Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Masasi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nami nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kudra zake na tumesimama hapa leo kuongea mbele ya Bunge lako hili Tukufu. Vilevile, ninaomba nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hii ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kutoa hoja yoyote na kuchangia, ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa nafasi zake mbili, kama Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na pili kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akiwa kama Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi alijipa heshima kubwa ya kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu uliopita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kinyang’anyiro hicho ninapenda kuwashukuru sana sana wananchi wa Jimbo langu la Masasi Mjini, ambao walikipa Chama Cha Mapinduzi ushindi mkubwa sana wa kiti cha urais, kiti cha Mbunge na vilevile viti vyote vya Madiwani katika Jimbo letu la Masasi Mjini.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine vilevile, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani yake kubwa kwangu kwa kunipa jukumu la kuiongoza Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ambayo inagusa hisia za kila Mtanzania kwa wakati huu. Ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba nitajitahidi kufanya kazi hizi kwa juhudi zote, kwa weledi wote na kumwomba Mwenyezi Mungu anisaidie ili niweze kutekeleza majukumu yale ambayo yanalengwa kwa Wizara yetu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Spika, ninapenda sasa nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri, ambayo imegusa maeneo mengi ya utekelezaji wa Serikali. Kwa upande wa Wizara yetu ya Ardhi, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelekeza masuala ambayo ni muhimu katika usimamizi wa sekta ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, la kwanza ni usimamizi wa upangaji na upimaji wa ardhi. Wote wanaelewa kwamba hili ndilo suluhu katika kuweka mipango ya ardhi iwe sawia ili kusiwe na migongano wala migogoro. Kwa hiyo, tumeshalichukua hilo na pia lipo katika mipango yetu ya kiwizara. Vilevile amezungumzia kuhusu uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA. Suala lingine aliongelea maboresho ya huduma za uthamini na ulipaji wa fidia, kuna utatuzi wa migogoro ya ardhi, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na uboreshaji wa miundombinu ya upimaji na ramani.
Mheshimiwa Spika, katika Bunge lako hili ninaahidi kwamba, Wizara itazingatia maelekezo haya yote yaliyotolewa katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuongeza tija, uwazi na kasi ya utoaji wa huduma za ardhi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na masuala ya ardhi yaliyoainishwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, zipo hoja mbalimbali ambazo ziliibuliwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakiwa wanachangia hotuba hii ya mjadala. Takribani ya Waheshimiwa Wabunge 10 tumewasikia wakiwa wanatoa hoja mbalimbali ambazo zinahusiana na mambo ya ardhi. Wametoa maoni na ushauri kuhusu hoja mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, moja kati ya mambo ambayo wameyazungumza Waheshimiwa Wabunge ni kuweka utaratibu madhubuti wa kutatua na kudhibiti migogoro na hususan ile inayohusu wakulima na wafugaji. Suala lingine walilolizungumzia ni kuhusu kuongeza kasi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi za vijiji, kwa kuamini kwamba mambo mengi sasa hivi yanatendeka huko vijijini kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni kurahisisha taratibu za upatikanaji wa hati miliki za ardhi. Jambo la nne ambalo wamelizungumza Waheshimiwa Wabunge wengi ni kuwezesha upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo kwa migogoro mingi hii ya ardhi ambayo inazungumzwa pande zote za nchi; Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba alitoa maelekezo kwa Wizara nne, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI; na Wizara ya Maliasili na Utalii; tukishirikiana pia na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, nitoe taarifa kwako kwamba tumeshaanza vikao vya maafisa ambao watajadili na kuchakata na kutoa maoni juu ya namna bora ya kusimamia ardhi ili kuondoa migogoro. Baada ya hapo watafika katika ngazi ya Waheshimiwa Mawaziri na baadaye