Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ambaye yupo safari kikazi Marekani, kuiwakilisha nchi kwenye Mkutano wa Idadi ya Watu na Maendeleo ya Nchi, ninaomba kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, niungane na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa neema na kibali cha kusimama mahali hapa leo kuchangia hotuba nzuri sana ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu iliyopo mezani. Pia nianze kwa kuwashukuru Wabunge wote waliochangia Wizara ya Afya wapatao Wabunge 26 na niwathibitishie kwamba hoja zao tumezipokea, ushauri wao tumeupokea na tutaufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, nitatoa maelekezo machache lakini majibu yao mengine yote watayapata tarehe 11 na tarehe 12, Mei Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anawasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Spika, niungane na Wabunge wenzangu waliompongeza Waziri Mkuu kwa kazi nzuri na kubwa aliyoifanya katika nchi hii. Nimebahatika kuambatana naye kwenye ziara mbalimbali ambazo Waziri Mkuu kwa ukweli zilikuwa ziara zenye tija sana. Sikusudii kurejea sifa nzuri na nyingi zilizotajwa, lakini nitaisema moja tu ya kujali watu. Kwenye ziara ya Waziri Mkuu tuliyoambatana naye, nilimwona akijali watu kwa kiasi cha hali ya juu sana. Aliwafuata watu waliokaa chini kwa maana ya watu wenye ulemavu na kuzungumza nao pale pale chini walipokaa ili kuwasikiliza vizuri.

Mheshimiwa Spika, hakuishia hapo tuliambatana mpaka kwenye hospitali kwenda kuwasikiliza wagonjwa yeye mwenyewe. Kule Lindi alifanya hivyo, Nachingwea alifanya hivyo na hakuishia hapo aliwasikiliza shida zao, lakini aliwapatia faraja ambayo ninaamini faraja ile waliyopewa na Waziri Mkuu itabaki kuwa alama kwenye maisha yao yote.

Mheshimiwa Spika, afya ni mtaji wa kila mtu, afya ni usalama wa nchi yetu na afya ni ustawi wa nchi yetu. Hapa kwa moyo wa dhati kabisa, nimpongeze Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa moyo wa dhati kabisa ameonesha kwa vitendo jinsi gani anathamini afya ya Watanzania na kwa vile Wabunge wengi walichangia kuhusu ubora wa afya inayotolewa katika nchi hii, kuhusu upatikanaji wa dawa, kuhusu sera na mambo mengine mengi. Ninaomba kwa heshima ya dhati kabisa niwaeleze Wabunge kuwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan alionesha passion yake ya kuipenda afya ya Watanzania pale mwaka 2019 alipokuwa Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Spika, aliposimama na kusema kwamba tujiongeze, tuwavushe salama, alikusudia tujiongeze na tuwavushe salama akina mama wa nchi hii wanaohangaika na afya zao na watoto wa nchi hii wanaohangaika na afya zao.

Mheshimiwa Spika, kwa nini alisimamia hapo? Afya na maendeleo ya nchi yoyote yanapimwa kwa afya ya mama na mtoto. Kwa hiyo, ikiwa kama key indicator ya kupima ubora wa afya basi mama na mtoto ni kigezo muhimu, alidhihirisha zaidi pale 2021 alipokuwa Rais wa Nchi hii, alipofanya maamuzi ya dhati kabisa ya kuendelea kuipandisha bajeti ya afya. Mwaka 2021 alianza na bajeti ya trilioni moja na hivi leo Wabunge ninavyowaeleza bajeti ya afya ni trilioni moja na pointi saba.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji huu aliouweka kwenye sekta ya afya ndiyo umefanya kuweza kujenga vituo vya afya katika nchi hii, kuweza kujenga zahanati katika nchi hii, kuweza kujenga hospitali za rufaa katika nchi hii, kuweza kuweka miundombinu bora na ya kisasa katika nchi hii na kipekee kuongeza bajeti ya dawa ambayo ni kilio cha Watanzania nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, ameongeza bajeti ya dawa kutoka bilioni mia mbili mwaka 2021, mpaka leo ninavyowaambia mwaka 2025/2026 bajeti ya dawa ni zaidi ya bilioni 398. Rais hakuishia hapo tu, amewekeza kwenye huduma bobezi katika nchi hii, huduma ambazo tulikuwa tunasafiri kwenda kuzifuata nje ya nchi, lakini sasa zinapatikana katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameendelea kuwekeza katika upandikizaji wa figo nchi, hospitali mbili sasa zinatoa, Benjamin Mkapa na Muhimbili, lakini wanapandikiza uroto kwa watoto wenye sickle cell. Tunapandikiza usikivu wa masikio kwa watoto wachanga wasiosikia, lakini tunapunguza uzito kwa kuweka puto kwa akina mama ili kupunguza uzito na hata akina baba pia.

