Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Prof. Pius Zebhe Yanda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. PIUS Z. YANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote, ninaomba kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kufika siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba pia nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nia njema na juhudi za kuwezesha maendeleo ya Watanzania. Hilo limeonekana wazi hata kwenye kipindi cha kwanza cha Awamu ya Sita ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Makubwa yamefanyika karibu nchi nzima, ushahidi tosha ni katika Wilaya yetu ya Buhigwe, kwa uchanga wake tulifanikiwa kupata uwezeshaji wa ujenzi wa shule, vituo vya afya, hospitali, barabara na kadhalika. Kilimo hakikuachwa nyuma; kulikuwa na uwezeshaji mkubwa sana katika sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. Tumeshuhudia wakati wa ziara yake ameweza kutatua changamoto za Watanzania na kwa kweli hiyo ni ishara ya upendo wa makusudi kuhakikisha kwamba anajaribu kuleta furaha kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme pia kwamba, kwenye mkoa wangu na wilaya yangu ninaomba nitambue kazi kubwa wanayofanya viongozi wangu; Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wangu kwa usimamizi makini wa miradi ya maendeleo mkoani na wilayani Buhigwe.

Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba nirejee kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ukweli uliopo wazi ni kwamba ile hotuba ya bajeti imeakisi Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano lakini Dira ya 2050. Hilo ni jambo jema kwa sababu tuweze kutambua tu kwamba ile dira imetengenezwa na Watanzania. Watanzania walisema Tanzania waitakayo 2050 inahitaji izingatie yafuatayo na kwa hiyo basi tunaliona wazi kwamba mipango yote ya maendeleo inatembea kwenye Dira ya 2050. Hilo kwa kweli ni jambo linahitaji pongezi kwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajitahidi kutorudia yale ambayo yameshasemwa na waliyochangia awali, lakini ninaomba nianze na sekta ya elimu. Tumeona kwenye sekta ya elimu kumekuwa na uwezeshaji mkubwa wa ujenzi wa majengo, madarasa, kadhalika na nyumba za walimu. Kilicho wazi kwenye bajeti hii ambayo tunajua wazi kwamba ni kwa sababu pia ya ufinyu wa bajeti, kipaumbele kinawekwa kwenda kumalizia yale maboma ambayo yapo.

Mheshimiwa Spika, tuwe wakweli pia kwamba, madarasa yaliyopo yaliyojengwa miaka ya 1970 yapo kwenye hali mbaya sana. Ninaogopa kwamba tunaweza tukafika mahali baadhi ya madarasa tukaya-condemn kwamba hayafai kwa matumizi ya watoto wa shule.

Mheshimiwa Spika, sasa ninalileta hili kwamba katika mikakati yetu ya kukamilisha yale maboma yaliyopo, tuweze kufikiria pia ukarabati wa yale madarasa yaliyopo ili tuwezeshe watoto waweze kusoma katika mazingira rafiki. Kwa maeneo yenye mvua nyingi kama kanda za mashariki, wakati wa masika na upepo mkali, watoto hawawezi kusoma kwenye madarasa hayo. Sasa ninafikiri ni muhimu sana tuweze kuangalia ni jinsi gani tunaweza kuboresha hilo.

Mheshimiwa Spika, tukirejea kwenye nyumba za walimu na madaktari; tunashukuru kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewezesha kuweza kuajiri madaktari wa kutosha na walimu wa kutosha, lakini ukweli ni kwamba nyumba ni changamoto sana. Sasa pendekezo langu ni hivi, kuna baadhi ya maeneo ambapo angalau kuna possibility ya hao madaktari na walimu kuweza kupanga nyumba, lakini kuna mazingira mengine ambayo siyo rafiki kabisa kupata nyumba za kupanga, matokeo yake wanabadilisha baadhi ya madarasa yanakuwa ndiyo nyumba zao za kuishi. Kwa hiyo, maeneo kama hayo yapewe kipaumbele ili kuwezesha kujenga nyumba za walimu na madaktari waweze kuishi katika mazingira rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukirudi kwenye upande wa afya ni kwamba kuna baadhi ya zahanati ambazo kwa kweli zimechoka na kadhalika, kwa zile halmashauri ambazo hazipati kipato kikubwa inaweza ikawa changamoto kukarabati hizo zahanati kwa kipato chao kinachopatikana kwenye halmashauri. Kwa hiyo, hilo ni jambo lingine ambalo linahitaji kuangaliwa kwenye jicho la pekee.

Mheshimiwa Spika, tukienda kwenye upande wa barabara, ni kweli barabara zimeharibika sana hasa zile za vijijini na tujue kwamba kule ndipo wakulima wanalima mazao na ili waweze kupata kipato lazima wapeleke sokoni, lakini barabara zikiwa ni mbovu kwa kweli uwezekano wa kufikisha hayo mazao sokoni ni shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukirudi kwenye maji kadhalika, makubwa yamefanyika katika miradi ya maji, lakini bado ile miradi skimu za zamani; nyingine zimefika mahali ambapo ni sawa na kama hazifanyi kazi. Sasa hapo pia tuangalie, tufanye tathmini na zile ambazo tunasema ni critical cases basi ziwe treated sambamba na ukamilishaji wa ile miradi ambayo haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, tukirudi ningependa nizungumzie...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Yanda, muda wako umekwisha, ninakushukuru kwa mchango mzuri.

MHE. PIUS Z. YANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)