Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kabla ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uhai ambao yeye aliweza kutufanya kuwepo katika Bunge letu Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu, katika maono yake na kutufanya sisi kuweza kuonekana katika himaya ya Kimataifa kama Tanzania, nchi iliyo juu sana katika hali ya maendeleo inayopiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninampongeza kwa namna yake, Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa anayoifanya kwa upande wa Zanzibar, kwa vile ndiko ninapoishi. Ninampongeza kwa sababu naye ni mmoja wa wasaidizi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kufanya kazi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nimpongeze sana, tena sana ndugu yangu na rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuelekeza na kutekeleza zile ahadi za Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusimamia vyema kazi zake na kuwasimamia Mawaziri kwa kutekeleza yale yote yaliyoagizwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninawapongeza Mawaziri ambao anafanya nao kazi katika Wizara hii ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Kipekee ninampongeza Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Watendaji wake kwa ubunifu, na kuweza kulibadilisha Bunge letu hili Tukufu ambalo kila mmoja kwa sasa hivi anaona kuna mabadiliko yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ukiingia Bungeni sasa hivi kuna mambo unayaona kwa macho tu. Bunge lililopita nilikuwa sijaona bendera zilizojipanga, lakini sasa hivi Bunge letu linang’ara kwa Bendera za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Bendera za Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, humu ndani katika kumbi zetu zote mbili, kila mmoja anaona namna zilivyo. Kwa hiyo, naye nimpongeze pamoja na watendaji wake akiwemo pamoja na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije upande wa hoja. Hoja yangu kubwa niielekeze upande wa kujikumbusha. Tujikumbushe katika lile Bunge la Kumi na Tatu ambalo lilikuja kuhutubiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa kama Mhimili wa Dola ambao ulikuja katika hili Bunge letu na kuja kuleta maelekezo, kutoa ahadi za kwanza na kutoa picha ya namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano itakavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba tu kwamba niliangalie jarida hili, kulisoma kidogo wakati ule ambapo alikuja. Jarida letu hili ninadhani kila Mbunge analo na kila Mbunge amelisoma. Mimi ninadhani uniruhusu nisome mambo machache ambayo yameandikwa katika hili jarida letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kilichonivuta katika hili jarida letu, kwanza katika ukurasa wa tano kuelekea miaka 2030 tutafanya mageuzi ya Mashirika ya Umma ili kuboresha ufanisi, uwazi na tija. Tunataka kuongeza siyo tu gawio ambalo Serikali inapokea, lakini pia kufikia lengo la Mashirika na Taasisi za Umma kuchangia angalau 10% ya mapato yote yasiyo ya kodi. Hilo sisi tutasema kwamba ni agizo la Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nije katika yale mambo ambayo aliyatolea ahadi katika kipindi cha siku 100 za uongozi wake. Pale kuna vitu ambavyo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema, suala la kwanza linahusu utumishi na utawala bora ambalo ni suala la uundaji wa Serikali. Serikali imeshaundwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika muktadha huo huo, alikuja na hoja ambayo mimi nitasema kwamba ni ya lazima viongozi ambao atawachagua pamoja na sisi wasimamizi kuna vitu ambavyo ni lazima tuvifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake tukizungumzia ni ‘lazima’ katika muktadha wa kisheria tunasema kwamba ni ‘shall.’ Kwa mfano, alisema ni lazima viongozi wa Serikali kwa ngazi zote kuanzia Mawaziri hadi Maafisa Tarafa wawe karibu na wananchi ili kuweza kufahamu changamoto zao na kuwajibika kwao. Hilo ni suala ambalo ni lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumaini kwamba sasa hivi Waziri Mkuu kwa zile ziara ambazo anazifanya moja anakwenda kusisitiza hili agizo ambalo alilisema Mheshimiwa Rais na kuliweka katika hotuba yake, kwamba hili suala ni lazima tukizungumzia kwamba viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za Mawaziri pamoja na Maafisa Tawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kinachotusikitisha ni kwamba katika ile ziara ya Waziri Mkuu kuna mambo ambayo wakati mwingine katika ile ziara yake katika ule utatuzi wa zile changamoto, maana yake kuna matatizo madogo sana ya kutatuliwa na Afisa Tarafa, lakini utakuta changamoto zile anapewa Waziri Mkuu aweze kuzitatua. Hii inaonekana wazi kwamba huko chini bado hakujawa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niishauri Serikali, maana yake kwa mujibu wa hili agizo na huu ulazimisho wa Mheshimiwa Rais ni lazima tuhakikishe kwamba kuna vitu ambavyo tunavitengeneza. Katika kuvitengeneza kwetu, iwe ni muundo maalumu. Ninaomba katika utengenezaji wetu huu tuandae kitu ambacho kinaitwa sustainable management ambapo kila kitu ambacho kimezungumzwa na Mheshimiwa Rais maana yake kiwe ni sustainable na lazima kiwe na usimamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wake maana yake tuwe na kitu tunachokiita conducting careful monitoring. Ipo Idara ambayo imeundwa chini ya Waziri Mkuu ambayo inafanya kazi ya monitoring katika vyombo vyetu na taasisi zetu. Tunachotakiwa ni kuziangalia hizo ziwe ni zina-conduct careful monitoring maana yake kuwe na ule ufuatiliaji wa kina ambako kila mmoja awe anafuatilia majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kisha katika hotuba hiyo hiyo ya Bunge la Kumi na Tatu maana yake kuna kitu ambacho ni cha lazima, ambacho wanasema, ni lazima tudhibiti wachache wanaotaka kuturudisha nyuma kwa kuendekeza maslahi binafsi. Hilo ni suala ambalo ni kitu cha ulazimisho. Kama katika muktadha wa kisheria nayo ni ‘shall.’

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninadhani katika utendaji wa hizi kazi zetu, ningeshauri kwamba Serikali pamoja na sisi Wabunge tuwe karibu sana kuziangalia zile hotuba na zile hoja zinazotolewa na Mheshimiwa Rais ili kuweza kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna anavyofanya kazi zake pamoja na watendaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninaunga mkono hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa asilimia mia moja, ahsante. (Makofi)