Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Awali ya yote, ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili kuchangia hoja iliyo mbele yetu hoja ya Waziri Mkuu, kwa maana ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini, kuniteua na kunipa dhamana ya kuwa Waziri wa Nchi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Kazi, Ajira na Mahusino. Ninamwahidi Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi hii nitaifanya kwa uhodari mkubwa, umakini, weledi na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, nimpongeze sana Makamu wetu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miongozo mbalimbali ambayo amekuwa akitupatia, iliyotuwezesha kufanya majukumu yetu kwa ufanisi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee pia nimshukuru sana na kumpongeza Waziri wetu Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. Sisi ambao tunafanya kazi chini yake, tunajivunia kuwa na kiongozi hodari, mchapakazi, mzalendo na anayetanguliza maslahi ya Taifa mbele.

Mheshimiwa Spika, tukiwa chini yake tunajifunza mambo mengi. Kwanza, juhudi ya kufanya kazi bila kuchoka. Tumejifunza sasa hata kutokuzima simu usiku kwa sababu muda wowote Mheshimiwa Waziri Mkuu atakutafuta, atakupa maelekezo na kukupangia majukumu. Hii inaonesha namna alivyo na commitment ya hali ya juu katika kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wangu, kwa namna ambavyo ameendelea kunisaidia majukumu yangu ya kila siku na kufanya kazi yangu iwe rahisi; vilevile Katibu Mkuu wetu wa Wizara yetu iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Mary Maganga; Naibu Katibu Mkuu, Bi. Zuhura Yunus Abdallah na timu nzima ya wataalam ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee pia niendelee kuishukuru Kamati yetu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, chini ya Mwenyekiti wetu hodari na shupavu Mheshimiwa Hawa Chakoma Mchafu na Makamu wake Dkt. Regina Malima. Timu hii imekuwa nzuri, imekuwa ikitupa ushauri thabiti na kutufanya sisi kuweza kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi na kuleta ustawi wa jamii ya Watanzania. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee vile vile kuwashukuru sana kipekee wananchi wa Jimbo la Kwela kwa kuniamini kwa kipindi cha pili kuja ndani ya Bunge hili kuja kuwawakilisha. Niwaahidi wananchi wa Jimbo la Kwela commitment yangu katika kuwahudumia itakuwa ile ile. Nitafanya kazi kwa uaminifu bila kujibakiza kama ambavyo imekuwa desturi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bila kuwasahau wadau tunaofanya nao kazi, katika maana ya utatu, vyama vya wafanyakazi na chama cha waajiri, ninawashukuru. Tumekuwa tukishirikiana nao kwa ukaribu mzuri, wamekuwa ni wadau wakubwa wa kufanikisha jukumu hili, hasa katika eneo linalohusu wafanyakazi. Nami sina budi kuwashukuru na kuwapongeza kwa ushirikiano mkubwa ambao wanatupatia.
Mheshimiwa Spika, katika mjadala huu wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hoja nyingi zimetolewa. Nianze na hoja za Kamati. Kamati imetoa ushauri katika maeneo mbalimbali yaliyoelekea Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano. Ninaomba niwahakikishie Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati na Wajumbe wote wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Maoni, ushauri na mapendekezo yote waliyotupatia tutaenda kuyazingatia. Niwahakikishie kwamba, hakuna jambo lolote tutakaloacha bila kulipa umakini na kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningepitia jambo moja baada ya lingine, lakini kwa sababu ya muda itoshe kwamba nitatoa ufafanuzi kwa mambo machache ambayo yameelekezwa kwenye ofisi hii kwenye eneo la kazi, ajira na mahusiano.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wapatao 29 ambao walichangia hoja katika bajeti hii ya Kazi, Ajira na Mahusiano kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. Hoja zao tumezipokea na tutazifanyia kazi. Kwa wale ambao walileta hoja ya ufafanuzi mahususi niwaahidi, kwamba baada ya kukamilisha zoezi la kupitisha bajeti hii, nitaweza kutoa majibu kwa maandishi ili yale yanayohitaji majibu mahususi waweze kuyapata kwa ufanisi wake.

