Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, niungane na wasemaji wote waliotangulia kusema kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kukutana tena katika siku hii muhimu ya kuhitimisha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2026/2027 tukiwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, ninakupongeza sana wewe mwenyewe; Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuongoza kwa umahiri na weledi mkubwa mijadala kuhusu hoja ya Bunge ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Ninakupongeza sana na ninakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Mbunge wetu wa Njombe, Mheshimiwa Mwanyika; Mheshimiwa Najma Giga na Mheshimiwa Cecilia Paresso. Kadhalika ninawapongeza Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge: Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI; Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii; na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa uchambuzi na michango yao kwenye bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli na ni ukweli usiopingika kwamba maoni yao pamoja na ushauri wao kwa wakati wote umekuwa na manufaa makubwa na umesaidia katika kutengeneza waraka huu. Kwa dhati ya moyo wangu pia ninapenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao. Hoja na michango yao waliyotoa inaakisi maeneo yote muhimu yanayohitaji kuimarishwa zaidi katika suala zima la kuwahudumia wananchi na kuboresha utendaji wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali itazingatia michango yao yote waliyoitoa katika utekelezaji na kuweka vipaumbele vya Serikali katika bajeti inayoendelea. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na tunawapongeza sana na kama ambavyo wenzangu waliotangulia kusema leo siyo siku ya kujibu bali ni siku ya kupokea maoni na mengine tutaendelea kuyafanyia kazi katika utekelezaji wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu. Kipekee nimkaribishe Ofisi ya Waziri Mkuu na nimtakie kila la heri mwalimu katika kutekeleza majukumu yake hayo mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Mheshimiwa Profesa Riziki Silas Shemdoe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kufanya. Nitumie nafasi hii kuwashukuru sana na kuwapongeza sana, wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha majukumu yaliyoko ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu na hususan katika Wizara ambazo Mheshimiwa Rais amewaamini katika kutimiza majukumu hayo ya kumsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie vilevile nafasi hii kuwashukuru: Mheshimiwa Ummy Hamisi Nderiananga, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu; Mheshimiwa Rahma Riyadh Kisuo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano; Mheshimiwa Dkt. Festo John Dugange na nimpongeze kwa majukumu hayo mapya ambayo ameaminiwa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI anayesimamia elimu; pamoja na Mheshimiwa Dkt. Jafar Rajab Seif, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI anayesimamia masuala ya afya. Wote kwa pamoja ninawapongeza kwa kazi nzuri wanaofanya na ninawashukuru sana kwa kutimiza vizuri majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye ufafanuzi wa hoja chache baada ya kuwa Waheshimiwa Mawaziri wamekwisha kufafanua, niungane na Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri ambao wamepata fursa ya kuchangia kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi ambazo amezifanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wala haziwezi kufifishwa wala kufutwa kwa kutokuzisemea. Legacy ambayo Mheshimiwa Rais ameiandika wala haiwezi kufutwa