Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia hoja hii, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ambaye amenibariki kupata nafasi ya kushiriki katika Bunge hili Tukufu kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Korogwe Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kati ya wengi kuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi katika Jimbo letu la Korogwe Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninawashukuru sana wananchi wa jimbo langu la Korogwe Mjini ambao wamenipa imani kubwa, ambao wameniunga mkono kwa kura nyingi katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29. Imani waliyonipa nami ninawaahidi nitawalipa kwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba tunatetea maslahi ya Jimbo la Korogwe Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeze Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anatekeleza majukumu yake na hasa kwa namna alivyotekeleza ahadi zake alizoziweka kwa ajili ya siku 100 za kwanza katika uongozi wake. Hakika mama ameamua kuitumikia nchi na tunaona akifanya kwa vitendo na Mungu ambariki azidi kumpa afya njema aendelee kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninampongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa namna ambavyo anaendelea kufanya kazi usiku na mchana pasipo kuchoka. Vilevile, tunamshukuru kwa ziara alizozifanya katika maeneo mengi ya nchi hususan sisi Wabunge wa Mkoa wa Tanga kwa namna ambavyo ziara yake aliyoifanya katika mkoa wetu wa Tanga imeleta tija kubwa na imeleta mwamko na uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali katika Mkoa wetu wa Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Jimbo la Korogwe Mjini wanamwomba, kwa kuwa katika ziara yake hawakupata nafasi ya kutoa kero zao kwa sababu kwa bahati mbaya ratiba haikuruhusu kuwa na wakati wa maswali alipokuwa katika eneo la Mswaha, basi wakati mwingine akipita atenge muda wa kukutana na wananchi wa Korogwe Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mkuu wangu wa Mkoa Dkt. Batilda Buriani kwa namna ambavyo anaendelea kufanya kazi kwa maslahi mapana na maendeleo ya Mkoa wa Tanga, na pia Mwenyekiti wetu wa Chama Ndugu yetu Rajabu Abdallah kwa namna ambavyo amekuwa kinara wa kuhakikisha duka la Mkoa wa Tanga linaendeshwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hakika katika awamu yake ya uongozi, miradi mingi mikubwa ya maendeleo imetekelezwa katika jimbo letu la Korogwe Mjini. Tumeona shule nyingi za sekondari zikiwa zimejengwa katika jimbo letu la Korogwe Mjini, tumeona sasa hivi ujenzi wa barabara ya TACTIC kilometa 10.4 ukiwa unaendelea na tunatazamia kabla ya mwisho wa mwaka huu, ujenzi ule utakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi ule utakwenda kubadili sura na mwonekano wa jimbo letu la Korogwe Mjini. Tutakuwa tunakwenda kupata barabara za lami, lakini pia taa za barabarani pamoja na mifereji, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imejaa matumaini makubwa kwa wananchi, imejaa nuru kwa wafanyabiashara, lakini vivyo hivyo pia matarajio ya maendeleo katika maeneo mengi na nyanja tofauti tofauti katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwa upande wa Jimbo letu la Korogwe Mjini tunapoongelea mageuzi ya kiuchumi na ongezeko la ajira, tuna vitu kadhaa ambavyo kwetu ni kipaumbele. Katika ziara ya kampeni ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyopita katika jimbo letu la Korogwe Mjini tulimwomba na aliridhia ujenzi wa bandari kavu katika Jimbo la Korogwe Mjini katika eneo letu la Kata ya Old Korogwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari kavu hii ina maana kubwa sana katika uchumi wa watu wa Korogwe. Bandari kavu hii itakwenda kupunguza congestion ya malori katika barabara ya Tanga – Segera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari kavu hii itakwenda kuongeza mzunguko wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, na wa kati katika Mji wetu wa Korogwe Mjini. Kwa hiyo, tunaomba, katika bajeti itakayoletwa, tuone utekelezaji wa ujenzi wa bandari kavu katika mji wa Korogwe, kwa sababu kwetu sisi hii inakwenda kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana wa Korogwe Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ilipitisha ujenzi wa bonde la umwagiliaji katika Kata yetu ya Kwamsisi kwa takribani shilingi bilioni 24.5 na pia, katika Kata ya Kwamndolwa kwa takribani shilingi bilioni nne. Ujenzi ule hauendelei kwa sasa. Tunaomba katika bajeti ya kilimo itakayokuja, basi miradi hii ioneshwe namna gani inakwenda kutekelezwa katika kipindi cha bajeti hiyo inayokuja kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nayo inakwenda kuchochea uchumi na uzalishaji wa mazao ya chakula pamoja na mbogamboga katika maeneo yetu ya Jimbo la Korogwe Mjini. Miradi hii ina tija kubwa, ninaomba tuipe kipaumbele cha juu ili kuhakikisha tunakwenda kuitekeleza na kukamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Kwamndolwa umekaa kwa muda mrefu, wakandarasi wameenda pale zaidi ya watatu wakiwa wanabadilishwa badilishwa kwa kushindwa kutekeleza mradi ule. Sasa wananchi wa Kata ya Kwamndolwa hawana imani kama kweli ahadi iliyowekwa itakwenda kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa imani yangu kubwa tuliyokuwanayo kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri mahiri wa Kilimo tunaamini mradi ule unakwenda kutekelezwa na ninaomba upewe kipaumbele cha kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba alipofanya ziara yake Mkoa wa Tanga tulimwomba kuhusiana na hospitali yetu ya Magunga. Kutokana na eneo iliyopo, Hospitali ya Magunga inahudumia watu wengi na siyo tu wakazi wa Jimbo la Korogwe Mjini, bali Wilaya za Lushoto, Handeni, na maeneo ya karibu ya Wilaya ya Muheza wote wanapata huduma hapa. Siyo hayo tu, kwa sababu ipo katikati ya barabara kubwa, wagonjwa wanaotokana na ajali za barabarani wengi wamekuwa kimbilio lao la kwanza ni Hospitali ya Magunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hiyo imekuwa kongwe kwa kuwa imejengwa tangu mwaka 1952, na sasa ina umri wa miaka zaidi ya 73. Tuliomba hospitali ile ijengwe upya na tunashukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetuletea shilingi bilioni moja ambayo tunatazamia kuanza ujenzi wa maternity complex.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa badala ya kuweka viraka katika hospitali ile, bajeti ya mwaka huu 2026/2027 na kuendelea, sasa iwekwe angalau kila mwaka tupate jengo moja kubwa jipya ili baada ya miaka mitatu au mitano tuwe tumepata majengo yote mapya ya Hospitali ya Magunga, iendane na hadhi ya ukuaji wa Mji wa Korogwe, na pia uendane na barabara hii sasa ambayo tunaitoa kutoka NMB kwenda katika Hospitali ile ya Magunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa barabara pamoja na kupata kilometa 10.4 za TARURA kupitia TACTIC, na bado jimbo letu lina changamoto kubwa sana ya barabara. Hivi tunavyoongea, na mvua zinazoendelea katika Mkoa wa Tanga Kata zetu za Mtonga, Bagamoyo, na Kilole miundombinu yake haipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba wenzetu wa TAMISEMI katika bajeti yao watutengee angalau kuongeza kilometa 10 - 15 za changarawe katika Jimbo la Korogwe Mjini. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumepunguza changamoto ambazo watakuwa wanazipata.
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. CHARLES M. NJAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)