Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza naanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ambaye ametupa afya na nafasi ya sisi sote kufika katika jengo hili kuendelea na shughuli zetu kama kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninamshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu, hasa katika hizi siku 100. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. Tatu, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Rais alipomteua hakukosea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ni mchapa kazi, ni mtu ambaye anataka kuona matokeo. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba tumemwona wakati akiwa Waziri wa Fedha, amefanya kazi yake vizuri na hata Mheshimiwa Rais akamwona, akampa cheo au nafasi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nakumbuka Januari tarehe 2, mapema tu baada ya kuteuliwa alifanya ziara katika Jimbo langu la Mpwapwa kuangalia athari za mafuriko ambayo yalitokana na kunyesha kwa mvua nyingi, ambayo iliharibu miundombinu ya reli. Kwa hiyo, ninampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni nzuri. Uzuri wa bajeti hii umefanya wananchi wengi wawe na matumaini makubwa kwamba, mwaka huu shughuli nyingi zinakwenda vizuri sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu kazi iliyobaki ni utekelezaji wa bajeti hii, ikitekelezwa kwa ukamilifu wake, basi wananchi wetu watanufaika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika siku 100 ameanza kutekeleza ahadi zake nyingi ambazo alizitoa wakati anapita kwenye Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Moja ya ahadi ambazo ameshatekeleza sasa, ni uanzishwaji wa Mpango wa Bima ya Afya Wote, mpaka sasa zaidi ya watu 1,400 tayari wameshaingizwa kwenye mpango huu, wale watu ambao wana kipato cha chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ni mzuri sana, utasaidia wananchi wengi na hasa wale ambao hawana uwezo wa kuhudumia matibabu yao. Jambo kubwa ambalo ningependa kushauri ni utekelezaji wa dhana yenyewe. Tuanze na watu wasio na uwezo, isitokee kwamba watu wenye uwezo ndiyo wanaanza kunufaika kabla ya watu wasio na uwezo. Kwa hiyo, Serikali isimamie vizuri, ili watu wasio na uwezo waanze kunufaika na mpango huu wa Bima ya Afya, halafu badaye watafuata watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mambo haya yakitokea huko nyuma, mfano mpango mzuri sana wa TASAF ambao Serikali iliuanzisha, lakini matokeo yake ni hata leo ukienda kwenye maeneo yetu kule kwenye majimbo, utakuta wanaonufaika na TASAF sio wale wenye sifa ya kuingia kwenye huu mpango. Wale ambao wana unafuu wa maisha ndio wameingia, wale ambao ni maskini kabisa wa mwisho wamekosa nafasi. Hii inatokana na nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeleta mpango mzuri, Mheshimiwa Rais alitarajia matarajio mazuri, lakini utekelezaji usiposimamiwa vizuri, basi tunakutana na tatizo hilo. Kwa hiyo, naomba mpango huu wa Bima ya Afya kwa Wote, uanze na kaya ambazo hazina uwezo kabisa wa kuhudumia matibabu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninampongeza Mheshimiwa Rais ni, ndani ya siku 100 ameanzisha mpango wa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kundi la vijana. Kwa hiyo, ninaamini ukitekelezwa vizuri, ukiratibiwa vizuri, mpango huu unaenda kuwakomboa vijana, utaongeza ajira katika sekta mbalimbali, utaongeza ajira kwenye kilimo, kwenye biashara, kwenye viwanda vidogo vidogo na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachotakiwa ni uratibu na hasa kule eneo ambalo fedha hizi zinatolewa, tukisimamia vizuri, tutaondoa upendeleo, ubadhirifu, kutengeneza vikundi hewa au waombaji hewa. Hayo ni mambo ambayo yanaweza kuathiri mpango huu mzuri ambao Mheshimiwa Rais ameukusudia. Kwa hiyo, lazima Serikali isimamie hasa kwenye halmashauri ambako mikopo hii inaenda kutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naongelea kuhusu barabara. Sasa kuna miradi mingi ya barabara, hasa zile ambazo zimetekelezwa, kuwekwa tabaka la lami, zimesimama kwa muda mrefu. Nikirudi Jimboni kwangu Mpwapwa, Mpwapwa ni Wilaya kongwe katika Mkoa wa Dodoma, ni kati ya Wilaya saba za Mkoa wa Dodoma; wilaya zote sita zimeunganishwa kwa barabara za lami isipokuwa Barabara ya Mpwapwa – Dodoma. Tuna kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 32 tu kutoka Kongwa Junction kwenda Mpwapwa Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi yuko site, zaidi ya miaka miwili sasa hajaanza kazi kwa sababu, hajalipwa fedha ya awali. Naiomba sana Serikali iangalie, haiwezekani jiji kama la Dodoma, Makao Makuu ya Serikali, kuna barabara moja katika wilaya moja katika mkoa huu wa Dodoma haijawekwa lami. Wabunge waliotangulia wamepiga kelele sana kuhusu jambo hilo, lakini bado ni kizungumkuti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wasiwasi, Wananchi wa Mpwapwa wana wasiwasi, kwamba inawezekana sasa mkandarasi akachoka akaondoka maana amekaa zaidi ya miaka miwili pale hakuna kitu kinaendelea. Wananchi wana hamu sana ya kutumia ile barabara kwa ajili ya kukuza uchumi wao. Kwa hiyo, naomba sana, Serikali iliangalie jambo hili kwa jicho la karibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kidogo kwenye upande wa kilimo. Kilimo ndiyo sekta ambayo inatoa ajira nyingi kuliko karibu sekta zote. Watu wengi wamejiajiri kwenye kilimo. Naipongeza Serikali kwamba, kwa sababu ya ruzuku ya mbolea tumeweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kama nchi kwa 130%. Pia, matumizi ya mbolea yameongezeka kwa zaidi ya 14%, ni kwa sababu, sasa watu wameona umuhimu wa mbolea, lakini pia, ile ruzuku imefanya watu wengi waweze kupata mbolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali iendelee kuratibu vizuri, kama ilivyokuwa inafanya, ili tuweze kujikwamua. Ule mpango wa mabwawa ya umwagiliaji ambao ulianzishwa katika kipindi cha nyuma, ulikuwa mzuri sana, lakini sasa mabwawa mengi utekelezaji wake hauendi kwa kasi iliyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kule kwenye Jimbo langu la Mpwapwa, tunalo Bwawa la Msagani ambalo linatumia gharama kubwa sana ya shilingi 27.8, lakini mpaka leo ujenzi wake haujafikia hata 60% kwa sababu, unasuasua na ni zaidi ya miaka miwili sasa bwawa hilo limejengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa haya ni muhimu sana, yangeweza kusaidia wananchi wakajikwamua na umaskini kwa kulima kilimo cha umwagiliaji. Idea ilikuwa nzuri sana kwamba, tukiwa na mabwawa maeneo mengi katika nchi yetu, wananchi watalima kilimo cha umwagiliaji, wataachana na kilimo cha kutegemea mvua; kuna mwaka inanyesha, lakini kuna mwaka mwingine hainyeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiwa na mabwawa haya, maana yake ni wananchi wataendelea kulima, mvua ipo au haipo watafanya kilimo wakati wa kiangazi, lakini pia hata wakati wa masika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie kupitia Wizara ya Kilimo mabwawa haya yajengwe haraka sana. Baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)