Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Prof. Riziki Silas Shemdoe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru kwa kunialika kuweza kuchangia hoja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kuchangia hotuba hii kwa unyenyekevu kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuwa hapa jioni ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona ninafaa kuongoza Wizara hii iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Makamu wa Rais kwa miongozo yake ambayo anatupatia, lakini vilevile nimpongeze sana, sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa mbayo anaifanya hapa Tanzania. Mheshimiwa Waziri Mkuu atakumbuka tulifika kule kwenye Jimbo la Lushoto na wale Wanalushoto wanafahamu na yeye anafahamu kwamba, cheni ichi alikisema kule Lushoto, ninamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nikupongeze wewe pamoja na viongozi wote wa Bunge ambao mnatuendeshea hili Bunge kisasa kabisa na tunaona hali ilivyo hapa. Hata hapa nilipo ninamwona Mheshimiwa Waziri Mkuu aki-concentrate kwenye hili tunalolifanya. Pia, ninachukua fursa hii kusimama mbele ya hili Bunge kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo ziko pamoja zimeletwa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya hapa niishukuru Kamati ya Bunge ya TAMISEMI inayoongozwa na Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge kwa maoni na ushauri bora kabisa ambao wametupatia. Ushauri wao unatuendeleza vizuri kuweza kutekeleza maelekezo na yote yaliyopo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi lakini kwenye Dira ya 2050. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru sana Manaibu Waziri, Dkt. Festo John Dugange na Mheshimiwa Dkt. Jafar Rajab Seif kwa kazi kubwa wanazozifanya. Pia, niwashukuru sana bwana Adolph Ndunguru, Katibu Mkuu; Manaibu Katibu Wakuu akiwepo Sospeter Mtwale; Eng. Rogatus Mativila; Prof. Tumaini Nagu; na bwana Atupele Mwambene; Wakuu wa Taasisi na Wakuu wa Idara kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI; na watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI kwa michango yao mikubwa wanayoitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ingawa siyo kwa umuhimu ninawashukuru sana Wakuu wa Mikoa; Makatibu Tawala wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; Makatibu Tawala wa Wilaya; Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Watumishi wote walioko kwenye hizi ofisi. Kwa sababu bila wao kazi kule chini zisingekuwa zinaweza kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru wananchi wa Lushoto kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao kwenye hili Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nichukue fursa hii kusimama mbele ya Bunge hili ili kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge. Tumepata michango ya Wabunge waliochangia TAMISEMI 120, ikiwepo michango 118 ya mazungumzo na michango miwili iliyoletwa kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hii michango yote tumezigawa hoja kwenye maeneo 14. Hoja ya kwanza ni Serikali kutakiwa kutenga fedha kwa ajili ukarabati wa shule chakavu nchini hususan kwenye Majimbo ya Hai, Temeke, Same, Bunda, Lushoto, Ludewa na sasa hivi tumesikia pia kutoka kwa Profesa Pius Yanda kule Buhigwe.

