Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim kwa kuturuzuku uhai, lakini kutujalia afya njema ya kutuwezesha kukutana katika Bunge lako Tukufu na kuelekea kukamilisha hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nichukue nukta hii kukushukuru sana kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu, lakini pia niweze kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kabla ya hilo, kipekee kabisa ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru kwa dhati kabisa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kunistahilisha nisiyestahili katika Serikali yake na kunipa imani kubwa katika nafasi mbalimbali. Ninamshukuru sana tarehe 17 Novemba, 2025 alivyoniteua kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Ninamshukuru sana tarehe 8 Januari, 2026 alivyoniteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Kazi Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru pia Mheshimiwa Rais tarehe 2 Aprili, 2026, aliponiteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu. Imani hiyo ya Mheshimiwa Rais katika muda huu wa miezi mitano, kunituma kazi katika maeneo matatu, amenipa heshima kubwa sana ambayo daima nitaiheshimu na kuienzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa amenipa kazi hii, jukumu hili ambalo ninataka nimhakikishie kwa heshima hii aliyonipa nitaitumikia nafasi hii na nina dhamira ya kuhakikisha kabisa kwamba, nitafanya kazi kwa bidii, kujituma, weledi, uaminifu na unyenyekevu mkubwa kwake. Pia nitahakikisha ninamsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa moyo wangu wote kwa nguvu zangu zote na akili zangu zote akiwa msimamizi wa uratibu wa shughuli za Serikali na Kiongozi wa shughuli za Serikali hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amenifundisha mengi, lakini kubwa ni hili Kazi na Utu (Work and Dignity), kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Mheshimiwa Rais katika ile kauli mbiu tuliyoanza nayo ya uhuru ni kazi, kazi iendelee, hapa ni kazi tu, sasa ameongeza suala zima la utu na utu huo unaendana na dhamira yake kubwa kwamba wananchi wa Tanzania wawe na tabasamu katika uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia, kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyomsaidia Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuliongoza Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii vile vile kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Mbunge na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza, kwa kuendelea kuratibu shughuli za Serikali, lakini pia kwa kutupa maelekezo na miongozo katika kutekeleza majukumu ya kila siku ya Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu kama wote walivyosema amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali. Kubwa nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu sana ameanza kazi hii kwa spidi kubwa.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie pamoja na rika langu, nimejifunza sasa kuanza kukimbia na ninaamini baada ya muda mfupi mwili huu utapungua kidogo. Kwa hiyo, atakuwa amenisaidia kuimarisha afya yangu. Kwa hiyo, ameufanya uzee wangu urejee kuwa ujana kwa sababu ya spidi ya kazi anayoifanya. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, tarehe 2 Januari alitembelea Jimbo la Kilosa kuja kujionea mwenyewe hali ya mafuriko kule Tindiga, lakini pia alifika Kidete na aliona hali nzima ya Reli ya SGR na matatizo yale ya mafuriko. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba hii nzuri kabisa aliyoitoa hapa Bungeni na ambayo leo tunaihitimisha kwa ufasaha mkubwa na inayoakisi mahitaji ya Taifa letu, lakini pia inaendelea kutupa mwelekeo sahihi katika kutekeleza majukumu ya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe na nikushukuru pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika kwa ufanisi katika kuliongoza Bunge letu Tukufu. Aidha, ninawashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria; Kamati ya Kudumu ya Bunge Afya na Masuala ya UKIMWI; na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa uchambuzi na maoni yao mbalimbali yanayohusu Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni pamoja na sehemu ya Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu. Maelekezo na maoni yao tutayazingatia.
Mheshimiwa Spika, kwa kipekee nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Eveline Munisi Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hatua hiyo inadhihirisha utashi na dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kukuza uhusiano kati ya vyama vya siasa, lakini kuibua vipaji vya wanasiasa vijana, wanawake kutoka vyama mbalimbali ili waweze kutoa mchango wao katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuna budi kumhakikishia Mheshimiwa Dkt. Evaline Munisi shirikiana na Waheshimiwa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi ili kuhakikisha yale ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameazimia yanatekelezwa. Pia yeye awe sauti ya Watanzania wengine katika nafasi yake katika kueleza yale matarajio ya wanawake na wasichana wa nchi hii katika maendeleo ili wao nao wapate nafasi ambayo baadaye itazidi kuimarisha demokrasia na kuleta maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru pia wafanyakazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu walio chini yangu. Kwanza kabisa Mheshimiwa Ummy Hamisi Nderiananga, Naibu Waziri kwa msaada mkubwa ambao ananipa katika Ofisi hii na katika muda mfupi huu nimekuwa mwanafunzi wake mzuri sana katika maisha haya.