kwa maneno, wala haiwezi kufutwa kwa chuki, wala haiwezi kufutwa kwa kutokutambua. Mheshimiwa Rais ameingia kwenye kumbukumbu ya viongozi wachache ndani ya nchi yetu ambao wamepata heshima na bahati ya kuandika dira ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo atafafanua kwa kirefu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, atakapoleta bajeti. Mheshimiwa Rais amekamilisha tena kwa umahiri mkubwa kuandika Dira ya nchi yetu ambayo haitaandikwa tena mpaka baada ya miaka 25 mingine. Kwa hiyo, ameingia kwenye kumbukumbu ya viongozi walioandika Dira ya Taifa letu. Tena ameboresha utaratibu wa uandishi wa Dira kwa kuandika Dira pamoja na nyaraka zingine muhimu za utekelezaji wa Dira ikiwemo Mpango wa Muda Mrefu ambao sasa umeandikwa sambamba na Dira tofauti na miaka mingine ambayo iliandikwa kwanza Dira na mipango ikaja kufuatia miaka 10 baadaye.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amefanya mageuzi makubwa katika elimu. Leo hii tunavyoongea na kama ambavyo umetoka kuwasikiliza Waheshimiwa Mawaziri tutaanza utekelezaji wa mitaala mipya ya elimu ambapo elimu ya msingi ya lazima itakuwa miaka 10. Jambo la aina hii kwa mara ya mwisho lilifanyika mwaka 1967. Mageuzi ya aina hii katika elimu yalifanyika kwa mara ya mwisho mwaka 1967. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa wazee wetu wanakumbuka wakati tunatoka kwenye elimu ya lazima iliyokuwa inaenda mpaka darasa la nne kwenda mpaka darasa la saba. Haya ni mageuzi makubwa ambayo hata tusiposema yatakuwepo katika historia kwamba yalifanyika wakati wa Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya si mageuzi tu ya kubadilisha miaka lakini ni mageuzi ambayo yameambatana na vitu vya msingi ambavyo vimekuwa kilio cha wadau na Watanzania kwa muda mrefu. Mheshimiwa Rais amechukua ujasiri bila kujali gharama kuweza kuhakikisha kwamba watoto wa Kitanzania wanapata elimu wanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya kutekeleza mpango huu mpya yameshafanyika kwa kiwango kikubwa na mengine yataendelea kukamilishwa ili kuweza kuhakikisha kwamba jambo hili kubwa katika nchi yetu linatekelezeka. Utakumbuka kwa miaka mingi iliyopita tulikuwa na takribani shule tano tu ambazo tunaweza tukaziita ni za ufundi. Miaka yote ile tulikuwa tunapambania shule tano watoto wote wa Kitanzania waende katika shule hizo tano.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amejenga shule za amali 103 kwa mpigo. Kwenye hizo 103; shule 29 ni za kihandisi moja kwa moja watoto wanasoma engineering kuanzia katika ngazi hizo. Ni katika awamu yake pia, yamejengwa madarasa mengi kwa mpigo. Madarasa 79,000 ambayo yameondoa kabisa utaratibu wa second selection, utaratibu ambao ulikuwa unapoteza fursa za watoto wa Kitanzania kwenda kupata masomo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi huku kwetu kuanzia hapa hapa kwa ndugu zetu Wagogo, kwetu huko Unyirambani kwa Wanyaturu, kwetu huko Usukumani, ukisema second selection unakuta watoto wa kike wamechaguliwa kwingine kule kwenye chaguraga mayo, anakuwa ameshaolewa, ikija second selection anakosa masomo. Uwepo wa shule na madarasa ya kutosha unatuhakikishia uwepo wa viongozi miaka ijayo ambao watatengenezwa kupitia fursa hii ya kutokukosa masomo na hii inaendelea kutuelezea tafsiri halisi ya kazi na utu.
Mheshimiwa Spika, yamejengwa madarasa zaidi ya 79,000 na shule za wasichana kila mkoa. Vimejengwa Vyuo vya Ufundi (VETA) kila wilaya ya nchi hii, ambayo ilikuwa haina Chuo cha VETA na vipo ambavyo viko katika hatua ya ukamilishwaji ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Sekta ataelezea kwa kina.