Mheshimiwa Spika, tunaweka bone marrow au kupandikiza mfupa kwa watu wanaoathirika na kansa, yote hayo ni kuwafanya Watanzania wenye shida kubwa wapate huduma hizi katika nchi. Huko tunakokwenda tunatarajia hivi karibuni kuanza kupandikiza moyo na ini katika Hospitali yetu ya Muhimbili.

Mheshimiwa Spika, haikuwa kazi rahisi sana kupunguza vifo vya mama na mtoto, lakini Rais yeye mwenyewe alikwenda kwenye wodi ya akina mama na watoto wachanga Katavi, siyo jambo rahisi Rais kwenda wodini na kwenda kwenye wodi ya watoto, akina mama na watoto wachanga na tunalifahamu lile joto lililopo pale, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya vile.

Mheshimiwa Spika, alikuja na mikakati mingi ya pamoja ambayo imetufanya tuweze kufikia hapa, kuongeza vyumba vya kufanya operation ya kumtoa mtoto tumboni kutoka vyumba 390 mwaka 2021 hadi sasa tuna vyumba 580 nchi nzima. Alikuja na mpango maalum wa M-mama. M-mama ni nini? Ni usafiri wa jamii ambao unamfanya mama aweze kusafirishwa kwa haraka ili aweze kupata huduma ya kutolewa mtoto tumboni. Nchi nzima kila siku wapo wataalam wa afya ambao wanajadili vifo vya mama kila mkoa kuhakikisha kwamba hakuna vifo vinaendelea na mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni uwekezaji mkubwa ambao ninawathibitishia kwamba hata tunapokwenda kwenye vikao vya kimataifa, basi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa wa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na mambo hayo yote mazuri ndiyo maana akatunukiwa Goalkeeper Award na The Gates Foundation mwaka 2025; na mwaka huu tena, mwezi wa pili kwenye Mkutano wa Addis Ababa amepewa ukinara wa kupunguza vifo vya mama na mtoto Afrika nzima. Amepewa hivyo kwa sababu ya jitihada hizi chache nilizozitaja hapa ambazo amezifanya katika nchi hii, za kupunguza vifo vya mama na mtoto. Dkt. Samia Suluhu Hassan anastahili pongezi. Anatambulika nchini, anatambulika Afrika na kimataifa.

Mheshimiwa Spika, tuzo hii ya Gates Foundation aliyopewa ni ya kwanza kupewa Rais duniani; ni Rais wa kwanza Afrika kupewa tuzo hiyo; na ni Rais wa kwanza mwanamke kupewa tuzo hiyo. Kwa hiyo si tuzo ndogo, amefanya makubwa ndiyo maana amepewa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili tuseme Watanzania wanapata huduma bora ni lazima tupunguze mwendo wa wananchi kwenda kufuata huduma; na sera inasema tupunguze kwa umbali wa kilometa tano…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, malizia.

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, tumeendelea kuboresha hizi huduma na Watanzania wanapata huduma kwenye hizo kilometa tano.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kwamba, tunayo mapambano dhidi ya magonjwa sugu ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusu hilo; ambayo yanapelekea kupata huduma ya dialysis, ambayo imeonekana ni kero kubwa kwa Watanzania na Waheshimiwa Wabunge kwa niaba ya wananchi wamechangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba niwathibitishie, kwamba hadi sasa tuna vituo 75 nchi nzima vinavyotoa huduma hizo kwa kutumia mashine 759. Tumejipanga kuendelea kusambaza huduma hizo katika hospitali zote za rufaa. Ninaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kutuamini, tutatimiza.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, huduma ya bima ya afya kwa wote imeanza nchi nzima na kaya 276,000 zitaanza kwa awamu ya kwanza. Watendaji wapo uwandani kwa ajili ya kuendelea kuzitambua kaya ambazo hazina uwezo; kwa maana ya watoto, wajawazito, wazee na watu wenye ulemavu na kuendelea kutoa kadi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imekwishakutupatia bilioni 48 kwa ajili ya zoezi hili na tunakwenda kuanza kutoa huduma kwa kaya hizo. Hivyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, waendelee kutuunga mkono. Mengine mengi tutakuja kuyamalizia tarehe 11 na 12 tutakapokuwa tunaleta hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)