Mheshimiwa Spika, watu watajiuliza kwa nini mwanafunzi? Kwa sababu kila Ofisi ina utamaduni na mila zake. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Ummy kwa kunisaidia kujua mila na desturi za Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, nimshukuru sana Dkt. Jim James Yonazi, Katibu Mkuu; Dkt. James Henry Kilabuko, Naibu Katibu Mkuu; pamoja na wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku na hasa katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa na bahati sana kila ninapoteuliwa, ninateuliwa wakati wa bajeti. Kwa hiyo wamenisaidia sana kuijua hii bajeti katika muda mfupi, inaelekea wapi ili tutakapoanza kuitekeleza niwe katika mstari ambao tayari walikwishauanzisha. Pia, ninawashukuru wadau mbalimbali tunaoshirikiana nao katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwemo: Shirikisho la Sekta Binafsi (Tanzania Private Sector Foundation); Baraza la Vyama vya Siasa; na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIYAWATA). Aidha, ninawashukuru pia wadau wote wa maendeleo kwa michango yao wanayotoa kufanikisha majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nami pia nitoe shukrani kwa wananchi wa Jimbo la Kilosa, kwanza kwa kuniamini na kunichagua kuwa Mbunge wao. Ninawaahidi kwamba katika kipindi hiki pamoja na majukumu yote haya niliyopewa daima niko nao na daima nitahakikisha maendeleo ya wananchi wa Kilosa yanazidi kusonga mbele kwa faida ya Kilosa yenyewe, kwa faida ya Mkoa wa Morogoro, lakini pia kwa faida ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tukitambua kwamba Wilaya ya Kilosa na Mji wa Kilosa ni mji wa kimkakati.
Mheshimiwa Spika, hilo litakuja kudhihirishwa na Waziri wa Uchukuzi atakapokuja kueleza; ninaamini umuhimu wa Mji wa Kilosa kwa sababu ndiyo mji pekee unaounganisha reli tatu katika nchi yetu. Reli ya TAZARA, Reli ya SGR na Reli ya MGR. Wote wanaopanda treni ya SGR zile tunnels (mahandaki) yote wanayoyapita wajue yako katika Jimbo la Kilosa. Kwa hiyo, nawakaribisha sana, wanapopita kwa utalii mzuri wa tunnels katika Jimbo la Kilosa.
Mheshimiwa Spika, ili Mheshimiwa Profesa Shemdoe asiwe peke yake, sikupata shoti lakini mimi pia nimshukuru sana mke wangu Dkt. Amina Kabudi na watoto wangu Dkt. Tumaini Kabudi na Aidan Kabudi kwa msaada mkubwa wanaonipa, upendo na uvumilivu katika kutekeleza majukumu yangu haya ya ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Ofisi yetu ya Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu imepata michango 32 na siwezi kutoa majibu kwa hoja zote. Kwa hiyo, nitaomba taarifa yangu hii au mchango wangu huu baadaye wote uchukuliwe kuwa sehemu ya Hansard.
Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ambayo ilitolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Sheria na Katiba ilikuwa ni kwamba Serikali ihakikishe inaimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati kwa kuzingatia thamani ya fedha na malengo yanayokusudiwa. Ushauri huo umepokelewa na Serikali imechukua hatua za kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwa kufanya yafuatayo:-
(i) Kuboresha Mwongozo wa Kitaifa wa Miradi ya Maendeleo kwa lengo la kuhimiza uwepo wa mpango wa madhubuti wa ufuatiliaji na tathmini tangu mwanzo;
(ii) Kuimarisha matumizi ya teknolojia kupitia Mfumo wa NPMIS unaowezesha ufuatiliaji wa miradi kwa wakati halisi; na
(iii) Kufanya ziara za ukaguzi wa miradi moja kwa moja kwenye maeneo ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika taasisi zote za umma ili kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi kwa ufanisi na kuhakikisha miradi inaleta matokeo chanya kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo lililetwa; hoja nyingine ilikuwa ni gharama za mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kule Zanzibar zijulikane na ujenzi wake uanze ili fedha zinazotengwa kwenye bajeti ziweze kutolewa.
Mheshimiwa Spika, ushauri huu umepokelewa na Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) ambaye ndiye mshauri elekezi wa ujenzi wa Jengo la Usajili wa Vyama vya Siasa Zanzibar. Amekamilisha michoro ya jengo hilo na kwa sasa nyaraka za zabuni ikiwemo BOQ zinakamilishwa. Hivyo gharama za ujenzi wa jengo hilo zitafahamika na baada ya taratibu za zabuni kukamilika ujenzi utaanza na baada ya mkandarasi kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo lililetwa ni hoja ya kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa ya Kulevya uimarishe udhibiti wa mipaka ya bahari na viwanja vya ndege kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza doria na ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika, hilo nalo limekubaliwa na Serikali italifanyia kazi. Tumekwisha ongeza midaki, yaani midaki ni scanner, kwa hiyo kiswahili cha scanner ni midaki. Midaki imeongezwa na tutafanya jambo hilo liwe la kudumu ili tuhakikishe jambo hilo...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, malizia.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, URATIBU NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limeelezwa na ningependa niliseme ni kwamba kwenye upande wa tathmini na ufuatiliaji tayari mwongozo unatayarishwa na ndani ya muda mfupi tutaanza mashauriano ya kuwa na mwongozo wa kitaifa wa tathmini na ufuatiliaji ili uweze kuongeza usimamizi katika Serikali.
Mheshimiwa Spika, mengine kama nilivyosema nitaomba suala lile ya UKIMWI na lile la watu wenye ulemavu tutahakikisha kwamba yote yanafanyiwa kazi na nitaomba mchango huu na majibu haya yawe sehemu ya Hansard yako ili Waheshimiwa Wabunge waweze kujua kwamba mambo haya yote tumeyafanyia kazi kama ambavyo umeelekeza.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/ 2027. (Makofi)