Mheshimiwa Spika, hili ni jambo kubwa ambalo limefanyika ndani ya nchi yetu katika kipindi cha Dkt. Samia Suluhu Hassan. Zimejengwa shule zaidi ya 1,300 za sekondari kwa ujumla wake, zaidi ya shule 2,700 za msingi, lakini pia, ndiyo muda ambapo vimejengwa vyuo vya kati na vyuo mbalimbali, ikiwa ni matawi ya vyuo vikuu katika kila mkoa wa Tanzania kwa upana wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais pia, anaingia kwenye rekodi ya kutekeleza jambo hili kubwa kwa sheria na utekelezaji wake, jambo la Bima ya Afya kwa wote. hili ni jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amesimamia kutungwa kwa sheria yake katika uongozi wake, lakini pia, mpango huu utekelezaji wake umeanza katika awamu yake. Tutaendelea kuuboresha, kama ambavyo tumeendelea kuelezea maelekezo ambayo ametupatia, ili kuweza kuhakikisha kwamba, Watanzania wananufaika na jambo hilo kubwa la afya. Jambo hili la bima ya afya kwa wote na lenyewe siyo tu sheria na siyo tu matamko, yamefanyika mambo makubwa kwenye miundombinu ya afya kuweza kuhakikisha kwamba, jambo hili linatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mambo makubwa ambayo yamefanyika, itakumbukwa kwamba, tulikuwa na wilaya zaidi ya 100 hazina hospitali ya wilaya. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Awamu yake ya Kwanza ya uongozi amejenga hospitali za wilaya na halmashauri 119 kwa mpigo. Tulikuwa na Makao Makuu ya Tarafa ambayo hayana vituo vya afya, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amejenga vituo vya afya 649 kwa mpigo vyenye hadhi ya hospitali za wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Rais anaingia kwenye kumbukumbu ya mageuzi makubwa kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo. Kama ambavyo umetoka kumsikia Waziri wa Kilimo, tumekuwa na kauli mbiu mbalimbali; Kilimo Kwanza, Kilimo ni Uti wa Mgongo, Kilimo ni Siasa na nyingine zote, lakini ni ukweli usiopingika kwamba, bajeti za kilimo hazikuwahi kuakisi yale mambo ambayo yamesemwa katika kauli mbiu hizo.
Mheshimiwa Spika, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa na ujasiri wa kuwekeza fedha nyingi za kiwango hicho kwenye kilimo. Bajeti ya kilimo imeongezeka kwa zaidi ya mara tano ndani ya awamu moja ya uongozi ambapo imetoka kutoka takribani shilingi bilioni 270 kwenda zaidi ya shilingi trilioni 1.2, hizi si namba za kwenye vitabu. Nimepita katika maeneo ya wilaya zetu, mikoa yetu na vijiji vyetu nimejionea miradi ya umwagiliaji yenye mabilioni ikiwa kwenye kijiji na imelenga kubadilisha maisha ya wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni nadra zamani kukuta mradi wa umwagiliaji umepelekwa kwenye kijiji, shilingi bilioni 30. Sasa hivi ni miradi ya kawaida iko vijijini, shilingi bilioni 30, shilingi bilioni 50, nimeenda juzi tukiwa pale Isimani tumepata taarifa ya Mwenyekiti wa Chama wa pale Isimani akielezea mradi wa zaidi ya shilingi bilioni 50 uko kwenye tarafa.
Mheshimiwa Spika, nimepita kule Karatu nimeona mradi wa umwagiliaji, nimepita Manyara nimeona mradi wa umwagiliaji na ninakumbuka miradi mingine ambayo inaendelea kwenye utekelezaji. Mheshimiwa Rais amekuta tuna takribani miradi 13 ya umwagiliaji na sasa kuna miradi zaidi ya 780, ambayo inajengwa na ni miradi ya umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais anaingia kwenye kumbukumbu kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati. Wakati Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ukianza Mheshimiwa Rais alikuwa Makamu wa Rais, ameupokea mradi huo ukiwa umetekelezwa takribani 27% kwenda 30%. Katika awamu yake Mheshimiwa Rais ameelekeza tufunge mikanda vyovyote vile tuwezavyo tuweze kuhakikisha mradi huo mkubwa wa ndoto ya Mwalimu Nyerere unatekelezwa na unakamilika kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania. Mradi huo ambao umetumia zaidi ya shilingi trilioni 6.5 umekamilika na sasa umeiweka nchi yetu kuwa nchi yenye ziada ya umeme.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ambayo sasa ina ziada ya zaidi ya megawatts 2000 za umeme kutokana na kukamilika kwa mradi huo. Kama vile hiyo haitoshi, Mheshimiwa Rais kaweka zaidi ya shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya mradi wa gridi imara, ili kuweza kuondokana na jambo la kukatikakatika kwa umeme. Nilipita kuweka jiwe la msingi pale Mkata moja ya mradi wa gridi imara unaounda miradi ambayo itagharimu zaidi ya trilioni shilingi 1.2, ili kuondokana na jambo la kukatikakatika umeme.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wakati wanachangia wameelezea kero hiyo ya kukatika umeme. Ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kukatikakatika umeme kwa sasa si upungufu wa umeme bali ni kwamba, gridi imejengwa siku nyingi na wakati huo makadirio ya umeme yalikuwa katika matumizi ya watu wachache, kwa sasa hivi ni kila kijiji, lakini Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali anayoiongoza ameliona jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa shilingi trilioni 1.2 wa kujenga gridi imara ili kuweza kuhakikisha kwamba, tunaondokana na tatizo hilo la kukatika katika umeme. Mheshimiwa Waziri wa Sekta atakapokuja kusoma bajeti ya kisekta atawaelezea maeneo ambayo yataondokana na kero hiyo ya kukatikakatika umeme punde zile gridi za ile miradi ya gridi imara itakapokuwa imekamilika.