Mheshimiwa Spika, suala la shule chakavu siyo kwenye majimbo haya tuliyoyataja pekee yake. Suala hili ni kwenye majimbo yote ya Tanzania. Sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tumeanza mchakato wa kuandaa andiko la Mradi unaoitwa SIFA. Mradi huu kirefu chake ni School Infrastructure Faith Lifting Programs. Lengo lake ni kuhakikisha kwamba zile shule zote kongwe za awali za msingi na sekondari zinafanyiwa ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika imebaini ukarabati unahitajika kwenye shule za msingi ikihusisha vyumba vya madarasa 42,716 na nyumba za walimu 31,813. Aidha kwa upande wa shule za sekondari inajumuisha vyumba vya madarasa 6,889, nyumba za walimu 3,518, maktaba 91, pamoja na mabweni 309.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati kwa awamu ambapo kati ya mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2025/2026, Serikali imetumia shilingi bilioni 237.9 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya ya shule za msingi na sekondari kongwe, chakavu nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na timu yake kule Wizara ya Mipango kwa kulipokea hili andiko ambalo tumekuja nalo ili liweze kutafutiwa fedha na hatimaye tuanze ku-implement mradi huu wa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ilikuwa ni watu wenye ulemavu kutokufikiwa na mikopo ya 10% kwa madai ya kukosekana kwa vikundi vya watu wenye ulemavu. Suala hili tumelifanyia kazi kama Wizara na tumefika mahali ambapo tumekubali kwamba mtu mmoja, mmoja mwenye ulemavu anaweza kuruhusiwa kuchukua huu mkopo ili kuwapa room waweze kunufaika na hii mikopo. Kwa hiyo, suala hili limeendelea kufanyiwa kazi na lina solution yake ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya tatu ni matumizi ya teknolojia sahihi katika ujenzi wa barabara ili kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo husika. Katika kupunguza gharama za ujenzi na kuwa na barabara za wilaya za kutosha zinazopitika, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia TARURA imekuwa ikitumia teknolojia sahihi na nafuu tunazoziita appropriate technology katika ujenzi wa barabara. Matumizi haya yamewezesha kuboreshwa kwa barabara (roads improvements) na kuwezesha maeneo korofi ama bottlenecks kupitika.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya teknolojia sahihi ni pamoja na ujenzi wa madaraja ya mawe 501, barabara za mawe kilometa 30.03 na ujenzi wa barabara za zege kilometa 246.77. Kwenye maeneo yenye miinuko na yenye kutuamisha maji. Aidha, ili maeneo korofi kupitika kwa ujenzi wa bei nafuu mikanda ya zege sehemu yanapokanyaga matairi imejengwa katika sehemu mbalimbali nchini. Tuna mifano ambayo ni baadhi ya barabara zinazopita Mlima wa Livingstone Wilaya ya Mbinga, Wilaya ya Nyasa na Ludewa ili kuendelea kuhakikisha barabara zinapitika mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeendelea kuwaelekeza TARURA kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi huu wa concrete strips na pia watumie aina ya ujenzi kwenye maeneo muafaka ya vijijini ambako idadi ya magari ni chache. Matumizi ya teknolojia yataweza kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo husika, jambo ambalo kimsingi ni faida kwenye ujenzi lakini pia yatawanufaisha wananchi ambao wanakaa yale maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya nne ilikuwa ni Serikali kutoa fedha za dharura kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha. Bajeti ya TARURA imeendelea kuongezeka kama tulivyoona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tumetoka shilingi bilioni 944 hadi shilingi trilioni 1.21 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 sawa na ongezeko la 22%. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ongezeko hili ni jitihada za kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa wakati akizindua Bunge letu la Kumi na Tatu, tarehe 24 Novemba, 2025.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio haya ya kupata bajeti hii, Serikali imetumia fedha za dharura shilingi bilioni 21.4 kurekebisha miundombinu ya barabara ambazo zimeathiriwa na mvua kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Aidha, Serikali imefanya tathmini ya miundombinu iliyoharibiwa na mvua na tumepata kiasi cha shilingi bilioni 99.636 zinazohitajika kwa ajili ya kurekebisha hizi barabara ambazo zimekatika.

Mheshimiwa Spika, bajeti hii tumeendelea kukaa na wenzetu wa Wizara ya Mipango pamoja wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuhakikisha kwamba angalau ndani ya muda mfupi fedha hizi zinapatikana ili tuweze kwenda kukwamua hali iliyopo kwenye maeneo yetu, kwenye majimbo yetu.

