Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Sylivia Francis Sigula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia katika Hotuba iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waswahili wanasema, ”Moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema yote.” Ninamshukuru Mungu sana kwa kunipa kibali, kwa kunipa afya njema, kunipa zawadi ya uhai na kunipa kibali cha kurejea tena katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kurejea kwa mara ya pili haikuwa rahisi, lakini Mungu alikuwa upande wangu. Ninamshukuru sana Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo, ninakishukuru Chama changu Cha Mapinduzi. Hapa ninaomba ieleweke kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 67 inasema hakuna Mbunge atakuwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pasipokuwa na chama cha siasa, pasipokupendekezwa na chama cha siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru CCM kwa kunipendekeza na kuniteua kuwa mgombea, lakini pia kupewa kura nyingi na akina mama wa Mkoa wa Rukwa. Kwangu mimi ni heshima kubwa sana. Kwa unyenyekevu mkubwa sana ninawashukuru wanawake wa Mkoa wa Rukwa kwa heshima kubwa ambayo walinipatia. Ahadi yangu kwao, kaulimbiu yangu ni ile ile, “Maneno Kidogo na Vitendo Vitaongea Zaidi.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninatumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wote ni mashahidi, Waziri Mkuu wa Tanzania ameanza na mguu mzuri, na sisi tumemwona akizunguka kwenye mikoa mbalimbali kusikiliza kero za wananchi, na hilo ndilo wananchi wanalolitaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nifikishe salamu za Wanarukwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wanarukwa wanamshukuru sana na wanamkaribisha tena na tena. Karibu sana Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitajikita ukurasa wa 29 kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, amezungumzia Sekta ya Uvuvi. Hapa kwa dhati ya moyo ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha inainua uvuvi katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niko hapa nikiwawakilisha wavuvi wa Mkoa wa Rukwa na wavuvi wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Wamenituma niseme yafuatayo: - (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika na wavuvi wa Mkoa wa Rukwa wana masikitiko makubwa sana. Wana maumivu makubwa sana kwa sababu Ziwa Tanganyika ni kama limesahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata nafasi ya kufanya ziara kwenda kuongea na wavuvi, na katika malalamiko yao waliyonipatia ni namna ambavyo rasilimali za nchi hii, au jinsi ambavyo keki ya Taifa ya nchi hii inawaneemesha watu wengine na kuwasahau wavuvi wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hatuba yake amesema, Serikali imetoa boti 219 kwa ajili ya wavuvi wa Tanzania. Kwa masikitiko makubwa, kati ya boti 219, boti ambazo zimekwenda Ziwa Tanganyika ni boti 16 tu. Ninavyoongea hivi, kati ya boti 16, boti ambazo zimekwenda Mkoa wa Rukwa ni boti tatu tu, lakini boti ambazo zimekwenda Mkoa wa Katavi ni boti moja. Wavuvi wanasema hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalinganisha siyo kwa sababu ya nia mbaya, hapana, lakini wavuvi hao wanafuatilia taarifa na wakati Waziri Mkuu anasoma kwamba Serikali imetoa boti 219 wavuvi wa Mkoa wa Rukwa wanaeleza wao boti tatu zinawakwamua vipi kwenye umaskini walionao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nisome ili tunapozungumzia Ziwa Tanganyika, sisi Wanarukwa ndiyo maisha yetu. Ziwa Tanganyika kwa sisi Wana-Rukwa, watu wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika, siyo maji tu, Ziwa Tanganyika ni uchumi, ni ajira, ni fursa, na ndiyo limeshikilia uchumi wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Rukwa wakiwemo akina mama ambao ni wafanyabiashara wakubwa wa mazao ya uvuvi wanasikitika sana kwa namna ambavyo Serikali imewaweka nyuma kwenye kugawa keki ya Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na mijadala mbalimbali hapa ya kufunga Ziwa Tanganyika, na Wabunge huwa wanasema Ziwa Tanganyika lifungwe. Hili ni jambo ambalo linatuumiza Wanarukwa kwa sababu kwenye ugawaji wa vizimba na hapa nitaomba niseme, ukienda Ziwa Victoria kuna vizimba 507, lakini ukija Ziwa Tanganyika kuna vizimba 29 tu, na hivyo vizimba 29 vizimba ambavyo viko Mkoa wa Rukwa ni vizimba viwili tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Rukwa tuna zaidi ya wananchi 1,540,000 ambao maisha yetu tunategemea Ziwa Tanganyika. Tumekuwa Wabunge hapa tukisema tunatamani kuona Ziwa Tanganyika linafunguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia Ziwa Tanganyika limepakana na nchi nne. Kwetu sisi tunachukua Ziwa Tanganyika kama fursa; tunaziona ajira, tunaona usafirishaji, lakini Ziwa Tanganyika ni giza. Tuko hapa tunapanga mipango ya 2050, lakini kama hatutaliingiza Ziwa Tanganyika na kulifungua bado tutaendelea kukwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongea haya kwa sababu tunaumia. Leo unaposema tunafunga Ziwa Tanganyika, na bado hatuna mbadala wa kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi maisha yao, tunawatesa wananchi bila sababu. Kwa vizimba viwili huwezi kufunga maisha ya watu 1,500,000. Hiyo siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wavuvi wa Ziwa Tanganyika wamenituma niiombe Serikali kuangalia namna bora ya kugawanya keki hii ya Taifa, kuangalia namna bora ya kuona uwekezaji katika Ziwa Tanganyika unakuwa wa kiwango kile ambacho Ziwa Tanganyika linalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona umewasha mic. Ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Hivyo basi, ninaomba niiache Serikali kwa maneno haya ninayoyasema. Sisi wananchi wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika ni Watanzania, na rasilimali za nchi hii na sisi zinatuhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali yetu sikivu ione namna bora ya kufungua Mkoa wetu wa Rukwa, ione namna bora ya kufungua Ziwa Tanganyika. Tuna imani kubwa giza lililoko kwenye Ziwa Tanganyika likiondolewa, tukipata meli za kusafirisha na meli za uvuvi tutaenda kujikwamua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)