Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ninapenda kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo imesheheni mipango mizuri ya maendeleo yetu ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa sana anayoifanya kwa kuleta maendeleo nchi yetu ya Tanzania. Anapamba vilivyo kwa juhudi kubwa sana. Sisi ni mashahidi sana kwa kazi zinazofanyika kwenye maeneo yetu, kwenye majimbo yetu, mikoa yetu, kujenga barabara, shule, zahanati, miradi ya maji, miradi ya umeme na mingine mingi ambayo anapambana ili tupate maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kama nilivyosema ilisheheni mipango ya mendeleo na mambo yaliyofanyika na yatakayofanyika. Sasa kwenye maendeleo yoyote changamoto hazikosi. Changamoto zipo mara kwa mara, mara nyingi tu, na ndiyo maana tupo hapa kujadili na kuleta mapendekezo mazuri ya kuboresha maendeleo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema Waheshimiwa Wabunge wenzangu hapa, barabara mwaka huu 2026 zimeharibika sana ninadhani kutokana na mvua nyingi nchi nzima, zimechimbika mashimo, lami zimeharibika, system zile za udongo vijijini ndiyo kabisa, zimeharibika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inanikumbusha jambo moja kwamba katika mgao wa fedha za Road Fund (Mfuko wa Barabara), wanaopewa fedha nyingi ni TANROADS. Siyo vibaya, ni vizuri kwamba wanahusika barabara kubwa, madaraja makubwa na wana kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hii isitusahaulishe kwamba kule vijijini ndiyo kuna kazi kubwa sana ya kuzalisha mazao, kupeleka pembejeo, kutoa mazao kule kuyaleta kwenye masoko, na kuna watu wengi sana kule vijijini wanaishi huko. Sasa kuwapa TARURA fedha kidogo, inasababisha barabara za kule ziwe mbaya sana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninatoka vijijini, ni Mbunge wa Bukoba Vijijini. Barabara zangu za vijijini zina hali mbaya sana na TARURA hawana fedha. Sasa hii inakuwa kidogo ni changamoto kubwa zaidi kwenye upande wa barabara. Ningetamani TARURA apewe 70%, TANROADS 30%. Siyo kwa kuwafifiza TANROADS, lakini tuweke mkazo kwenye barabara za vijijini. Tusionekane kwamba tunapendelea watu wa mijini, barabara za TANROADS hizi, tunawasahau wa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA waongezewe fedha, wapate fedha nyingi, barabara zitengenezwe. Ni za udongo zile ndiyo zinazoathiriwa sana na mvua kuliko za lami. Sasa kama hawawezi kupewa 70%, basi angalau wapewe hamsini, hamsini wote. TARURA 50% ya zile fedha, TANROADS 50% ya zile fedha, ili tuweze kupata barabara nzuri maeneo yote ya nchi yetu. Hilo ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni la maendeleo. Tuna vijiji vingi nchi hii, tuna ardhi nyingi sana ambayo tunaitumia kwenye kuzalisha vyakula, mazao ya biashara na mengine. Ni jambo jema, lakini ardhi ile thamani yake ni hiyo tu basi, kuzalisha chakula na mazao ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni kichocheo kikubwa cha maendeleo, ni uchumi mkubwa sana. Tatizo ni kwamba ardhi hii haijapimwa wala kusajiliwa. Tuna mabenki mengi sana Tanzania, zaidi ya 45, mabenki mbalimbali, tukiongozwa na CRDB na NMB kwa ukubwa. Hizi benki 45 na zaidi zina fedha nyingi sana za maendeleo. Mnaona wanavyokuja hapa tukianza Bunge jipya, wanavyokuwa pale nje getini wanatuita njoo uchukue hela, njoo uchukue hela, wanazo hela nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili benki itoe fedha kwa mtu yeyote, lazima iwe na usalama wa fedha yako. Usalama mkubwa wa kwanza ni ardhi, lakini ardhi ambayo haijapimwa, haijasajiliwa, haina haki, haina thamani yoyote zaidi ya chakula tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninatoa wito kwa Serikali, ardhi hii ipimwe yote Tanzania, ipimwe yote. Tutenge bajeti kubwa, siyo kubwa sana ni kawaida tu. Tayari kila mkoa una masjala ya ardhi, na kila baadhi ya wilaya nyingi tu masjala zipo. Hatua kubwa kwenye kuelekea huko, tuzitumie masjala hizi ili ardhi ipimwe yote, kila mwenye ardhi yake, robo eka, eka kumi, eka mia awe na hati yake, aende benki, achukue fedha, aingie kwenye maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutapata kuchochea uchumi wetu kwa kasi kubwa sana. Watu wataanza miradi ya mbao, kukata mbao, viwanda vya selemara, viwanda vidogo vidogo, kuboresha vyakula vyetu, kuvipeleka hata nchi za nje, wataingia kwenye madini, amesema Mbunge mmoja hapa wachimbaji wadogo, wadogo daima, hawakui kuwa wachimbaji wa kati. Watapata kuchukua fedha benki kama wana hati, wataendeleza uchimbaji wao, tutapata maendeleo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutapima ardhi yetu yote, ikawa na hati, benki zitoe fedha, watu wajiendeleze, wataajiri wenzao, vijana watapata ajira, kwa sababu kutakuwa na miradi mingi, watu wakiwa na fedha kutoka benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni Jimbo langu la Bukoba Vijijini. Ninashukuru miradi ya maji inaendelea na ya umeme na mingine niliyoisema. Hata hivyo, kuna mradi mmoja wa maji pale Kemondo, unaitwa Mradi wa Maji wa Kemondo Maruku. Kati ya kata tano, kata mbili zimepata maji kwa ukamilifu, kata moja kwa sehemu, kata mbili hazijapata maji, ambazo ni Kata ya Maruku na Kata ya Kanyangereko. Sasa ni mwaka wa saba huu, tangu mradi umeanza. Naomba fedha itengwe ipelekwe pale, maji yaende Maruku na Kanyangereko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)