye masikio, basi ameshaona, na ninaamini wafanyakazi wote walio chini yake, ninaamini njia wameshaiona na ninaamini kwamba sasa watafuata nyayo zake na tunaamini mabadiliko makubwa kabisa kabisa yanaenda kutokea katika Taifa letu la Tanzania. Mungu ambariki sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, aendelee kuchapa kazi, nasi tunamuunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mazuri mengi kweli yamefanywa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunawapongeza sana. Ilikuwa ukiongelea umeme, ni vijijini, lakini leo hii ni vitongoji. Ukiongelea maji, miradi mbalimbali inaendelea katika vijiji vyetu. Ukiongelea ujenzi wa shule, ujenzi wa zahanati na mambo kadha wa kadha, yanaendelea katika Taifa letu la Tanzania. Kimsingi tunaendelea kuipongeza Serikali yetu na tunaamini kweli uchumi wa kati unawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mazuri sana ambayo Serikali yetu imekuwa inatufanyia, bado kuna changamoto ambazo zinaendelea kuwakabili Watanzania. Moja ya changamoto hizi ni ufinyu wa maeneo ya shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Taifa letu hili la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukulia mfano katika Mkoa wetu wa Tabora na hususan katika Jimbo letu la Sikonge changamoto hii ni kubwa na imepelekea kuwa na mwingiliano mkubwa sana kati ya wakulima, wafugaji na warinaji wa asali vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, Jimbo letu la Sikonge na Wilaya yetu ya Sikonge ina jumla ya ukubwa wa kilomita za mraba 27,870, lakini kati ya kilomita hizo, ni kilomita 1,533.01 tu ndizo zinazotumika katika shughuli za kimaendeleo, katika shughuli za ufugaji, katika shughuli za kilimo pamoja na urinaji wa asali. Eneo hili ni dogo sana. Eneo lote lililobaki takribani kilomita za mraba 26,300.99 zote hizi zimebaki kama ni mapori ya akiba na mengine ni kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna mashaka wala hatuna shida na Hifadhi ya Taifa, shida yetu ipo katika mapori haya ya akiba. Tunaomba sana Waziri Mkuu hebu hawa wananchi wa Sikonge kutoka kwenye asilimia tano nukta tano wanazozitumia kwa shughuli za kilimo, hebu ziongezeke hizi angalau tufikie hata 20%, tunaomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii yale ambayo ni mapori ya akiba, kimsingi haya mapori tayari kuna wageni, kuna watu kutoka nje ya Mkoa wa Tabora wameshavamia kwa sababu wanajua haya ni mapori yamekaa tu hayafanyi kazi yoyote, yameshavamiwa kwa kiasi kikubwa sana. Hivyo tunaomba tunaomba Serikali tunaiomba hebu ituongezee haya maeneo na yale yatakayobaki kama ni akiba na hifadhi, basi kuwe na management nzuri ya kuona kwamba kama ni akiba basi iendelee kuwa ni akiba na kama ni hifadhi, basi iendelee kuwa na hifadhi na yasivamiwe, tunaomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkutano uliopita wa Bunge hili niliuliza swali la nyongeza kuhusu maeneo haya, jibu ambalo Serikali ilitoa, ilisema kwamba kuna Kamati ya Mawaziri Nane ambayo iliundwa na tathmini yao inasubiriwa ili kusudi hatua stahiki ziweze kuchukuliwa ili wananchi hawa waweze kuongezewa maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiri sasa hivi ni mwaka wa tatu na nimwombe sasa kwa vile Mawaziri hawa wanane wako chini ya Waziri Mkuu, basi hebu aitishe basi hiyo taarifa ili kusudi tathmini iweze kuonekana na ikiwezekana basi, ninaamini itawezekana kwa sababu hata Rais katika taarifa yake ya kuzindua Bunge hili alisema anaenda kuongeza takribani ekari 2,500,000, mimi ninaamini katika nyanja zote hizo Wanasikonge wanaenda kupata maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ukienda katika kijiografia ya Mkoa wetu wa Tabora na hususan katika Wilaya yetu ya Sikonge hatuna maziwa wala mito ya kudumu. Kimsingi ni kwamba hatuna Bahari, hatuna maji, lakini tumejaliwa kuwa na mito midogo midogo ya msimu, ambapo wakati wa mvua kubwa kama mwaka huu inajaza mabwawa ya kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mto wetu Uruwa, tunalo bwawa letu la Urua na lilikuwa limeshaingizwa tayari kwenye skimu ya umwagiliaji, lakini baadaye sintofahamu ikatokea kwamba oh, iko karibu na hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani kilomita zote zile tulizozisema za mraba 26,300.99 zote hizo kukata tu kaeneo kadogo na sisi tukapata skimu ya umwagiliaji haiwezekani! Hapana. Tunamwomba sana Waziri Mkuu ili na sisi tuweze kupatiwa lile eneo tupunguze kidogo tu kule kwenye hifadhi ili na sisi tuwe na umwagiliaji tuweze kulima mpunga, tunaomba sana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha, kengele ya pili imeshalia.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, lakini nimalizie tu mara moja. Bado kuna eneo la ajira vilevile kwa kweli vijana wetu walioko kule vijijini wanalia na wamekata tamaa, anafika kijana anakwambia, Mheshimiwa mimi siajiriki, unamwambia kwa nini huajiriki? Anasema sina connection. Huu msamiati wa connection!
MWENYEKITI: Mheshimiwa tunashukuru kwa mchango wako.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)