Mheshimiwa Spika, hoja ya tano ni Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma ya elimu na afya kabla ya kuanza miradi mipya. Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati kwenye kata za kimkakati ambazo mwaka wa fedha 2024/2025 na mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali ilitoa shilingi bilioni 116.25 kwa ajili ya kujenga na kukamilisha vituo vya afya 202 na zahanati 426.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetoa shilingi bilioni 22.64 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 1,267 ya miundombinu ya shule za msingi na sekondari. Maboma 474 ya vyumba vya madarasa vya shule ya msingi, maboma 330 vyumba vya madarasa vya sekondari, mabweni 130 na maboma 333 ya vyumba vya madarasa. Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kukamilisha maboma katika vituo vya kutolea huduma za afya na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya sita ilikuwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zisimamie halmashauri zinazokusanya mapato ya ndani yanayozidi shilingi bilioni 10, waweke 10% kuzipeleka kwenye ujenzi wa barabara zao. Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeendelea kuzisimamia halmashauri zenye mapato makubwa kutenga 10% kwa ajili ya kuchangia utekelezaji wa miradi ya barabara. Katika mwaka wa fedha 2026/2027, shilingi bilioni 61.238 zimetengwa na halmashauri 16 zenye mapato yanayozidi shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Halmashauri hizo ni; Jiji la Dar es Salaam shilingi bilioni 14.5, Kinondoni Municipality shilingi bilioni 8.0, Dodoma Jiji shilingi bilioni 7.0, Arusha Jiji shilingi bilioni 7.0, Temeke Municipality shilingi bilioni 6.5, ubungo shilingi bilioni 3.2, Chalinze shilingi bilioni 2.225, Tunduma shilingi bilioni 1.8, Tanga shilingi bilioni 1.8, Mwanza shilingi bilioni 1.7, Mbeya shilingi 1.4, Kigamboni shilingi bilioni 1.3, Geita shilingi bilioni 1.2, Ilemela shilingi milioni 950, Morogoro Municipality shilingi milioni 840 na Mkuranga kwa ndugu yangu Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega shilingi milioni 800. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo halmashauri nyingine ambazo haziko kwenye kundi la kuchangia 70% kwenye miradi ya maendeleo kutoka kwenye mapato yao ya ndani. Halmashauri hizi pia tumezielekeza angalau zitenge kiasi cha fedha kwa ajili ya kwenda kurekebisha barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya saba ilikuwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ifanye tathmini ya Miradi ya TACTIC kwenye majiji na miji kujua kwa nini miradi inachelewa kukamilika na lini itakamilika? Utekelezaji wa Miradi ya TACTIC unatekelezwa kwenye miji 45, miradi hii imegawanyika katika makundi matatu; kundi la kwanza lina miji 12, kundi la pili lina miji 15 na kundi la tatu lina miji 18.

Mheshimiwa Spika, awamu za miji hiyo ni kama ifuatavyo: kundi la kwanza, lina Halmashauri za Majiji ya Arusha, Mwanza, Dodoma na Mbeya, Manispaa za Kigoma Ujiji, Ilemela, Geita, Morogoro, Songea, Sumbawanga, Tabora na Kahama.

Mheshimiwa Spika, kundi la pili, niJiji la Tanga, Manispaa za Mtwara, Bukoba, Iringa, Kibaha, Lindi, Moshi, Mpanda, Musoma, Singida, Shinyanga na Mji wa Babati, Bariadi, Korogwe na Njombe.

Mheshimiwa Spika, kundi la tatu, ni Miji ya Bunda, Handeni, Ifakara, Kasulu, Kondoa, Mafinga, Makambako, Masasi, Mbinga, Mbulu, Nanyamba, Newala, Nzega, Tarime, Tunduma, Bagamoyo na Wilaya za Chato na Mbozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maendeleo ya utekelezaji wa miradi hii iko katika hatua zifuatazo: moja kwenye miji 12 ya kwanza miradi ya barabara katika miji hiyo imekamilika na miradi isiyo ya barabara utekelezaji wake unaendelea na umefikia 98%.

