Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax, Waziri wa Ulinzi kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Katika kipindi chake akiwa Waziri wa Ulinzi, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno katika ulinzi na amani na kupelekea kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio makubwa ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, bado kuna wapiganaji wetu ambao ni wastaafu na wengine walishiriki kwenye vita kwa kulinda mipaka yetu hususani vita ya Kagera, wanalalamikia stahiki zao kutolipwa kikamilifu. Kwa kuzingatia wamefanya kazi kwa uzalendo mkubwa na iwe motisha kwa askari wetu, napendekeza Serikali iangalie jinsi ya kutatua changamoto hii na kuangalia upya stahiki zao ikiwemo kuboresha mafao ya pensheni zao.
Mheshimiwa Spika, napendekeza Wizara ya Ulinzi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu kuangalia jinsi ya elimu ya ulinzi na usalama kuunganishwa kwenye mitaala ya elimu. Pia Serikali iendelee kuboresha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ikiwemo mafunzo ya uzalendo na ujasiriamali. Kutokana na mafaniko makubwa ya mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria, Serikali irudishe utaratibu wa mafunzo hayo kwa miezi kumi na mbili na mafunzo haya yawe maandalizi ya kuwajenga vijana kwenye uzalendo na ulinzi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.