Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. YAHYA E. NAWANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Katika jambo kubwa Mheshimiwa Rais amelifanya ni kumchagua Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu, na pia kuwa Msimamizi Mkuu wa TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ndiyo roho ya nchi yetu. Tukizungumza kuhusu TAMISEMI karibia 20% ya bajeti yetu inakwenda TAMISEMI. Kwa hiyo, tukiwa na kiongozi shupavu kama Mheshimiwa Dkt. Lameck Nchemba tunaenda kufanya mapinduzi makubwa katika TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeshawahi kufanya kazi na Mheshimiwa Mwigulu. Yeye ni mtu ambaye anapenda matokeo, na pia ni mtu muungwa na hapendi ubadhirifu, na vile vile ni mtu ambaye anapenda wananchi wake. Kwa hiyo, ninaweza kusema Wizara ya TAMISEMI imempata mtu shupavu na kwa hakika ninaona TAMISEMI inaenda kubadilika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba nijikite katika hoja tatu, au nne. Kwanza ni barabara. Wabunge wote wamezungumza kuhusu ubovu wa barabara zetu. Katika Wilaya ya Newala sisi tuna jumla ya network ya barabara kilometa 966, na hizi zote zinahudumiwa chini ya TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizi barabara zetu tunategemea kupata fedha nyingi kutoka Road Board au Road Fund. Katika fedha za Road Fund Wabunge wote wamezungumza, kila Mbunge hapa anazungumza kuhusu kuongeza fedha, lakini pia barabara zetu nyingi zimeharibika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Jimbo langu la Newala Vijijini, Barabara kutoka Mkoma Moja hadi Mnyame haipitiki kabisa. Pia, Barabara kutoka Chiwonga – Pacha Nne mpaka Nambali – Mkongi haipitiki. Pia, ukiangalia Barabara ya Maputi – Chilangala mpaka Ndanda pia haipitiki. Pia, hata barabara kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sababu mimi ni Mbunge mkazi wa Iramba, barabara ya kutoka Mtoa – Mtekente – Ndago nayo ina changamoto pia kwa sababu ya mvua kubwa ambayo imetokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeiomba Wizara na Mheshimiwa Waziri Mkuu, akija basi tuletee majawabu ya barabara zetu namna gani tunaenda kuziimarisha ili ziweze kupitika mwaka mzima na kurudisha taswira ya barabara hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaomba nijikite katika kilimo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya hasa katika kukuza zao la korosho. Wakati anaingia, korosho tulikuwa tunapata tani 100,000 sasa hivi tunakwenda mpaka tani 600,000. Haya ni mapinduzi makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu kwa mwaka huu 2026/2027 pembejeo ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia anakuja kutuletea ni zaidi ya shilingi bilioni 27 ambazo zinaenda kuhudumia hekta zaidi ya 200,000. Kwenye zao la korosho ningeweza kushauri yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije na mpango mzuri wa kuhakikisha tunaongeza ruzuku ya pembejeo ili kila mwananchi ambaye anaweza kulima aweze kuongeza tija. Pia, Serikali imekuwa inatoa pembejeo ya sulphur, na dawa za maji. Ningependa kuishauri Serikali, sasa iongeze viuatilifu au dawa za kuuia magugu (weeder). Hii itasaidia sana kuongeza uzalishaji na hata yale mashamba ya zamani tunaweza kuyaongezea tija na kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inaweza kuongeza fedha za kigeni, lakini pia kwa wananchi wataongeza uzalishaji, na fedha za export levy zitaongezeka kwa sababu mashamba mengi ya wananchi yatakuwa yamelimwa kwa wakati, pia tutaongeza uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ningependa kujikita katika suala la maji. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, wilaya yetu na katika mradi kwa bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu page number 69 amezungumza, katika miradi ambayo inaenda kunufaika na fedha nyingi ni Mradi wa Makonde, ambao unatoka katika Jimbo la Newala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameleta jumla ya fedha za mradi ule shilingi bilioni 84. Ningependa kumwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, ule Mradi mpaka sasa hivi Mkandarasi amepewa fedha shilingi bilioni 18 pekee yake na asilimia imefika 46%. Ule Mradi ulikuwa unatakiwa ukamilike tarehe 30 Machi, lakini mpaka leo mradi ule bado unasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, ule Mradi wa Maji wa Makonde unaenda kuhudumia Wilaya ya Newala, Wilaya ya Tandahimba, na Wilaya ya Mtwara, majimbo zaidi ya saba. Asilimia zaidi ya 45 ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanaenda kunufaika na ule mradi wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa mradi ule unaenda kusaidia sana wananchi wa wilaya hizi nilizozitaja hasa Majimbo ya Newala Mjini, Newala Vijijini, Tandahimba, Lulindi, Nanyamba, na Mtwara Vijijini. Hawa wote wanategemea huo mradi mzuri wa Makonde. Kwa hiyo, ningependa kuishauri Serikali tumalize huu mradi kwa wakati ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nichukue nafasi hii kumshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Aweso. Huu mradi ulikuwa ni jitihada zake, alienda kumwomba Mheshimiwa Rais na akatukabidhi huo mradi. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ambariki sana na sisi tunamwombea heri na mwisho wa siku huu mradi ukikamilika, mambo yanaenda kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vituo vya afya, Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga vituo vya afya vingi sana, lakini katika Jimbo la Newala Vijijini tuna vituo vitatu vimekamilika. Pia, tunaiomba Serikali, kukamilika tu kwa jengo, tungependa kuweka vifaa pia katika vituo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya Mkwedu, Nandwahi, na Kituo cha Malatu, hivi vituo vimekamilika. Kwa hiyo, tungependa sana hivi vituo pia vipate ambulance, na pia vifaa ambavyo vingeweza kusaidia kufanya kazi kwa ufanisi. Pia, Vituo vya Mtunguru, Mdimba Mpelepele, pamoja na Mikumbi, hivi vipo katika pipeline; na katika bajeti ningeomba Serikali pia iweze kusaidia na kukamilisha vituo hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ningeweza kuleta mawazo kidogo katika migogoro ya wananchi. Serikali inafanya vizuri sana katika kuhakikisha migogoro hii inakwisha. Tunaisadia Serikali yetu kuhakikisha tunajikita zaidi katika kupunguza kero za wananchi. Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, na Wakuu wa Wilaya wanafanya kazi nzuri sana, lakini pia mimi ningeweza kushauri kuwe na institutional framework, ili kama mgogoro katika ngazi ya wilaya unahusu afya au ardhi, basi Afisa Ardhi, Mwanasheria wa Halmashauri, au Kilimo na hao watu watatue huo mgogoro. Kuwe na institution framework. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka nilivyokuwa DC Iramba nilikwenda Shelui kutatua mgogoro ambao tayari Mzee Chiligati miaka 35 nyuma alishautatua. Kwa hiyo, bila institution framework tutakuwa hatufanyi ile kazi ya kuwasaidia wananchi ambayo kwa hakika tumeona kazi kubwa ambayo Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu anaifanya, na mwisho tutaendelea kuwalaumu tu Wakuu wa Mikoa na tutaendelea kuwalaumu Wakuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwajengea nguvu kubwa tutengeneze institution framework ambayo itawasaidia wao pia katika kuhakikisha hizi kazi zinafanyika, na migogoro inaratibiwa na hata akija kiongozi mwingine mgeni, basi anajua kama katika kijiji fulani mgogoro umetatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)