Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uhai na leo kuweza kutoa mchango wangu hapa Bungeni. Nikishukuru chama changu cha Mapinduzi, ninamshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake, Mawaziri wote na Manaibu Waziri kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimehudumu kwenye halmashauri zaidi ya miaka 15, na huu mwaka wa kumi sasa nipo hapa Bungeni. Katika miaka mitano ambayo Serikali imefanya mambo makubwa ya maendeleo ni miaka hii ya Rais wetu Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha nyingi za maendeleo zimekuja majimboni mwetu, na kwa wale wanaofahamu historia, Jimbo la Mbagala, Mbunge alikuwa harudi mara mbili. Safari hii nimerudi kwa sababu ya miradi mikubwa iliyofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. "Man lam yashkurin-nas, lam yashkurillah." Asiyemshukuru binadamu mwenziye hata Mwenyezi Mungu hatomshukuru. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la fedha, kwa kweli Serikali imepeleka fedha za kutekeleza miradi ya afya, miradi ya elimu na miradi ya barabara. Miradi ya afya na elimu, majengo yaliyojengwa yanaonekana. Sitaki kuyataja kwa sababu ya muda, lakini sasa hivi kwenye jimbo langu, kuna majengo ya ghorofa ya elimu na afya, tunaendelea kushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio kingi cha Wabunge hapa, pamoja na wananchi wetu tunaowaongoza ni miundombinu ya barabara. Ukipiga hesabu, fedha zilizokwenda kwenye barabara na fedha zilizokwenda kwenye afya na elimu, ukipiga hesabu vizuri, utakuta fedha zilizokwenda kwenye barabara ni nyingi kuliko kwenye afya na elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ukija kwenye matokeo ya fedha za elimu na barabara yanaonekana kwa macho. Elimu na afya yanaonekana kwa macho, lakini matokeo ya fedha zilizoenda kwenye barabara hazionekani. Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndiyo swali la kujiuliza hapo, tatizo ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya utafiti kidogo, miaka mitano iliyopita, Halmashauri ya Manisapaa ya Temeke, imepata shilingi bilioni 50 kwa ajili ya barabara. Kwa hesabu za kawaida, shilingi bilioni 50 ni kilometa za lami 50. Ukiacha miradi hii ambayo imekuja kwa ajili ya idadi maalumu ya DMDP, nenda katafute kilometa 50 za lami katika Halmashauri ya Temeke. Hii ni kwa Mkoa mzima wa Dar es Salaam, na ikiwezekana kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapato ya ndani, ndani ya miaka mitano, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imepeleka shilingi bilioni 20 kwa ajili ya barabara. Nenda katafute kilometa 20 za lami zilizojengwa kwa mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejifunza, fedha hizi tunazipeleka na tukishakuzipeleka, tunazisambaza katika kila eneo kwa uchache sana, kitu ambacho hakikidhi mahitaji ya ujenzi wa barabara wa maeneo hayo. Jana Mheshimiwa Naibu Waziri, alinijibu katika swali langu, alisema pale Kilungule, Mtaa wa Kwa Mwarabu, kilometa 0.88 wametenga fedha shilingi milioni 165.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mita 880 kwa shilingi milioni 165 unaenda kujenga changarawe. Ukiweka changarawe bila mifereji, mwaka unaofuata lazima changarawe ile itaondoka. Ukija mwaka mwingine kuitafuta shilingi milioni 165 huwezi kuiona kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazo baadhi ya barabara ambazo nimepiga hesabu yake, kwa mfano, barabara inayokwenda kule Saku Mwisho ni kilometa 3.6 ndani ya miaka mitano, imepelekewa changarawe na kushindiliwa zaidi ya shilingi bilioni 2.6, lakini sasa hivi barabara haipitiki. Barabara hiyo ingejengwa kwa kiwango cha lami au zege, tungetumia shilingi bilioni tatu, na tusingekuwa tena na uendelezaji wa barabara ile kwa sababu ilikuwa imekamilika kwa miundombinu yote ya mifereji pamoja na lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, ukiangalia kwa Halmashauri za Dar es Salaam na Halmashauri za Majiji trend ya makusanyo inaongezeka kila mwaka. Kama ndani ya miaka mitano, tumeweza kupata fedha za barabara shilingi bilioni 50, kilometa tano, kwa nini Serikali yetu isiangalie utaratibu wa kutengeneza kilometa 100 za lami, kwa kutafuta wakandarasi sasa na kuwapa kazi, lakini tukawalipa ndani ya miaka sita au saba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, barabara zitakuwa haziharibiki kwa sababu zitajengwa kwa ubora. Hata hivyo, uwezo wa halmashauri wa kulipa wenyewe upo. Kama ndani ya miaka mitano, halmashauri imepeleka shilingi bilioni 20 kutengeneza barabara, je, barabara kilometa 100 ambazo zitagharimu shilingi bilioni 100 zitaweza kulipwa na halmashauri ndani ya kipindi cha miaka mitano mpaka saba? Tutakuwa hatufanyi tena sport improvement, wala periodic maintenance, barabara zile zile, kazi yetu itakuwa ni kusafisha mifereji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali iangalie jambo hili. Nikiwa Meya wa Temeke, Mradi wa DMDP ambao umekwenda kuzaa miradi hii ya TACTIC na miradi mingine; chanzo chake kilikuwa Halmashauri ya Temeke. Baada ya kutakiwa tulipe fidia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, tulitakiwa tulipe fidia ya shilingi bilioni 19, halmashauri uwezo wa kulipa shilingi bilioni 19 kwa mara moja haupo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukaandika andiko, wapo tuliobezwa, lakini kwa andiko lile tulichukua mkopo CRDB shilingi bilioni 16 tumelipa fidia. Mradi wa DMDP umejenga barabara za lami, matokeo yake na Kinondoni na Ilala wamefaidika. Kwa kutekeleza mradi huo, leo tunapata mradi wa Rais na miradi mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba sana mipango yetu ambayo Temeke tumeipeleka kwa Wizara ambayo itatuwezesha tutoke, tu-graduate, tuondokane na kutegemea fedha za Serikali Kuu, halmashauri za Dar es Salaam zinakusanya kuanzia shilingi bilioni 70 kwenda juu. Hebu ibarikini mipango yetu ili tuweze kutoka kwenye tatizo la barabara na hatimaye tuweze kujitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sitaki kulalamikia barabara za jimbo langu. Ninatoa mipango kwa Serikali, wakiibariki mipango yetu nitakuwa sina sababu ya kulalamika kwa sababu tunaenda kutekeleza miradi ya barabara kwa mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)