Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nami ninaungana na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazoendelea kufanya katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi ambazo anaendelea kufanya katika Taifa letu kama ambavyo Mheshimiwa Rais amemwamini. Ninawapongeza sana sana wasaidizi wake kwa maana ya Mawaziri ambao wako chini ya Wizara yake kwa kazi kubwa ambazo wanaendelea kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kama mawili hivi. Jambo la kwanza, Waheshimiwa Wabunge wamesema sana juu ya barabara. Nami ninaomba nijikite hapo juu ya barabara. Barabara kwa kweli zimeharibika, lazima tuwe na mpango wa kuhakikisha kwamba tunarekebisha barabara zetu katika maeneo yetu kwa sababu zimeharibiwa sana na mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikiliza jana Baba Levo akizungumza. Kuna baadhi ya maeneo mvua zinaharibu kwa sababu ya kutokuwa na mitaro. Busega tunalo jambo kubwa ambalo tumekuwa tukiomba fedha Serikalini kwa ajili ya mitaro ya Mji wetu wa Lamadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Lamadi ni Mji mkubwa katika Jimbo la Busega, lakini bado hatujawekeza katika mitaro ya barabara na ndiyo maana barabara zinaharibika kila mara kwenye Mji wetu wa Lamadi. Tumeomba fedha, sasa ni wakati sahihi wa kupatiwa fedha ili tuweze kurekebisha Mji wa Lamadi ikiwa ni pamoja na kutengeneza mitaro ili kuzinusuru barabara za Mji wa Lamadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninafanya utafiti, tunapitisha bajeti kwa ajili ya barabara, lakini pia tuna vyanzo kwa ajili ya miradi ya barabara. Tuna Mfuko wa Barabara na tumekuwa tukikusanya fedha kwa ajili ya barabara. Haya ambayo yanasemwa na Waheshimiwa Wabunge juu ya barabara, mojawapo ni kwa sababu ya Mfuko wa Barabara haujapelekewa fedha ikilinganishwa na makusanyo yanavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano mdogo. Ukiangalia TRA katika tozo ambayo tumeweka kwa ajili ya Mfuko wa Barabara, mpaka mwezi wa Pili mwaka huu wamekusanya takribani shilingi bilioni 800, lakini zilizoenda kwenye taasisi yetu ya Mfuko wa Barabara ni takribani shilingi bilioni 200, sawa na 25%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kusema barabara zimeharibika kwa sababu hatujapeleka fedha kwenye Mfuko wa Barabara, ili Mfuko wa Barabara na wao wapeleke fedha TANROADS 70% na kule TARURA 30%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwekeze, na Mheshimiwa Waziri Mkuu nilimsikiliza alisema sasa fedha hizi ziende moja kwa moja kwenye mifuko inayohusika. Mheshimiwa Waziri Mkuu shikilia hapo hapo fedha ziende, na ikibidi kwa muda ambao umebaki wa kutoka sasa mpaka mwezi wa sita, zile fedha ambazo zimekusanywa kwa ajili ya Mfuko wa Barabara takribani zaidi ya shilingi bilioni 600 ambazo hazijaenda, ziende kwenda kurekebisha barabara katika majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia TARURA, bajeti tuliyowapitishia ni shilingi bilioni 957, fedha zilizoenda 40% sawa na shilingi bilioni 380. Tutafika kwa style ipi? Ili barabara zetu ziendelee kuimarika, lazima tupeleke fedha kama ambavyo tumewapitishia. Tukipeleka fedha TARURA, tukipeleka fedha TANROAD, tukipeleka fedha kwenye mifuko ambayo ina vyanzo vyake, ni hakika barabara zetu zitaenda kuimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kuwa kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kuhakikisha kwamba fedha zinavyokusanywa ziende moja kwa moja, zikienda kama ambavyo Waziri Mkuu amesema hapa Bungeni, ni imani yangu kwamba barabara zetu zinaenda kuimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, wakulima wa zao la pamba hasa wa Mkoa wa Simiyu wamenituma. Uzalishaji wa pamba katika Taifa letu ni takribani 51% ya pamba inayozalishwa inatoka katika Mkoa wa Simiyu. Hata hivyo, kuna jambo ambalo linaendelea sasa na ninamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aingilie kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo linaitwa, kuna watu wanaitwa wawekezaji. Mimi sina tatizo na wawekezaji, tatizo langu ni modality ya hawa wawekezaji wanapowekeza kwenye maeneo husika. Wanapokuwa wamewekeza kwenye zao la pamba, sharti lao mojawapo ni kuhakikisha kwamba mwananchi atakapovuna pamba yake amuuzie mtu mmoja ambaye amewekeza kwenye eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuko huko sasa hivi? Tulishahama kwenye mambo ya monopoly muda mrefu. Tulishahama mambo ya mnunuzi mmoja kwenye sekta ya pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba suala hili la pamba aingilie kati. Wananchi ambao wanazalisha pamba hasa Mkoa wa Simiyu, wamekuwa wakinyanyasika na bei ya pamba kwa sababu ya mnunuzi mmoja anaenda kununua kwenye sehemu hiyo, ananunua peke yake. Maana yake kama kuna ushindani, yeye mwananchi hauoni kwa sababu mnunuzi wa pamba ni mmoja, na ndio anapanga bei. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya maeneo unaona sehemu ambayo mwekezaji amewekeza kwenye kata husika, bei elekezi ni labda ni shilingi 1,250, lakini hapa katikati bei ya pamba inakuja kupanda inakuwa hata shilingi 1,300, au shilingi 1,400. Huyu anasema aah aah, kwa sababu mimi hapa niliwekeza, ninaendelea kununua kwa shilingi 1,250, na mwananchi wa kawaida ambaye ameteseka kwa takribani miezi mitano akilima zao la pamba hanufaiki na kuiona thamani ya zao la pamba kwa sababu ya bei ya mnunuzi mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakulima kawaida yetu kama hakuna ushindani, hata kama bei itakuwa shilingi 10,000 kama sijaona ushindani, siwezi kuamini kama hiyo bei ni halali. Ili bei niiamini kwamba ni halali, lazima nione ushindani. Mheshimiwa Prof Shemdoe ananunua kilo kwa shilingi 1,200 na Mheshimiwa Prof. Kabudi shilingi 1,200, na Mheshimiwa Hasunga hapa shilingi 1,200, hapo ndipo nita-justify kwamba bei ya pamba ni shilingi 1,200; lakini kama ananunua mmoja, Mheshimiwa Songe, peke yake shilingi 1,200, nitakuwa na mind kichwani mwangu kwamba inawezekana bei ni shilingi 1,500. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili suala hili lifanyike vizuri zaidi, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu angilie eneo hili la uzalishaji wa pamba kwa wananchi wetu. Tunatamani wananchi wetu wanufaike na zao la pamba ikiwa ni pamoja na Soko Huria kwa wananchi wetu, ili mwananchi aamue anaenda kuuza kwa nani? Anaenda kuuza kwa yupi ili nufaike na kile kilimo ambacho anakusudia? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuona umewasha mic, nami ninaungana na wenzangu kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)