Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia bajeti hii. Kwanza ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri inayofanywa kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza sana Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Taifa letu. Tumekuwa tukimwona maeneo mbalimbali na wananchi wanamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Ofisi ya Waziri Mkuu. Ofisi ya Waziri Mkuu ina mifuko na programu za uwezeshaji 75 ambazo zinasimamiwa na Serikali na Sekta Binafsi na katika mifuko hiyo, mifuko 72 ni mifuko inayosimamiwa na Serikali. Tatizo ni kwamba huku mtaani taarifa hizi hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanufaika wa mifuko hii na hususan hawa wajasiriamali, akinamama, vijana na watu wenye ulemavu hawana taarifa na hii mifuko. Mtaani mfuko ambao almaarufu unajulikana ni mmoja tu, wa 10% na ndiyo maana kumekuwa na foleni kubwa sana kule kuliko kwenye hii mifuko na fursa nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku mitaani changamoto siyo fursa. Fursa wananchi wanaishi nazo kila siku. Changamoto ni mitaji, nani anayewajibika kusimamia mfuko huu na kuhakikisha taarifa zinakwenda chini, zinawafikia wananchi? Tuna kundi kubwa la vijana wamemaliza vyuo, wana elimu ya darasani, wanashindwa kufanya vitendo kuingia kwenye ujasiriamali kwa sababu ya kukosa mitaji. Ni nani anayewajibika kuhakikisha taarifa hizi zinashuka chini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mifuko hii ijulikane huko chini ili wananchi wakanufaike nayo. Ukiangalia kwenye makaratasi, kuna mipango mizuri sana. Ukipitia kwenye ripoti unaona kabisa kwamba sasa tatizo limekwisha, lakini kwenye utekelezaji hakuna, hatuoni tija, hatuoni matokeo na mafanikio ya mifuko hiyo huku mtaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu shilingi bilioni 200 zilizotolewa na Mheshimiwa Rais. Fedha hizi wakati zinatangazwa na kunadiwa wakati wa kampeni, wananchi walishukuru sana na waliamini sasa wanakwenda kumaliza changamoto zao zote. Fedha hizi zimekwenda kwenye Wizara tano za kisekta, ni jambo zuri na ninaipongeza Serikali kwa kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu zote zingeenda Wizara ya Vijana kungekuwa na urasimu, lakini pia kungekuwa na vurugu mechi nyingi sana. Kwa hiyo, kitendo cha Serikali kuona kwamba hizi fedha ziende kwenye Wizara tano, ni kitu kizuri na kila Mkoa una wanufaika katika hizi Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukulia Mkoa wa Dar es Salaam unaweza kusema, vijana wanaweza kusema labda sisi tunanufaika nini na mambo ya kilimo? Dar es Salaam wapo wakina mama na vijana wanalima mbogamboga. Ukiacha Mkoa wa Arusha ambao unalima sana mazao ya maua, Mkoa wa Dar es Salaam vijana wengi wanalima kilimo cha maua pembezoni mwa barabara. Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi mnakuja Dar es Salaam na mnaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara hiyo hiyo ya Kilimo tunaona mazao mengi sana yanakuja kuuzwa Dar es Salaam. Dar es Salaam ndiyo kwenye soko kubwa. Wale wanaoleta mazao siyo wakulima, mkulima yuko huko mkoani shambani. Kuna vijana na wakina mama wana vikundi, wana uwezo wa kufuata yale mazao shambani wakayaleta Dar es Salaam na wakauza kwa bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba taarifa ya hii mifuko na hizi fursa ishuke chini. Huku chini bado hata hao vijana wenyewe bado hawafahamu wanawezaje kupata fursa hii? Bado hawafahamu. Siyo kila kijana, siyo kila mtu mwenye ulemavu na siyo kila mama mjasiriamali ambaye anatakiwa kunufaika na fedha hizi ana smartphone na kuona kwenye mitandao ya kijamii, kuna wengine wanatumia simu za tochi, wanapataje taarifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Ofisi za Watendaji wa Kata wapelekewe