Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Latifa Khamis Juwakali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa kibali na neema ya uhai. Vilevile, kwa dhati ya moyo wangu ninaomba nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya kwa wananchi wake wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Makamu wa Rais, pia ninampongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Lameck Nchemba kwa kazi nzuri na kubwa anayoendelea kuifanya. Hotuba hii ya Waziri Mkuu ni hotuba inayolenga kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi wa Tanzania hasa vijana, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda ninaomba nijielekeze katika maeneo makuu matatu. Eneo la kwanza nitachangia katika 10% za mapato ya halmashauri; eneo la pili nitachangia katika Wizara ya Ajira, Kazi na Mahusiano; na eneo langu la tatu nitachangia kuhusu Mifuko ya Uwezeshaji Kiuchumi ambayo inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alileta mapendekezo na kufanywa maboresho makubwa kwa hizi 10% ambazo zinatolewa katika halmashauri. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu mpaka kuleta mapendekezo yale kulikuwa kuna changamoto ambazo zinajitokeza katika halmashauri.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi lengo lake ni kuwawezesha na kuwasaidia vijana wa nchi hii, akina mama na watu wenye ulemavu. Kwa vile mimi ni Mbunge ninayewakilisha kundi la vijana, ninaomba ni focus zaidi kwenye hii asilimia nne ya vijana. Niungane na Wabunge wenzangu waliyochangia hapa wamezungumza kwa moyo mkunjufu lakini wamezungumza ili kuweza kuwasaidia akina mama, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia asilimia nne za vijana kwenye halmashauri, hizi fedha zinatengwa na bahati nzuri kila mwaka zinatengwa. Unatenga fedha, lakini kwenye hizi fedha nani ambaye ni coordinator? Nani ambaye anazisimamia? Ipo haja sasa, tunapozungumzia rasilimali watu ni pamoja na watumishi.

Mheshimiwa Spika, utaungana na mimi na Wabunge wataungana na mimi; hakuna watumishi (Afisa Maendeleo na Afisa Vijana) katika halmashauri. Katika halmashauri utakuta kuna Afisa Maendeleo, huyo anashughulikia kila kitu, lakini kinachoshangaza utakuta mratibu na msimamizi wa masuala ya Misitu, Afisa Nyuki, wapo katika halmashauri lakini kwenye kundi hili kubwa la vijana kukosekana kwa watumishi, hili jambo kwa kweli linatukosesha amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeamua sasa kufanya maboresho na marekebisho, ni wakati sasa umefika wa kutenga bajeti maalum ya kuwaajiri watumishi hawa ili waweze kwenda kuwasaidia vijana. Sote tunafahamu chuo chetu kile cha Mzumbe Dar es Salaam sasa hivi tunao graduate, mwaka wa pili huu wame-graduate: vijana mbalimbali wenye ujuzi, wenye taaluma ambao wana uwezo na wamefunzwa vizuri masuala ya vijana, tuwaajiri ili waweze kuwasaidia vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na hivyo, vijana hawa tutakaoenda kuwaajiri lazima tuwatazame vijana ambao wanaendana na kasi na teknolojia ya nchi yetu. Haiwezekani unaenda kumwajiri Afisa Maendeleo hata kutumia WhatsApp hawezi, kijana akienda pale anataka karatasi yake aitume kwenye WhatsApp hawezi, yaani yupo nyuma. Ninaomba sana na hili tulizingatie.

Mheshimiwa Spika, ninajielekeza katika Wizara ya Ajira, Kazi na Mahusiano. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuianzisha Wizara hii. Tunapoizungumzia Wizara hii ya Mahusiano ni Wizara nyeti na muhimu sana kwa maslahi ya vijana wa nchi hii. Utakapoyaweka vizuri mahusiano maana yake umetengeneza ajira; utakapoyaweka vizuri mahusiano maana yake umetengeneza kazi kwa vijana.

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wetu, tujitahidi sana, tuanzishe mahusiano mazuri katika sekta binafsi, lakini pia tuanzishe mahusiano mazuri katika maeneo hata ya nje ya nchi. Sisi tunatembea sana, huko maeneo mengine tunapokwenda unashangaa unatua pale Dubai unawakuta vijana mbalimbali wameajiriwa, lakini wa nchi nyingine siyo wa nchi za pale, lakini wale unawaona kwa sababu wapo very creative lakini very coordinated na waliowa-coordinate ni nani, viongozi wao. Tunaomba sana na sisi vijana wetu zinapotokea fursa kama hizi tuwasaidie, tuwaelekeze na tuwa- coordinate. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana, Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja hapa ku-wind up, atusaidie sana kutueleza Wizara hii imejiandaa vipi na imejipanga ....

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Juwakali, ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)