Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara muhimu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla sijaanza kuchangia Wizara ya TAMISEMI, wananchi wa Bunda Mjini wamechoka kusikia Habari ya mchakato unaendelea kuhusiana na mradi wa TACTIC. Wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini wanaungana na Rais wao Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba wanahitaji matokeo, wanataka stendi ya kisasa, barabara za lami, na wanahitaji soko la kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kumsaidia Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi tutawaunga mkono hasa kwa style ya Waziri Mkuu wetu ya kukemea uzembe, kuhitaji uadilifu na uchapakazi. Hayo yote ndiyo yataenda kufanya Dira yetu ya 2025 - 2050 iweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ninyi na mimi tutakubaliana kwamba nchi yetu inapiga hatua. Tunajenga miradi mbalimbali, tunajenga shule, na tunajenga hospitali. Hivi tumeshajiuliza, tutalindaje hii miradi ili vizazi na vizazi waweze kuviona?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu bado hatujawa na utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati (maintenance). Pia, ninyi mnajua, nyumba yako tu unayoishi, ukiijenga ukaiacha, baadaye ikachakaa, itakupa gharama kubwa kuirudisha katika ubora wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimetoka Dar es Salaam, kila unapopita construction zinaendelea za miundombinu mbalimbali. Hivi tumekujaje? Tumejiuliza hii miundombinu tutaitunzaje ili ibaki katika ubora wake? Lazima kama Taifa kupitia Dira hii tunayoiweka ni wakati muafaka wa kutenga fungu maalum tutakalolitafutia chanzo na kukiwekea sheria kwa ajili ya ukarabati na kulinda miradi yetu mbalimbali na miundombinu mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninapitia bajeti iliyopita, TAMISEMI peke yake imetekeleza miradi nane ya shilingi trilioni 8.9. Hii miradi tutailindaje? Tutahakikishaje inabaki na ubora na ukizingatia kwenye miradi ya Serikali hasa majengo yanapaswa kudumu kwa miaka 55? Hii miaka 55 yes, tutahakikisha inakuwa na ubora, haiwezi ikadumu kama tusipotenga fedha kwa ajili ya ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tuna shule za msingi chakavu 11,000, tuna shule za sekondari chakavu 405, na tuna madarasa chakavu 7,741. Hii tu ni sekta ya elimu, tunahitaji shilingi trilioni 3.8 ili shule hizi 11,000 za primary, shule 405 za secondary (madarasa) 7,700 zirudi kwenye hali yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani? Tuliacha zikachakaa, tumejenga, watoto wametumia, tukasahau kuweka fungu la ukarabati, na hii utaandika historia kuwa Waziri Mkuu wa kwanza utakayeweka historia ya kuhakikisha miundombinu ya Watanzania inalindwa vizuri kwa kutenga fungu maalum kwa ajili ya ukarabati, tukalitungia sheria. Tulinde miundombinu yetu ya barabara tunayojenga, tulinde shule zetu, na tulinde hospitali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo nilikuwa nimetaja sekta ya elimu. Tukija kwenye sekta ya afya, tuna zahanati 1,785 zinahitaji shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kama Taifa kwenye dira yetu, tuanze kuwa na culture ya kuweka fedha kwa ajili ya kulinda miradi yetu mbalimbali ambayo tunaijenga. Hapo nimesema zahanati, ukija kwenye vituo vya afya 534 zinahitajika fedha za ukarabati shilingi bilioni 192.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga, tumefanya maendeleo sana, tuna wajibu wa kulinda miundombinu yetu kwa kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati. Tusipofanya hivyo, tutakuwa tunajenga; yes, tunasema tumejenga barabara, tumejenga shule, tunapiga hatua kumi mbele, tunarudi sita nyuma, kwa sababu sisi wenyewe tumeshindwa kuweka mechanism ya kulinda miundombinu yetu ya kulinda miradi mikubwa tunayoijenga, ya kulinda miundombinu ya shule, ya kulinda miundombinu ya zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapo nimezungumzia hivi vilivyopo, tukija kwenye maboma, maboma ambayo yanahitaji kukamilishwa. Tuna maboma 1,596 ya zahanati: mbali na hizi shule zilizojengwa, mbali ya zilizochakaa, haya maboma kukamilika kwake yanahitaji shilingi bilioni 115, haya tumeyakamilisha, tunayalindaje ili wananchi wetu waweze kupata huduma kwenye hospitali zilizobora kwenye zahanati zilizo bora? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye hospitali ambazo bado zinahitaji shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya ukarabati, sisi tu kwenye Serikali yetu, tumeweza kukarabati maboma 346 yenye thamani ya shilingi billion 30. Kupanga ni kuchagua, hii kasi ya maendeleo inayofanywa na Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lazima tuweke mkakati wa kuhakikisha miradi yote inakuwa na ubora, na kwa kuwa na fungu la ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isipojibu hili, nitashika shilingi, kwa sababu tunataka miundombinu tunayoijenga, shule tunazozijenga, hospitali tunazozijenga zibaki na ubora wake, tuwe na culture ya kuhakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya ukarabati, na hili linawezekana. Tukiweka nidhamu tu, hata kile tunachokitengea kitumike kwa matumizi sahihi. Hata hivyo, tukienda kwenye culture, kama tunatenga fedha za mfuko wa barabara zipo kwenye ring-fence lakini mpaka leo 42% tu wamepokea, haitakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana tulinde miradi yetu, tulinde miundombinu tunayoijenga ili iwe na tija. Vizazi na vizazi, vitakuja kutukumbuka Bunge hili kwenye dira hii ya 2025 - 2030 kwamba, kulikuwa na Bunge, liliamua kuweka utaratibu wa kuhakikisha miradi inayojengwa inabaki kwenye ubora, ili tuweze kupiga hatua kwa namna ambavyo tunataka Taifa letu liende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, narudi Jimbo la Bunda Mjini. Jana, Mheshimiwa Waziri Dkt. Dugange nimempa document ya miradi viporo na maboma ya zaidi ya shilingi bilioni 2.4 inahitaji kukamilika kwenye Jimbo la Bunda Mjini, ili wananchi wangu waweze kupata huduma bora za afya, huduma bora ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)