Mheshimiwa Spika, miradi ya kundi la pili yenye miji 15, utekelezaji wake upo 30% na miradi ya kundi la tatu ambao utekelezaji wake haujaanza, lakini usanifu umekamilika na tuko tayari kwa kutangaza tender za zabuni ili kazi hizi ziweze kuanza. Aidha, Serikali itaendelea na usimamizi wa mradi huu hadi kukamilika kwake ili wananchi wapate manufaa yanayokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya nane, ni Serikali iweke mkakati wa matumizi ya fedha za bakaa ambazo zinatakiwa kutumika ndani ya miezi sita kwa mwaka mpya wa fedha ambapo matumizi ya fedha hizi hufanyika bila kuzingatia ubora wa miradi inayotekelezwa. Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba fedha za bakaa zinatumika kwa mujibu wa sheria ya bajeti sura ya 439 na kanuni zake, ambazo fedha hizo zinatakiwa zitumike ndani ya miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine tunaloweza kuulizwa kwa nini tunavuka na fedha nyingi, wakati mwingine za bakaa. Fedha hizi ziko kwenye miradi ambayo mingine imeletwa na wabia wa maendeleo kwa hiyo inapokuja ili tuweze kukamilisha ile miradi wakati mwingine inakuja kwa kuchelewa; kwa hiyo lazima tuvuke nazo kwenye mwaka unaofuata. Sisi kazi yetu kubwa kama Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kwamba, tunazingatia Sura ya 439 ya bajeti ambayo inatuelekeza kwamba fedha hizi zitumike ndani ya miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya tisa, imeitaka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuweka utaratibu wa kufanya ufuatiliaji katika halmashauri nchini ili kuona uhalisia wa fedha zinazopelekwa na zinavyotumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi ya wizara, mikoa, wilaya na halmashauri. Katika kutekeleza hili, Serikali imeboresha miundombinu kwa kuanzisha idara ya ufuatiliaji, usimamizi na ukaguzi, pamoja na vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika ngazi za mikoa na halmashauri ili kuviwezesha kwa kivipatia watumishi, rasilimali fedha na vitendea kazi ikiwemo magari kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inaendelea kuimarisha vitengo vya ukaguzi wa ndani, pamoja na kujenga mifumo ya TEHAMA ikiwepo Integrated Monitoring and Evaluation Systems (IMES), Mfumo wa Mpango na Bajeti tunaoita PlanRep na mifumo ya matumizi ngazi ya halmashauri na vituo vya kutolea huduma; ikiwemo mifumo ya TAUSI na FFARS.

Mheshimiwa Spika, hoja ya 10 ni Serikali iangalie utaratibu wa kutumia miundombinu ya ghorofa kwenye maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa ardhi. Serikali tayari imeanza utaratibu wa ujenzi wa miundombinu ya ghorofa katika maeneo yenye ufinyu wa ardhi ya miundombinu ya kutolea huduma za afya na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna mifano mizuri kwenye jiji la Dar es Salaam, lakini vilevile na manispaa zake kule Dar es Salaam, tumejenga shule za maghorofa kule, tumejenga vituo vya afya vya ghorofa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano wa maeneo yaliyoanza utekelezaji huo kama nilivyosema ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Manispaa za Temeke, Ubungo na Kinondoni pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tunduma, anapotokea Mheshimiwa David Ernest Silinde. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, kabla ya kuanza utekelezaji wa ujenzi huo, halmashauri zinatakiwa kuwasilisha michoro ili kupata idhini ya kuendelea na ujenzi. Kwa hivyo, halmashauri zenye uwezo wa kujenga majengo hayo, hata leo kama upo tayari zilete michoro hiyo na wenzetu hapa wizarani wataipitia michoro hiyo na kuhakikisha kwamba tunatoa vibali, majengo hayo yaendelee kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya kumi na moja, watumishi walipwe gharama za matibabu walizozitumia wanapowasilisha madai. Suala hili lilitolewa mfano kwa Mwalimu anaitwa Medrits Gabriel Bukala, ambaye alitumia kiasi cha shilingi milioni 41, lakini fedha hizi hatukufahamu kwamba amezitumia kwa sababu alikuwa hajaleta application za kwake za kuwa-refunded.

