Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nianze kukushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji katika hotuba hii ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kabla sijaendelea, ninaomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo hotuba yake imeelezwa kwa kina na kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama kwenye Bunge hili. Ninasema wazi kuwa, katika muda huu mfupi Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. Ndiyo maana wananchi wote katika Nchi yetu ya Tanzania, kila mkoa na kila wilaya, hii leo wanatamani ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu; hata Jimboni kwangu Mkuranga watu wanatamani aje kesho. Hizi ziara zimeleta matokeo chanya, zimeleta msukumo na zimeamsha ari ya utendaji kazi ndani ya Serikali katika kuwahudumia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi na shukurani hizi kubwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninasema kwamba, tumechukua maoni ya Waheshimiwa Wabunge waliyoyatoa kuanzia tunaanza kazi ya kujadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ni ukweli ulio wazi kwamba, kama liko jambo limejadiliwa kwa kina sana kwenye hotuba hii basi ni miundombinu ya barabara na madaraja. Sisi vibarua, watenda kazi, tunaona kuwa tunao wajibu mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba, matamanio haya ya Waheshimiwa Wabunge, kwa niaba ya wananchi, tunayafanyia kazi usiku na mchana bila ya kuchoka, ili kuweza kupata matokeo chanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, kwa kuwa, tunayo Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, tumejipanga vyema kujibu hoja kwa hoja, zilizotolewa, kwa kuanzia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hata zile zitakazokuja wakati wa kuchangia Bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Ni ukweli ulio wazi kuwa, nchi yetu inajengwa na tunamshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakuna mahali utapita katika nchi yetu hii leo usikute miradi ya ujenzi, kila mahali panajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawahakikishia, liko jambo pia limezungumzwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge juu ya malipo ya wakandarasi, hususani wakandarasi wetu wa ndani. Jumla ya fedha shilingi 166,000,000,000 kuanzia mwezi Januari mpaka tarehe 15 leo zimelipwa kwa wakandarasi wetu wa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni msisitizo wa Mheshimiwa Rais ya kwamba wakati tunalipa madeni ya wakandarasi kipaumbele cha kwanza ni wakandarasi wa ndani. Tunafanya hivyo ili kuhakikisha kwamba, zile fedha tunazolipa zinabaki ndani ya nchi yetu na zinaendeleza mzunguko wa fedha na kwa hivyo, kuinua hali ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wako Wabunge pia, wamezungumza juu ya maandalizi yetu ya michuano mikubwa ya AFCON mwakani na wakapata wasiwasi juu ya namna ya miundombinu. Ninawahakikishia jambo hilo liko kwenye mikono salama na tunayo furaha kubwa; mfano, katika Mkoa wa Arusha kesho kutwa tunamwona kiongozi Mheshimiwa Waziri Mkuu akienda kuanzisha jambo la ujenzi wa Barabara kutoka Mbauda mpaka Losinyai inayoingia katika uwanja wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wa AFCON ulioko pale Arusha Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, jumla ya fedha shilingi 17,000,000,000 zimetolewa kama advance payment ya kwenda kumlipa mkandarasi CCEC. Tayari mkandarasi huyo amefanya mobilization na kesho kutwa ground inakwenda kuvunjwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuonesha namna ambavyo tumejipanga vyema, ikiwa ni pamoja na fidia ya Mradi wa Kilombero unaokwenda Airport ya Kisongo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumepanga Miji yetu ya Dar es Salaam na Mji wa Arusha kwenye jambo hili la AFCON, ukiachilia mbali ujenzi tu wa miundombinu, itapendeza sana. Tumetenga jumla ya fedha za Kitanzania shilingi 40,000,000,000 zitakazosambaza taa kila kona na kila barabara inayohudumia AFCON. Kwa hivyo, tuna uhakika kwamba, jambo letu hili litakwenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia ninasema tu kwamba, barabara ni kama mishipa ya damu katika mwili wa binadamu. Sisi tutaendeleza kazi kubwa na nzuri iliyoanza, msimamo wetu ni kwamba, miradi yote viporo hakuna utakaoachwa nyuma. Msimamo wetu wa pili ni, miradi yote iliyosainiwa, tutahakikisha kwamba, inapata advance payment na yote inakwenda kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, tunawashukuru sana kwa namna ambavyo wamechangia katika Bunge hili na kuonesha umuhimu mkubwa wa miundombinu ya Taifa letu. Tunawaahidi kwa mara nyingine tumechukua michango yote, tunakwenda kuifanyia kazi na tunakwenda kuijibu pia, wakati wa Hotuba ya Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)