Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Mgore Miraji Kigera

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MGORE M. KIGERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi. Kwanza kabisa, ninaomba nitoe shukrani za dhati kwa Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha siku hii ya leo kusimama hapa nikiwawakilisha wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nitoe pongezi za dhati kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo ameweza kuzifanya katika Jimbo la Musoma Mjini na hapa ninampongeza pia kwa kuwathamini Watanzania na kuamua kumteua na kumpendekeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa sababu amemleta katika wakati sahihi ambao Watanzania wamekuwa wakihitaji matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wetu kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa siku ya tarehe 01Aprili, 2026, hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2026/2027. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Watu wana msemo wanasema: “Full package.” Hapa tunayo, full package ya Watanzania ambaye ni Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa sababu ukiangalia hotuba yake inaonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Tanzania Unaona na kutatua changamoto na kero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameweza kuzunguka mikoa mingi sana. Hapa ninamwomba, hii neema aliyopitanayo kwenye mikoa mingine na majimbo mengine, wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini wanamsubiria kwa hamu sana ili ile mifupa migumu yote aweze kuitafuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijikite moja kwa moja kwenye uchangiaji ambapo nitagusia Dira 2050. Dira inaelezea kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi wa Tanzania. Nami kama Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini ninaongelea suala zima la uchumi wa eneo langu. Musoma Mjini tulikuwa na bandari ambapo Meli ya MV Umoja ilikuwa ikifanya safari zake. Ni takribani miaka 20 bandari hiyo haifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapenda kumshukuru Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa. Aliweza kufunga safari na kufika Jimbo la Musoma Mjini na akashuhudia Bandari ile ni bandari inayohitaji marekebisho kidogo ili iweze kufanya kazi. Itakapofanya kazi itaenda kufungua fursa za uchumi na kuchochea ajira kwa wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo meli yetu ya MV. New Mwanza. Ninampongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 120 na kujenga meli ambayo ndiyo kubwa katika Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tunatarajia wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini na wenyewe waweze kunufaika na mradi huu wa hii meli, kwani sisi Musoma Mjini na Mkoa wa Mara tumepakana na nchi mbili ambayo ni Kenya pamoja na Uganda. Meli hiyo ikianza safari ya kupita Musoma ikaenda Kisumu pamoja na Jinja, itachochea uchumi wa Musoma Mjini, Mkoa wa Mara na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende moja kwa moja kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Ninampongeza Mheshimiwa Prof. Shemdoe kaka yangu, anafanya kazi nzuri na kubwa kupitia TARURA. Hapa TARURA tuendelee kuwapongeza, lakini ninaomba nitoe ushauri kwa Waziri wa TAMISEMI kupitia TARURA. TARURA wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kufungua barabara zetu, na hapa watu wanaongelea kuhusiana na bajeti. Kila Mbunge amesimama anaongelea kuhusu barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali kupitia TARURA, tufanye kazi ya kutengeneza mitaro ambayo itakuwa ni protection ya barabara zetu instead ya kufanya reformation mara kwa mara. Kwa kuwa barabara zinaharibika kutokana na kutokuwa na protection za maji pamoja na kuwa na structures, tukijenga mitaro ya kutosha, tukajenga ma-culvert na madaraja, hata mvua ikija tutaweza ku-protect barabara zetu na wananchi wetu wataweza kunufaika na mradi huu ambao umekuwa ukiletewa fedha nyingi sana na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye sekta hii ya barabara, ninaendelea kuwashukuru Wizara ya TAMISEMI kwa mradi wa TACTIC ambao uliletwa katika Jimbo la Musoma Mjini. Barabara ya Kutoka Musoma Bus – Kwangwa ilikuwa ni changamoto kubwa sana na sasa hivi tunaye mkandarasi kwa mradi wa shilingi bilioni 19.9 ambazo zimeletwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mkandarasi huyo yuko site na ameshapokea shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kuendelea na mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya, kwani kupitia Wizara yetu ya Uchukuzi hiyo hiyo pamoja na Sekta ya Utalii wameweza kufanya vizuri sana. Tukiongelea uchumi katika Jimbo la Musoma Mjini, sisi tuna takribani kilometa 130 kufika Mbuga ya Wanyama Serengeti. Mbuga ya Wanyama Serengeti ndiyo mbuga bora na inayofanya vizuri duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, imeonesha ni namna gani Sekta ya Utalii imeongezeka na kufanya vizuri kwa 10.73%. Ninaiomba Serikali yangu sikivu iweze kufikiria iweze kutengeneza Marine Parks katika Jimbo na Musoma Mjini, kwani sisi tuko kando kando ya ziwa. Kwenye fukwe zetu tukiwa na Marine Parks, itasaidia utalii kukua, na fursa za ajira zitaongezeka kwa wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini na uchumi utaendelea kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Afya, nimeona hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia Bima za Afya kwa Wote, tunawashukuru wananchi wa Musoma Mjini kaya 501 kati ya Kaya 663 wamenufaika na Bima za Afya kwa Wote. Hapo Ninaendelea kuishukuru Serikali na Mheshimiwa Rais, katika Kada ya Afya wafanyakazi 5,000 walioajiriwa, Musoma Mjini tumenufaika na wafanyakazi 68.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali yangu sikivu, hili jambo nimeshalifikisha kwa Waziri wa TAMISEMI na hapa ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kuangalia. Tuna Kituo kikongwe cha Afya cha Bweri. Kituo hiki kimejengwa toka mwaka 1970. Kituo hiki ni chakavu sana na kinaleta athari kwa wananchi wetu. Ni kituo ambacho kipo katika kata yenye wakazi 22,987, ni wakazi wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali iweze kutufanyia maboresho ya kituo hicho ili wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini hasa Kata ya Bweri waweze kunufaika na huduma bora za afya ... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, kengele ya pili.

MHE. MGORE M. KIGERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)