tutatoa taarifa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ametoa maelekezo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutaendelea na mikakati yetu ya ndani ya kila siku ya kusimamia mambo yote yanayohusu ardhi. Kama tunavyofahamu, wizara inafanya mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kuendesha kliniki za ardhi ambazo ya mwisho kabisa tutaikumbuka kabisa ilikuwa inaitwa Samia Ardhi Kliniki ambayo ilikutana na watu takribani 13,000 wenye matatizo mbalimbali ya ardhi. Takribani 8,000 walisikilizwa na kutatuliwa matatizo yao. Tutaendelea na kliniki hizi kwa sababu ni moja kati ya mikakati ambayo imeonesha ufanisi mkubwa katika kutatua migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi. Kwanza kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Kuna mambo mengine ni kuhusu tu sheria, watu wanajua kwamba ardhi hii inamilikiwa na mtu Fulani, lakini wanaingia. Hiyo ni kutengeneza migogoro. Kwa hiyo, tutazidi kutoa elimu kwa wananchi wajue kwamba si vizuri kuingia katika eneo ambalo si lako na kuanza kuliendeleza.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuna migogoro mingi ambayo inatokana na vitendo hivyo vya wananchi wetu; wanaingia mpaka katika ardhi ambazo ni mali ya taasisi, tena za Serikali. Kule Mtwara nilifika mpaka nikasikia kwamba wameingia katika maeneo ya jeshi. Sasa mpaka mimi nikashangaa, mpaka eneo la jeshi linavamiwa na wananchi, lakini yote hayo ni kwa sababu ya kutozingatia sheria, taratibu na kanuni.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo tunaliangalia ni kuongeza kasi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi; tukijua kwamba hiyo nayo ni njia mojawapo ya kutatua migogoro. Vilevile, tutaendelea kutambua na kusajili nyanda za malisho kwa ajili ya kukabidhiana na changamoto ya mwingiliano baina ya watumiaji, hasa katika maeneo ya wakulima na wafugaji. Vilevile, kuna wawekezaji na kuna Hifadhi za Taifa. Tutaongeza kasi ya upangaji wa miji hii, maeneo haya ili kuondoa migogoro.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kusimamia kwa ukaribu taratibu za utwaaji wa ardhi kwa kuhakikisha kwamba wamiliki wa ardhi iliyotwaliwa wanalipwa fidia yao kwa haki, kwa ukamilifu na kwa wakati. Hapa niombe, taasisi zote ambazo zitaomba kutwaa ardhi mahali popote pale zijiandae, ziwe na fedha za malipo kwa wale wafidiwa. Kwa sababu, tutakapokuwa tumefanya upimaji na kufanya tathmini, wananchi wasichukue muda mrefu kabla ya kufanyiwa malipo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vijiji, Serikali inaendelea kutenga bajeti ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji ili kuondoa migongano ambayo nimeieleza hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka huu wa Fedha 2025/2026 ambao tunaumaliza tumeandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 253 na hivyo kuwa na jumla ya vijiji 4,925 ambavyo vimeandaliwa mipango yao ya matumizi ya ardhi. Mwaka huu wa fedha unaokuja, tumejipanga kuweka mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 426; na kwa hii tutakuwa tunaongeza idadi ile ambayo tunayo mpaka sasa hivi 4,925.
Mheshimiwa Spika, upimaji na uandaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ndilo suluhisho la migogoro yote ya wakulima na wafugaji, kwa sababu huwa inawahusisha wadau wote wa hilo eneo na kukubaliana nini kifanyike katika eneo lao na maeneo gani yawe ya mifugo, maeneo gani yawe ya wakulima.
Mheshimiwa Spika, katika kurahisiha upatikanaji wa hati miliki Wizara yetu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inajiingiza katika mifumo ya TEHAMA; na tunavyoongea mpaka sasa hivi, majiji yote nchini yanatumia mifumo ya TEHAMA katika mambo ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Tuna jumla ya halmashauri 48 ambazo nazo zimekwishaingizwa katika mfumo. Hapa niwaondolee wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, masuala ya kupata eneo moja kuwa na hati mbili hayatatokea tena kwa sababu mfumo utakataa kuweka jina la mtu mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maeneo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyajadili tutayatolea ufafanuzi wakati wizara yangu itakapokuwa inawasilisha bajeti yake mwezi Mei tarehe 28; lakini yote tumeyachukua na tunayazingatia.
Mheshimiwa Spika, kwa kufika hapo ninaomba niunge mkono hoja na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imetupa mwelekeo. Ahsante sana. (Makofi)