Mheshimiwa Spika, kama vile hiyo haitoshi, kwenye miradi ya kimkakati, Mheshimiwa Spika wewe ni mkongwe katika Bunge hili, Unakumbuka jinsi ambavyo kila Bunge Waheshimiwa Wabunge wameimba kuhusu miradi ya kimkakati, LNG, Liganga na Mchuchuma. Mheshimiwa Rais kwa uthubutu wake na kwa umakini wa kuzingatia matumizi bora ya rasilimali za nchi yetu anakwenda kuikwamua miradi hii.
Mheshimiwa Spika, miradi hii yote imepiga hatua nzuri. Ipo kwenye hatua nzuri ambayo tunaamini siku si nyingi, kupitia Kamati za Bunge, taarifa hizo zitaanza kutolewa, za hatua za ukamilishwaji wa miradi hiyo. Miradi ambayo itakwenda kubadilisha kabisa kiwango cha uchumi wa nchi yetu. Mradi kama wa LNG wenye takribani uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 42, takribani shilingi trilioni 100, unaenda kuifanya Tanzania kuwa ni big brother wa GDP kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na SADC.
Mheshimiwa Spika, haya yote ni maeneo ambayo yanakwenda kumweka Mheshimiwa Rais kwenye kumbukumbu kupitia legacy yake ambayo ameifanya kupitia miradi hii mikubwa. Hivyo hivyo na kwenye miradi mingine ambayo imetekelezwa, ukiwepo Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR, ambapo sasa kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma inatumika. Juzi imetolewa award, imetolewa zawadi ya best arrangement, utaratibu mzuri wa kutafuta fedha za kutekeleza miradi kwa lot ya tatu na ya nne, kipande cha tatu na cha nne, ambapo taasisi kubwa duniani zimetolea mfano kwamba, Tanzania ni nchi ya mfano kwenye kutafuta rasilimali za kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kama hiyo ya reli.
Mheshimiwa Spika, wenzetu wamekwenda kupokea zawadi hiyo kupitia taasisi kubwa za fedha, ikiwemo Benki ya Dunia, IMF, Shirika la Fedha la Kimataifa, pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika ambapo sasa kipande cha tatu na cha nne kimepata fedha. Kipande cha tano kimepata fedha na utekelezaji wake unategemea tu zile certificate za mtekelezaji kadri anavyokamilisha, fedha za utekelezaji wa mradi huo zipo tayari. Kipande cha kutoka Tabora kwenda Kigoma na chenyewe Benki ya Maendeleo ya Afrika ndiyo ambaye ni leader ranger katika kuhakikisha kwamba, fedha za kutekeleza mradi huo vinapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna wakati sisi Watanzania huwa tunapenda kujidogosha na hasa tusipofanya ulinganifu na nchi zingine. Hapa Tanzania tunaongelea kila kitongoji na kila kaya kupata umeme, kuna nchi hapa hapa Afrika ambazo wameunganisha makao makuu tu ya mikoa tu umeme kwingine kote ni mtu na generator yake na mtu na solar yake. Sisi kila kijiji umeme umeshafika na kwenye vitongoji takribani 68,000 nusu yake vimepata umeme.