taarifa za Wizara zote fursa hii ipoje? Upatikanaji upoje? Zinaombwaje? Utaratibu wote upoje? Mtu badala ya kutoka aanze kutafuta kwenye mitandao ya kijamii, aende wilayani, au aende kwenye Ofisi ya Kata, kwa Mtendaji wa Kata apewe kipeperushi cha kila Wizara aangalie nature ya shughuli yake anayofanya inaendana na fursa ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hapa tunapoongea bado kuna kundi kubwa sana hawaelewi hizi fursa. Hii ya shilingi bilioni 200 wanaipataje? Bado hawaelewi. Pale pale Dar es Salaam kuna vijana ambao wanadhani kwamba ni lazima wawe content creator ndiyo wapate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Wizara ya Michezo angalau imejiinua na kutangaza sana, lakini siyo vijana wote wanafanya hii content creators. Kuna wakina mama wanafanya shughuli za kutunga mashairi, kuandika vitabu, kutengeneza bidhaa za utamaduni, wanatakiwa wanufaike na mfuko huu. Siyo vijana peke yao, lakini nani anawapelekea taarifa? Mafunzo ya kupata hii mikopo au hizi fursa nani anayewajibika kwenda kuwaeleza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hata halmashauri zetu huku wilayani Mabibi Maendeleo wanapokutana na hawa wanufaika wa mikopo wawaeleweshe na hii. Sababu kuna watu ambao wapo huku chini upataji wao wa taarifa ni changamoto mpaka muda unafika wanakuja kuelewa kwamba hata wao ni wanufaika wa hii mifuko, hii fedha itakuwa imekwisha. Fedha hii italeta tija na itaonekana ina thamani kama itaweza kuingia kwenye mikoa yote na ikaweza kunufaisha makundi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mikopo ya 10%. Lengo la mikopo hii ilikuwa ni nzuri sana, lakini tija mtaani bado haionekani. Leo hii kikundi kimeshajisajili, kimeshafikiwa, kinapewa mafunzo ili kipate hiyo mikopo. Mafunzo ya siku mbili hayatoshi kumfanya mtu akachukue ile hela kwenda kuizalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweke nguvu kubwa kwenye kuwafundisha watu wapate elimu ya fedha, wapewe macho zaidi ya kuziona fursa zinazowazunguka. Pia fedha hizi zinatakiwa zikopwe na zirudi ili watu wengi waweze kunufaika nazo. Hizi fedha siyo msaada inatakiwa zizunguke, lakini tumeona vikundi vingi vimeweza kupewa hizi fedha vimeshindwa kurudisha (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie namna nyingine ya kuonyesha tija ya hizi fedha kwenye mitaa huko chini. Kwa nini sasa Serikali isiangalie namna ya kupitia hizi fedha kuanzisha miradi ya kimkakati hata viwanda vidogo vya wakinamama, vijana na watu wenye ulemavu? Itaonekana tija na thamani ya hii fedha, na pia tutatengeneza ajira na malengo ya hii fedha yataonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda halmashauri, tunakuta kwenye taarifa kwamba kuna mafunzo yanatolewa kwa vikundi, lakini kuna shida gani mafunzo yale Wabunge wasishirikishwe hata Madiwani? Leo hii Bibi Maendeleo yupo wilayani, ni kweli anaweza kuvisimamia vikundi vyote wahakikishe hela wamerudisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anapokuja kiongozi mkubwa kwenye mkoa wako, anaenda kwenye kata fulani, labda kuna mradi anaosimamia, akitoa nafasi hata watu watatu tu waeleze changamoto, lazima akutane na manung’uniko ya mikopo ya 10%. Kiongozi anaomsimamisha Mbunge au Diwani kwamba naomba kujua hii mikopo imekuwaje? Mbunge hana taarifa, wala Diwani anayeishi nao wale watu kwenye Kata, hana taarifa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Diwani wa Viti Maalum wa Kata ndio mtu wa kwanza anatakiwa kujua kwenye kata yake vikundi vingapi vimepata mikopo? Wanafanya shughuli gani? Kwa nini hawarejeshi? Wale ndio watakaosaidia mikopo hii iweze kurudi, lakini Diwani hashirikishwi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ya pili imegonga…

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)