Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyenijalia afya na uzima na kunipa kibali cha kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu kuweza kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyekiti wangu wa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Kamati Kuu kwa kuweza kuniteua kuwa Mgombea wa Jimbo la Itwangi. Nitumie fursa hii pia kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Itwangi kwa kuweza kuniamini ili niweze kuwawakilisha ndani ya Bunge. Ninawaahidi nitawawakilisha vyema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambazo anazifanya. Naomba kumtia moyo Mheshimiwa Rais, kazi kubwa anazozifanya, Watanzania tunaziona, Wananchi wa Jimbo la Itwangi wanaziona. Mwenye macho haambiwi tazama, kazi zinaonekana. Tuko pamoja naye, tutahakikisha Watanzania wanakwenda kupata maendeleo kama ambavyo kiu yake inatamani kuwafanyia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika Jimbo langu la Itwangi ambako ndiko ninapowawakilisha wananchi walionileta ndani ya Bunge hili. Ninaishukuru pia Serikali kwa fedha ambazo imetuletea kwa ajili ya barabara zetu ambazo zimekatika na kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, kuna barabara ilikuwa imekatika, ilikuwa haina mawasiliano, ametupatia fedha, mkandarasi yuko site, na sasa hivi barabara ile ya Usule – Buchama iliyopo ndani ya Jimbo la Itwangi inatengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninawashukuru sana TARURA kwa maana ya kwamba kuna barabara ambazo zilikuwa zimekatika hatukuwa na makalavati, lakini sasa makalavati yamepatikana, fedha imetengwa, na makalavati yale yanakwenda kuwekwa, na mkandarasi yuko site. Ninaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaishukuru sana Serikali kwa sababu kuna shule ambazo katika Jimbo langu zina msongamano mkubwa wa wanafunzi. Shule hizo miongoni mwao ni Shule ya Msingi Tinde A na B. Serikali imetujengea shule mpya kwa maana ya kuwa na Tinde B Shule ya Msingi ambayo mwezi huu inakwenda kufunguliwa rasmi. Tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Itwangi tuna maboma mengi ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi, yanahitaji ukamilishwaji. Maboma hayo ni maboma ya zahanati, maboma ya shule za msingi na shule za sekondari. Ninaiomba Serikali itambue nguvu za wananchi zilizowekwa pale kwenda kuhakikisha kwamba tunakwenda kukamilisha maboma yale na wananchi wa Jimbo la Itwangi waweze kupata huduma zilizo bora za vituo vya afya, zahanati na katika shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mfano mdogo tu. Katika Jimbo la Itwangi nina vijiji 58, nina kata 14, zahanati 23 tu zinazofanya kazi, na pia nina maboma 14 ambayo yanahitaji ukamilishwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba tena Serikali kwenda kuhakikisha kwamba wanatupatia fedha kwenda kukamilisha maboma haya ya zahanati yalioanzishwa na nguvu za wananchi. Nitatoa mfano kidogo tu wa maboma hayo. Kuna boma lipo Kijiji cha Chaburuba, Imesela, Bunonga, Mwamkanga, Masunura na mengine yote kutimiza vijiji 14. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo letu la Itwangi kuna shule ambazo zina msongamano mkubwa wa wanafunzi. Shule hizi zinahitaji kugawanywa ili wanafunzi waweze kusoma vizuri na walimu waweze kufundisha vizuri katika shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hizi zenye idadi kubwa ambazo naomba ziende zikagawanywe na TAMISEMI ni Shule ya Msingi Didia, Shule ya Msingi Ihalo, Shule ya Msingi Shingita na Shule ya Msingi Bubale. Ukifika katika shule hizi wanafunzi ni wengi. Shule moja inachukua wanafunzi 1,700 mpaka 2,000. Ukiangalia kiuhalisia hata walimu utendaji wao wa kazi unakuwa ni mgumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Itwangi kuna shule zilizochakaa, hazifai, kwani majengo yake yamechoka. Ninaiomba Serikali ituangalie na kwenda kutujengea majengo mapya katika shule hizi: Shule ya Msingi Didia, Shule ya Msingi Manyada, Shule ya Msingi Jida na Shule ya Msingi Kihongwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Itwangi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, miundombinu ya barabara imeharibika, madaraja mengi yamekatika, yamebomoka na hakuna mawasiliano. Ninaiomba sana Serikali, na TARURA, hakuna mawasiliano ndani ya Jimbo langu. Nimeshaenda ofisini kwake, nimesema sana, na mpaka sasa hakuna mawasiliano kutoka kata moja kwenda kata nyingine na kutoka kijiji kimoja kwenda kijiji kingine. Nashukuru kwa kile nilichopewa, lakini asilimia kubwa bado hakuna mawasiliano ndani ya Jimbo la Itwangi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana tuangalie barabara inayounganisha Jimbo la Itwangi na Jimbo la Manonga, Wilaya ya Igunga. Kutoka kijiji cha Ikonda kwenda kijiji cha Mwamashiku kuna daraja kubwa, kuna mto mkubwa wa Manonga unaopita pale. Kila inapofika masika, wananchi wetu wanakosa mawasiliano kwa kukosa daraja la kuweza kuwatoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri aiangalie sana barabara hii ili kuweza kutuunganisha wananchi wa Jimbo la Itwangi na wananchi wa Jimbo la Manonga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Itwangi kuna daraja kubwa la Butini na Nsalala limebomoka na limekatika, na lina zaidi ya miaka mitatu leo, hakuna mawasiliano kabisa. Katika kata hizi mbili ndipo kunapozalishwa asilimia kubwa ya mpunga unaotoka Shinyanga. Wananchi wanashindwa kusafirisha mazao yao kwa sababu hakuna mawasiliano. Ninaiomba sana Serikali yangu sikivu ituangalie kwenda kutujengea madaraja hayo yaliyokatika na kutengeneza barabara zetu ili ziweze kupitika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba pia katika Jimbo la Itwangi kuna barabara inaitwa Didia – Solo. Kutoka njia panda ya Luhumbo kwenda Didia Center ni kilometa tano tu. Mji huu wa Didia ndiyo Mji unaokua kwa kasi katika Jimbo la Itwangi. Wafanyabiashara wote wa mchele, mashine zote za mchele ziko kwa center hii kubwa ya Didia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika center hii kubwa ya Didia ndipo ambapo kunajengwa stesheni ya SGR. Ombi langu kwa TARURA ni kwenda kukijenga kipande hiki cha kilometa tano kutoka njia panda ya Luhumbo kwenda center ya Didia kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua hakuna kinachoshindikana. Center hii ndiyo inayoipatia Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mapato kwa kiasi kikubwa. Ninaomba sana hata kwa awamu mkitenga hata awamu mbili kilometa hizi tano haziwezi kushindikana kwenda kuwekewa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, katika miradi ya TARURA ambayo ilikuwa imeshatangazwa ndani ya Halmashauri ya Shinyanga na hususan katika Jimbo la Itwangi, basi wapewe vibali ili kazi hizo ziende zikatekelezwe kwa sababu barabara hazipitiki kabisa. Nina imani Mheshimiwa Waziri ananisikia na atakwenda kulifanyia kazi…

MWENYEKITI: Ahsante…

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia RC wangu kwa kazi kubwa anayoifanya, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)