Mheshimiwa Spika, katika kazi hii inayofuata, ambavyo kama watapata undani wake kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Sekta, tayari vitongoji zaidi ya 9,000 mkataba umesainiwa na kazi hiyo inavyoendelea mpaka ifikapo 2030 uwezekano mkubwa kwamba vitongoji vyote vitakuwa vimepata umeme. Hii ni hatua kubwa ambayo kila mmoja anatakiwa aone heshima kwamba, yuko kwenye nchi ambayo viongozi wake wanajali maisha ya kila mtu na kuhakikisha kwamba, keki ya Taifa inamfikia kila mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, tunaongelea vijiji vyote kupata maji na kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Sekta amesema, ni vijiji 1,500 tu bado havijapata mradi wa maji. Hapa tulipo, katika ilani, bajeti zinazofuata na katika dira, uelekeo ni kuwa na maji ya uhakika kupitia Gridi ya Taifa, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ametoka kugusia na anajua ataelezea kwa kina wakati atakapoleta bajeti. Hilo ni jambo lingine ambalo linatutofautisha na nchi nyingi.
Mheshimiwa Spika, nimeshiriki vikao kadhaa vya Benki ya Dunia. Mara zote Tanzania ilikuwa inatolewa mfano na inapata heshima ya kuwaelezea nchi zingine wamefanya nini kuhusu maji, kuelezea nchi zingine wamefanya nini kuhusu umeme, kuelezea nchi zingine wamefanya nini kuhusu maeneo ya nishati. Haya ni mambo ambayo nasema Mheshimiwa Rais ameandika historia, ameweka legacy na ataendelea kuwepo kwenye kumbukumbu hizo za kuipeleka nchi yetu katika hatua kubwa ya kimaendeleo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu upande wa utawala bora, ambapo Waheshimiwa Wabunge wameelezea kwa kina. Tumepokea yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa ushauri na sisi tutaendelea kuyafanyia kazi. Mengine ambayo bado hatujagusia tumeyapokea, lakini kila Waziri atakapokuwa anasimama yale yanayogusa Wizara za Kisekta Waheshimiwa Mawaziri wataendelea kuyafafanua tutakapokuwa tunaleta hoja za kisekta.
Mheshimiwa Spika, imeongelewa sana kuhusu TARURA, barabara na maeneo mengine ambayo nimeyasema. Nimesema wakati nawasilisha bajeti kwamba, tunatarajia tutakapoanza utekelezaji wa bajeti hii tutawianisha fedha zinazotoka moja kwa moja kwenye makusanyo kwenda kwenye mifuko ya fedha ambayo imekuwa ring fenced ziende moja kwa moja kwenye mifuko kuanzia kwa wakusanyaji, ili kuanzia kwa chanzo chetu cha makusanyo, mamlaka ya mapato, kwenda kwenye mifuko husika, ili waweze kutekeleza miradi ya maendeleo inayowahusu.
Mheshimiwa Spika, katika kuhitimisha ninaendelea kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuhitimisha bajeti yetu. Kipekee ninaendelea kuwashukuru wadau ambao wamehusika katika kukamilika kwa hotuba hii. Ninaanza na Makatibu Wakuu, Dkt. Jimmy Yonazi upande wa Sera, Bunge na Uratibu na Wenye Ulemavu, Bi. Mary Maganga – Kazi, Ajira na Mahusiano. Bwana Adolf Ndunguru – TAMISEMI, Makatibu Tawala wa Mikoa, pamoja na Wakuu wa Mikoa ambao ni askari wa mwavuli kwa kule mikoani.
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Naibu Makatibu Wakuu: Dkt. James Kilabuko – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu. Bi Zuhura Yunus – Kazi, Ajira na Mahusiano, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bwana Sospeter Mtwale, Mhandisi Rogatus Mativila, Bwana Atupele Mwambene pamoja na Profesa Tumaini Nagu. Kipekee pia, ninawashukuru wakuu wa idara zote na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ambayo wameifanya.
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila pia, kama sitawashukuru Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na taasisi zake. Sasa baada ya maelezo haya ninatumia nafasi hii adhimu kuliomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake, Mfuko wa Bunge, kama ilivyoainishwa katika hoja yangu ya tarehe Mosi Aprili, 2026.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja. (Makofi)