Mheshimiwa Spika, tumelichukua hili na tumeshapeleka Hazina kuomba refund ya mwalimu huyu aweze kurejeshewa gharama zake. Aidha gharama za usafiri wa kwenda na kurudi wa hospitali wa mtumishi huyo zililipwa na halmashauri wakati wa matibabu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya kumi na mbili, ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iharakishe ukamilishaji wa sera ya ukaguzi wa madaraka yaani D by D, ili kuzipa nguvu za utekelezaji mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ilifanya tathmini ya utekelezaji wa Tamko la Kisera ya Maboresho ya Serikali ya Mitaa ya Mwaka 1998. Tathmini hiyo ilipendekeza kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Ugatuzi, ambayo rasimu yake iko katika ngazi za maamuzi na mapendekezo ya rasimu ya sera hiyo, yamezingatia mahitaji ya sasa ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya kumi na tatu, ni kuhakikisha hakuna uchelewaji wa kutoa vibali ya matumizi ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa izisimamie Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa vibali za matumizi ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inaendelea kuzisimamia halmashauri kwa ajili ya kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati ikiwemo kutoa vibali vya matumizi ya fedha kwa haraka. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inaendelea kuboresha mifumo ya kieleketroniki ikiwemo; kupokea taarifa za miradi na mabadiliko ya vifungu vya matumizi ya fedha yaani reallocation kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na PPRA vilevile, Wizara imeendelea kutoa mafunzo ya mfumo wa NeST kwa watumiaji 9,678 walioko kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ikiwepo wakandarasi wa ndani. Wizara itaendelea kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi katika mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha hakuna ucheleweshaji wa utoaji wa vibali vya utekelezaji wa miradi katika ngazi za halmashauri na vituo vya kutolea huduma za afya na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya mwisho, hoja namba kumi na nne, ni kuitaka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuwaelekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kupanga ratiba ya vikao vya Kamati ya Fedha pamoja na Mabaraza ya Halmashauri kufanyika siku za Jumamosi au siku yenye nafasi watakayokubaliana na Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuwataka pia wakurugenzi kutoa taarifa za miradi ya maendeleo, taarifa ya fedha za miradi ya maendeleo inayokwenda kule kwenye halmashauri kwa Waheshimiwa Wabunge ambao ndiyo wanaohangaika kuzitafuta hizi fedha humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imekuwa ikisisitiza vikao vya Kamati za Fedha na Mabaraza kufanyika siku za Jumamosi au siku yenye nafasi kwa watakayokubaliana na Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ametoa maelekezo haya mara kwa mara, nami leo nisisitize kwamba, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu tutaendelea kuyafuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anipe kibali kwa wale ambao watakiuka maelekezo haya ambayo ameyatoa hapa Bungeni, basi tuweze kuchukua hatua za kinidhamu ama hatua za kiutumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo letu ni kama Mheshimiwa Raisi alivyotuelekeza kupeleka tabasamu kwa Watanzania na tutapeleka tabasamu hii kama wote tutashirikiana kuhakikisha kwamba tunatekeleza miradi ya maendeleo kwa kadri fedha zilivyotolewa hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, niwashukuru tena wananchi wa Jimbo la Lushoto, nimshukuru mke wangu mpendwa Bi. Rahel na watoto wangu Silas, Steve, Robinson, Rodney na Mjukuu wangu Willys. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimelileta hili pia ili kumwelekeza Mheshimiwa Baba Levo kwamba, huku Dodoma sina watoto. Watoto wangu na mke wangu wako pale Dar es Salaam na wengine wakiwa shule za boarding na kaka yao mkubwa na mke wake na mjukuu wako Arusha. Kwa hiyo, alichokisema Mheshimiwa Baba Levo amenitilia shoti kule nyumbani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, ninaomba kuuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)