Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Awali ya yote nichukue nafasi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uzima na afya na siku ya leo tunaenda kuhitimisha bajeti hii muhimu kabisa na hasa ukizingatia hotuba yake ilivyoshiba.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Miaka mitano tuliyoimaliza Mheshimiwa Rais ameonesha ni mlezi, ni mama. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya kutupatia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumshukuru Makamu wetu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Nchimbi, lakini pia tumshukuru kwa kazi kubwa anazozifanya Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. Tumeshuhudia kazi kubwa ambazo amezifanya katika baadhi ya majimbo alipopata nafasi ya kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninasimama hapa nikiwa nimejawa na moyo wa shukurani, lakini moyo ambao nimetumwa na wananchi wa Wilaya ya Hanang kuendelea kuishukuru Serikali, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Toka nchi yetu imekuwepo, Wilaya ya Hanang tulikuwa tuna vituo vitatu vya afya lakini baada ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani hakika muujiza umetokea tumepata vituo sita vipya vya afya lakini pia tumepata zahanati saba mpya. Hakika ahsante Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba upande wa afya, kazi hii kubwa na njema ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya kwenye jimbo langu, tunaomba sasa tukapate vifaatiba lakini na wauguzi ili kazi hii na majengo haya yaliyojengwa yaweze kutoa tija kwa wananchi kwa kuanza kuitoa huduma.

Mheshimiwa Spika, upande wa afya pamoja na kazi kubwa ambayo imeshafanyika, bado katika bajeti hii ninaomba, Mheshimiwa Rais amekuja kufanya mapinduzi makubwa ya afya katika Wilaya ya Hanang, lakini bado tuna upungufu katika kata 27. Tunaendelea kumwombea afya njema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na katika bajeti hii tuendelee kuliona tabasamu ambalo mama anahitaji Wanahanang waendelee kulipata kwa kuongezewa vituo vya afya pamoja na ujenzi wa zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuletea neema na baraka ya mvua katika nchi yetu. Mvua zimekuwa za kutosha na zimeweza kufanya uharibifu kwenye barabara. Siyo laana kwa sababu pia tunaenda kupata mazao. Sasa ni wakati wa kuipitisha bajeti hapa ili kuweza kwenda kuijenga miundombinu; mazao ambayo wananchi wetu wamelima yawe na tija. Magari yanayoingia yachukue mizigo kwa bei nafuu na kusaidia urahisi wa maisha kwa wafanyabiashara lakini pia kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachukua nafasi hii kuomba sana barabara, nikianza na TANROADS. Ninaomba bajeti isukumwe TANROADS, ili kuweza kujenga na kufanya ukarabati kwenye barabara zinazounganisha mkoa na mkoa na kuhakikisha ule uharibifu uliotokana na mvua, unarekebishwa ili kurejesha barabara hizo. Ninaomba sana kipande cha Barabara kutoka Dareda mpaka Gehandu katika Jimbo la Hanang, chenye urefu wa kilometa 80, twende tukafanye ukarabati huu kwa sababu, barabara hii ni kiunganishi cha nchi yetu kwa kuunganisha mkoa kwa mkoa na ni kiunganishi cha nchi nyingine za jirani.

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kujielekeza katika TARURA. Uharibifu ni kweli umefanyika katika mtandao wa barabara katika Wilaya ya Hanang wa jumla ya kilometa 1050.5. Nimepitishiwa bajeti ya shilingi bilioni 2.3, ili iweze kwenda kujenga kilometa 62 za Barabara. Tunaishukuru sana Serikali, lakini tunaomba bajeti hii iongezwe kwa sababu, Wilaya ya Hanang ina mtandao mkubwa wa barabara, kilometa ni nyingi, shilingi 2,000,000,000. Ninaomba niongezwe fedha, ili tuongeze kiwango cha barabara kwa sababu, kwa kujenga kilometa hizi 62 tutachukua miaka mingi, ili kukamilisha mtandao wa kilometa 1,050. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda ninaendelea kuishukuru sana Serikali na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake mema kwa vijana wa Tanzania, akina mama wa Tanzania, Wazee wa Tanzania na wananchi wa Tanzania. Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya shilingi 200,000,000,000 kwa ajili ya kuwasaidia. Mheshimiwa Rais anaendelea kuzigawa fedha hizi ziweze kutoa fursa pana ya ajira kwa vijana wajasiriamali akina mama na akina baba na iweze kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba nitoe ushauri wangu hapa. Tuna Mifuko zaidi ya 72 ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, Mifuko hii ni mingi sana, tunaomba ipunguzwe, ili wananchi hawa wajasiriamali wadogo na vikundi maalum viwe na madirisha machache ya kujua wapi wanapata mkopo. Ninaomba Mifuko hii ipunguzwe.

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kuipongeza dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha taasisi zote zilizopo chini ya Serikali zinatenga 30% kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Ikiwezekana taasisi hizi za Serikali, kupitia hizi 30%, ziwe zina Mfuko mmoja wa Kitaifa ambao utakusanya na kugawanywa na chombo kimoja, ili sasa ule uwezeshaji wa wananchi kiuchumi uwe na tija.

Mheshimiwa Spika, ninafahamu zipo Wizara mbalimbali hapa tutapitisha bajeti. Hatuna hofu na kuipitisha bajeti ya nchi hii kwa sababu, Mheshimiwa Rais miaka mitano iliyopita amefanya kazi kwa vitendo, kazi yetu ni moja, kupitisha bajeti ili twende tukaitekeleze Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, ninakushuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Asia, ahsante, lakini hujaunga mkono hoja.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)