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya ya utangulizi nijielekeze kwenye hoja ambazo zimeletwa na Waheshimiwa Wabunge. Hoja kubwa ya kwanza ilikuwa ni juu ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwanza kwa kuruhusu Sera yetu ya Kinga ya Jamii kuzinduliwa mwezi Februari mwaka huu, ambayo hiyo inaenda kuweka mwelekeo wa Sekta yote ya Kinga ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuonesha utofauti wa kujali Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hadi anapoingia Mheshimiwa Rais nitaanza kuchambua Mfuko mmoja baada ya mwingine nikianza na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipokuwa anaingia madarakani alikuta Mfuko huu una thamani ya shilingi trilioni 4.36. Mpaka leo tunavyoongea Mfuko huu umekua na kufikia thamani ya trilioni 10.5; ni kazi kubwa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Mfuko unaohudumia Watumishi wa Sekta ya Umma (PSSSF), Mheshimiwa Rais alipokuwa anaingia madarakani alikuta Mfuko huu una thamani ya shilingi trilioni 5.74. Mpaka hivi ninavyoongea mbele ya Bunge lako, Mfuko huu na thamani ya shilingi trilioni 12.96. Mheshimiwa Rais ameonesha nia ya dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mabadiliko haya ya Mfuko yanatokana na nini? Katika Bunge la Kumi na Mbili tuliona Waheshimiwa Wabunge walipiga kelele kubwa juu ya madeni ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamiii na mmoja wapo alikuwa shemeji yangu pale Mheshimiwa Esther Bulaya. Hii inawezekana kuwa sababu iliyomfanya ahame kutoka upande huu asogee upande huu kwa sababu hii ilikuwa ni hoja yake mahususi aliyosimama nayo nyakati zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Deni la Serikali kwenye Mfuko wetu wa PSSSF lilikuwa ni shilingi trilioni 4.46. Mwaka wa fedha 2022/2023 Mheshimiwa Rais akatoa shilingi trilioni 2.1 kwenda kulipa deni katika Mfuko wetu wa PSSSF. Hakuishia hapo aliendelea kulipa deni kwenye huu Mfuko, juzi ame-commit fedha trilioni 2.09 ambayo itafanya thamani ya Serikali kulipa Mfuko huu wa PSSSF kufikia 95% ni jambo kubwa sana alilolifanya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa impact yake imekuwa ni nini? Mfuko umeimarika kwa maana ya ukwasi imepelekea sasa kuanza ulipaji wa mafao kwa sekta ya umma siku za ulipaji wa mafao zimepungua hadi kufikia siku 25. Ndani ya siku 25 mafao yanakuwa processed na wanachama wanalipwa mafao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ni la kujivunia sana kwa Mheshimiwa Rais. Wastaafu walikuwa wanalipwa shilingi 100,000 kima cha chini. Baada ya kuboresha na kulipa madeni haya, sasa kima cha chini cha wastaafu ni shilingi 250,000 ambalo ni sawa na ongezeko la 150%; haijawahi kutokea katika historia ya nchi hii. Hapa ndipo tunampa sifa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anapoweka fedha pia kwenye Mifuko hii Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo mahususi na kati ya maelekezo aliyoyatoa ni kuhakikisha fedha hizi zinawekeza katika maeneo yenye tija. Nitawapa mfano katika jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amekuja kuleta mtazamo na mwelekeo katika uwekezaji wa fedha zilizo kwenye Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamiii.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyoongea tuna habari ya Kiwanda chetu cha Mkulazi na Mheshimiwa Chief Whip Mheshimiwa Profesa Kabudi anatokea Kilosa na Mheshimiwa Dennis Londo watakuwa mashahidi. Kiwanda cha Mkulazi kilipigiwa kelele kwamba ni kiwanda ambacho ni mufilisi, kimeshindwa tulianzisha mradi ambao ni White Elephant.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais mwaka 2024 ameenda pale kufanya ziara. Tuna uwekezaji wa shilingi bilioni 354 ameenda kuelekeza kwamba kiwanda hiki kiweze kufufuka na kuweza kuanza kufanya kazi. Ninaomba niwape habari njema Waheshimiwa Wabunge, kiwanda kile sasa kimekuwa ni kimbilio, kiwanda kile kinaanza kuzalisha sukari ya kiwandani. Hiki kitakuwa ni kiwanda pekee Tanzania kinachozalisha industrial sugar na kinaenda kuondoa nakisi ya 20% katika uagizaji wa sukari ya viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Tunaenda kutunza fedha zetu za kigeni ambazo tungeenda kuagiza sukari ya viwandani 20% itatoka kwenye Kiwanda chetu cha Mkulazi, lakini wakulima (out growers) wanaozunguka kiwanda kile wamepata manufaa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo ni muhimu sana; ajira zaidi ya 11,000 zimepatikana ndani ya muda mfupi, lakini fedha zilizotumika kwa mwaka wa fedha 2024/2025, wakulima waliweza kuuza tani 37,981 kwa thamani ya shilingi bilioni 2.85. Mwaka huu wanaenda kununua miwa tani 53,128 kwa thamani ya shilingi bilioni 4.06. Wakulima wale walikuwa na deni kwenye Benki ya Azania ambalo deni la mwanzo principal amount ilikuwa shilingi bilioni 2.34, zili-accrue interest mpaka shilingi bilioni 5.7.

Mheshimiwa Spika, kupitia uwekezaji huu kwenye kiwanda tayari tumefanya mazungumzo na Benki ya Azania wananchi wa kule Kilosa ndani ya Jimbo la Mheshimiwa Profesa Kabudi wanaenda kutoka kwenye huo mzigo wa deni kwa sababu kiwanda katika mnyororo wa thamani wananufaika kupata hiyo fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda ninaomba niunge mkono hoja. Ahsante kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia katika hotuba hii. (Makofi)